Halo! Ni matumaini yangu kuwa uko hewani na unanisikia mheshimiwa. Nakuomba univumilie nimejiunga na mtandao wa Jamhuri kwa kuwa Voda, Tigo, Airtel na Zantel wameniambia salio langu halitoshi kuniwezesha niwe hewani kwa muda niutakao.

Najua mheshimiwa, simu yako iko hewani saa ishirini na nne, kwa kuwa wewe ni miongoni mwa watumishi wachache wanaojishughulisha na kazi za kutatua kero za wananchi mbalimbali bila kujali nafasi zao katika jamii.

 

Nasikia hapo bandarini mizigo haizagai ovyo tena na wala haina nafasi kupumua. Makontena siku hizi hayana muda wa kusubiri, mihuri iliyofungiwa kwenye ofisi ya bosi fulani ambaye amezoea kupokea kitu kidogo ndipo apitishe vibali sasa inapatikana. Nasikia kuna mfumo wa Electronic Cargo Tracking Note System (ECTN). Mambo yanakwenda barabara!

 

Mheshimiwa, nakupongeza sana kwa jitihada zako. Nasikia hapo bandari kuna babu zetu walishasahau kuwa wamefikisha umri wa kustaafu, ila ulipofika na kuwakuta, baada ya muda mfupi ukaagiza wapelekewe kimemo. Walipofungua wakakutana na maneno haya, “Retired Officers, why are you still here?”

 

Mheshimiwa, nasikia virago vikakusanywa haraka haraka. Maswahiba wakaanza kulalamika. Kelele zao hazikusaidia kitu. Sasa mambo safi.

 

Mheshimiwa, nimeongea kifasihi kidogo, nisije nikakukwaza. Nazungumzia mageuzi makubwa ya uongozi uliyoyafanya hapo bandarini, watu walishapageuza kwao, wakawa wanafanya wanavyotaka, wizi mchana-mchana. Nakumbuka ulivyowanasa wale polisi na mizigo ileee siku ileee. Sijui wako wapi kwani sikufuatilia sana lile sakata lao. Najua utakuwa ulishawaadabisha. Huna utani linapokuja suala la kitaifa.

 

Halo! Mheshimiwa, usikate simu najua kuna makabrasha yapo hapo mezani inabidi uyapitie na kutoa baraka zako lakini nataka nikudokezee hili mheshimiwa. Nakumbuka ulipokabidhiwa mikoba ya wizara hiyo nyeti uliyonayo, ulifanya ukaguzi kwenye mabasi ya daladala ukagundua kuwa nauli zinazotozwa si halali. Nakumbuka ulisema utalifanyia kazi. Sasa mheshimiwa, kitendo chako kilikuwa kama ni kutoa ruhusa kwa wenye magari kufanya wanavyotaka.

 

Mheshimiwa, ninavyozungumza na wewe sasa hivi nipo Kariakoo. Ni saa 9:30 nasubiri usafiri wa kwenda Mbezi. Abiria ni wengi kweli kweli. Magari ya Kimara na Mbezi si mengi sana hapo stendi jirani na Kituo cha Polisi Msimbazi. Mabasi mengi yanayokuja ni ya Kariakoo-Ubungo na Mwenge- Ubungo.

 

Najaribu kuuliza kwa wapiga debe, mmoja ananiambia mabasi ya Kimara na Mbezi yanageuzia kwa Bakhresa. Hayafiki kituo cha mwisho. Kijana huyu ananiambia kuwa sasa kutoka Kariakoo hadi Mbezi kwa kugeuza ni Sh 1,000 wakati nauli halali ni Sh 500.

 

Kwa kuwa abiria wenyewe ndiyo wanaogombea hakuna anayelalamika, kwa kuwa wengi wanaishi mbali na jiji lazima waondoke tu. Madereva na makondakta wameona ni bora wavunje sheria. Polisi wa Msimbazi sijui kama hilo la kugeuzia njiani wanaliona au la.

 

Halo! Mheshimiwa, wakati naambiwa hayo kuna Hiace na Noah zimekuja hapa, nauli zinazotangazwa ni Sh 2,000. Mpiga debe anaongeza buku (Sh 1,000) inakuwa Sh 3,000. Naona mwenye gari mmoja anatabasamu, anawatazama abiria na kisha anaruhusu waanze kuingia.

 

Mheshimiwa, nilidhani magari haya hayatapata watu. Lo! Mheshimiwa, yote yanajaa tena kwa watu kukanyagana, ila mheshimiwa, kuna kijana mmoja nasikia analalamika hapa anasema yeye afadhali atembee kwa miguu hadi Mbezi kuliko kulipa Sh 3,000. Anasema hajauza kiwanja Masaki na wala hana hicho kiwanja. Kapewa nauli na mdosi wake Sh 1,000 ya kurudi nyumbani Sh 500 na kuja kazini kesho yake Sh 500.

 

Nadhani mheshimiwa, umenielewa. Hapa nilipo kuna akina mama wana watoto. Kuna wengine wana mizigo. Hakuna ustaarabu hata kidogo.

Mheshimiwa, haya magari binafsi yamepewa na nani kibali cha kuja vituoni na kutukamua kiasi hicho? Serikali na Sumatra wamepanga bei ambazo tumezikubali shingo upande, japo si kubwa sana. Sasa hawa wenzetu wameanzia Sh 2,000 hadi Sh 3,000 Kariakoo-Kimara au Kariakoo-Mbezi!

 

Hawa wa taxi sina tatizo nao sana, maana wao ndiyo biashara yao. Wanachokifanya ni kutoza Sh 1,500 kwa kila abiria kutoka Kariakoo hadi Ubungo. Akipata abiria wanne wanamtosha.

 

Mheshimiwa, kilio changu ni hicho. Nauli, nauli, holela. Tusaidie mheshimiwa, umetuwekea treni lakini tuko wengi hapa mjini. Treni hazitoshi, wengi wanasema stesheni mbali kutoka wanapofanyia kazi. Na kwa nini wasipande daladala?

 

Mheshimiwa, simu yangu bado ina salio isipokuwa chaji inakaribia kuisha. Natambua juhudi zako. Najua utafika mwenyewe ujionee hali halisi. Halafu hutapata shida ya kuwakamata hawa wanyonyaji kwa sababu polisi wapo jirani. Tena utawakuta wengine nyuma ya jengo lao wakipewa maagizo na maafisa kwa ajili ya kazi mbalimbali, watakusaidia.

 

Mheshimiwa, nakushukuru sana kwa kutumia muda mwingi kunisikiliza japo maelezo ya kwenye simu huwa hayapangiliwi vizuri sana, ila ukitaka nije ofisini kwako niko tayari, nikuletee taarifa iliyo kamili na sauti za wapiga debe wanavyong’ang’ania hizo elfu tatu-tatu, wananchi wanashindwa waende wapi, hawapendi ila wanaogopa kuchelewa kurudi nyumbani na kukabwa na vibaka.

 

Kilio hiki kiko kila kona, nenda kituo cha Mwenge-Buguruni, Kimara-Kariakoo/Posta, Mbezi-Kariakoo/Kivukoni utashuhudia haya.

 

Asante mheshimiwa, nakutakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yako na Mwenyezi Mungu aendelee kukupa afya njema.

 

0763 – 400283

[email protected]


By Jamhuri