Home Kitaifa Diallo: Serikali Hacheni Kuingilia Uchaguzi wa CCM

Diallo: Serikali Hacheni Kuingilia Uchaguzi wa CCM

by Jamhuri

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo, ambaye mwishoni mwa wiki alipekuliwa na maofisa wa Takukuru, ameitaka Serikali kutoingilia masuala ya uchaguzi wa chama hicho, badala yake iangalie na kuwaongoza wanapokosea.

Diallo alitoa kauli hiyo juzi usiku wakati akiwashukuru wajumbe wa CCM waliomchagua kwa mara nyingine na kusema umefika wakati chama kitafute utaratibu mahsusi kwa viongozi wa kiserikali kuacha kuingilia masuala ya uchaguzi.
Kuna umuhimu wa kutengeneza kiapo kitakachosaidia Serikali kutoingilia masuala ya uchaguzi bali waangalie na kutuongoza pale tunapoenda kinyume, alisema.

Jumamosi, gari la Diallo, ambaye amefanikiwa kutetea kiti chake, lilisimamishwa na maofisa wa Takukuru na baadaye kupekuliwa kabla ya kumuachia aendelee na shughuli za kampeni za uchaguzi wa viongozi wa CCM.

Maofisa hao walipekua gari lake wakati waziri huyo wa zamani akiwa wilayani Ukerewe.

Kitendo cha gari yangu kusimamishwa na maofisa wa polisi na kuanza kupekuliwa hakijanifurahisha kwani hata mimi najua rushwa ni adui wa haki, alisema Diallo, ambaye ni mfanyabiashara maarufu anayemiliki vyombo vya habari.

You may also like