Kwa mwaka Mtanzania hafanyi kazi kwa siku 140!

Makala yangu ya wiki iliyopita ya “Wakati mwingine Wakristo wanaanzisha chokochoko”, imepokewa kwa hisia tofauti na wasomaji wa safu hii.

Makala ililenga kupinga msimamo wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wa kutaka Jumapili isitumike kwa kura ya maoni inayotarajiwa kupigwa kama sehemu ya kupata Katiba mpya.

 

Hoja yangu ilikuwa kuwa madai haya, na yale ya kupinga siku hiyo kuwa ya Uchaguzi Mkuu hapa nchini, inaweza kuwafanya Waislamu nao kuibuka na madai ya kutaka Ijumaa ‘iheshimiwe’.

 

Wapo walionipongeza, lakini wengine wamekasirishwa. Nimepokea simu nyingi pamoja na ujumbe mfupi wa maandishi usiokuwa na idadi. Hisia za walionipinga zilikwenda mbali zaidi – wapo waliokosa uvumilivu wa kupambana na mimi kwa hoja, wakaishia kutoa maneno makali. Nilishangaa, hasa kuona kuwa wengine wakijitambulisha kuwa ni walokole na wachungaji! Sikushangaa kwa sababu leo hadhi ya uchungaji imeingia doa. Kumsikia mchungaji akitukana, akiiba, akisafirisha mihadarati, si jambo la kushangaza.

 

Najua sina nguvu za kuwazuia Watanzania wengi wapenda mapumziko kuona Jumapili ikiondolewa kwenye ratiba za mambo mengine, isipokuwa ibada kwa Wakristo. Lakini ni vema nikajiweka kando na unafiki unaoenezwa kuwa ibada zimekuwa zikitibuliwa kwa sababu ya Wakristo kushiriki uchaguzi Jumapili.

 

Hatari ya madai ya Wakristo naiona kwenye hatima ya umoja na mshikamano wetu. Kama nilivyosema, jamii lazima iishi kwa kuvumiliana. Kama Waislamu wanaweza kuvumilia mambo fulani fulani, Wakristo nao wanapaswa kufanya hivyo. Wapo waliotoa hoja dhaifu wakisema mbona Kenya au Zimbabwe uchaguzi mkuu wao unafanywa siku za katikati ya wiki.

 

Madai haya ni ya kichovu kwa sababu si kila kinachofanywa huko kwingine, basi lazima kifanyike Tanzania. Ndiyo maana wachungaji hao hao, kwa kutambua kuwa Ulaya na Marekani wameruhusu madume kuoana, hapa kwetu wamepinga kwa nguvu zote. Hii inatosha kukubali kuwa si kila linalofanywa huko kwa wenzetu, tunapaswa kuliiga.

 

Mmoja wa wasomaji nilimwuliza swali ambalo hajanipa jibu. Nilimwuliza kwamba Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa Mkatoliki, ndiye tangu mwaka 1965 alipobariki Jumapili ya mwisho wa mwezi Oktoba iwe siku ya uchaguzi mkuu. Ukatoliki wa Mwalimu haukuwa na shaka, ndiyo maana zinafanyika juhudi za kumtangaza Mwenyeheri. Aliijua Biblia kiasi kwamba kaandika vitabu, mashairi, tenzi na mambo mengine mengi kutoka katika Biblia. Mbona hakuwa na kikwazo kwa Jumapili kuwa siku ya uchaguzi mkuu?

 

Wakristo na Waislamu ni kama watoto wa familia moja. Kwenye familia hiyo, mtoto mmoja anapoibua madai ya kununuliwa kitu fulani, mara nyingi yule mtoto mwingine naye atataka anunuliwe. Ndiyo maana wakati wa sikukuu utaona familia zikihangaika kununua nguo kwa watoto wote.

 

Vivyo hivyo, inapotokea Wakristo wakashinikiza jambo fulani, hata kama kufanyika kwake hakuwezi kuwakosesha ‘kuingia mbinguni’, haitashangaza Waislamu nao wakaibua madai yao. Ikiwa kwao ni halali kutaka Jumapili isiguswe, kwanini iwe haramu kwa Waislamu kutaka Ijumaa isiguswe? Wasabato watakuwa na kosa gani kutaka Jumamosi isiguswe kabisa? Tukiamua hivyo, kuwa Ijumaa, Jumamosi na Jumapili zisiguswe, Taifa hili litakuwa la aina gani?

 

Tatizo jingine ninaloliona hapa Tanzania, ni watu kupenda sana mapumziko. Wenye umri kama wangu watakumbuka kuwa zamani wanafunzi tulisoma Jumatatu hadi Jumamosi saa sita mchana. Wafanyakazi katika ofisi za umma walikwenda kazini hadi saa 6 au saa 6:30 mchana kwa Jumamosi. Utaratibu huo ulifutwa baadaye na tukawa na Jumamosi na Jumapili za kupumzika.

 

Kosa jingine likafanywa na uongozi wa awamu ya pili. Nalo likawa kuwa inapotokea sikukuu yoyote ya kitaifa imeangukia Jumamosi au Jumapili, ifidiwe kwenye siku ya kwanza ya juma! Huu ulikuwa uamuzi wa ajabu sana.

 

Taifa masikini kimaendeleo kama Tanzania, watu wake hawapaswi kupumzika kwa staili hii. Tunapaswa kufanya kazi usiku na mchana. Ulaya, Marekani, Asia na kwingineko ambako wameendelea, hawalali; seuze sisi!

 

Nimepitia kalenda ya mwaka huu wenye siku 365. Kati ya siku hizo, siku ambazo Watanzania wanapaswa kisheria kuwapo ofisini ni 226.  Tunapumzika hivi: Siku 104 ni Jumamosi na Jumapili za mwaka tunazopumzika. Siku 17 ni sikukuu kuanzia ya mwaka mpya hadi Sikukuu ya Zawadi. Siku 28 ni za likizo. Jumla ya siku tunazokuwa nje ya ofisi (kwa watumishi wenye ajira rasmi) ni 140 hivi!

 

Siku hizo 140 tunazopumzika, ni nje kabisa ya siku za udhuru! Kuhudhuria misiba ya majirani, ndugu na kadhalika. Hizo ni nje ya kitchen parties ambazo kwa kawaida zinafanyika katikati ya wiki! Siku hizo ni nje kabisa ya siku ambazo mtumishi anatega kwenda kazini kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo za ulevi na visingizio vingi.

 

Mapumziko haya makubwa hayahusishi saa ambazo mtumishi anakuwa ofisini. Anaweza kuchelewa kuingia ofisini, lakini mara moja akaenda kunywa supu; na kwa sababu ya ulevi, akisharejea ofisini atajifungia katika chumba na kuuchapa usingizi. Kwa vile walevi wengine wanaamini katika kuzimua pombe, wengine huwahi kutoka ofisini ili wapite baa.

 

Haya yote ni nje na utaratibu wa siku za Jumatatu na Ijumaa, siku ambazo kimsingi ‘si za kazi’. Kwanini si siku za kazi? Si siku za kazi kwa sababu Jumatatu tunaingia ofisini tukiwa tuna mawenge ya ulevi. Kazi hazifanywi vizuri.

 

Ijumaa tunaiita “siku ya lala salama”. Siku hii ndiyo inayotumiwa na wengi kukwepa kazi, wakiwa katika maandalizi ya wikiendi. Asiye na fedha, Ijumaa hakai ofisini. Huhangaika huku na kule alimradi apate cha kumwezesha kustarehe wikendi.

 

Kuhusu nini kianze kati ya starehe na kazi, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha ‘Ujamaa ni Imani (2)’, anasema: “Tunajidanganya sisi kufikiri kwamba tunaweza kuanza na raha halafu ndiyo tuendelee. Hata kidogo”.

 

Kama tunaweza kufanya kazi mchana pekee, kisha usiku tukawa ni watu wa kupiga soga na kulala, kamwe hatuwezi kuendelea.  Kwa mfano, kuna sababu gani sasa ya msingi ya kuyazuia mabasi kusafiri usiku? Usiku ungeweza kutumiwa vizuri sana kwa wafanyabiashara wanaotumia magari hayo.

 

Mathalani, mfanyabiashara anaweza kuondoka Arusha jioni, alfajiri akawa ameshafika Dar es Salaam. Duka likafunguliwa akiwapo. Mchana kutwa akafanya shughuli za ununuzi, kisha jioni akalala ndani ya basi akirejea Arusha. Hii maana yake ni kuwa mchana atakuwa ametekeleza wajibu wake, na usiku inakuwa zamu ya dereva na wasaidizi wake kufanya kazi. Ndivyo nchi inavyojengwa.

 

Hatuwezi kupata maendeleo kama tunapumzika nusu nzima ya mwaka! Mapendekezo yangu yako wazi. Jumamosi iwe siku ya kazi kama kawaida. Kuna sikukuu za kiimani ambazo haziwezi kubadilishwa.

 

Warusi wanao utaratibu mzuri. Siku za sikukuu zinazoangukia siku za kazi, hupumzika, lakini huzifidia kwa kuongeza muda wa kufanya kazi katika siku nyingine. Nasi tufanye hivyo.

 

Tukitekeleza madai ya Wakristo ya kuongeza siku nyingine ya mapumziko, tutakuwa tunajichimbia kaburi ya maendeleo. Tusiwe watumwa wa fikra. Huko Ukristo ulikoanzia wameendelea. Hawana utitiri wa siku za mapumziko kama tulivyo sisi. Wao wanachapa kazi usiku na mchana. Matokeo yake ndiyo haya ya sisi kwenda kuhemea kwao. Hapa makanisa yetu hayajiendeshi bila misaada yao. Utajiri haukuwashukia tu kutoka mbinguni, bali ni kwa kusali na kuchapa kazi.

 

Hatuna sababu ya kuwa na Nyerere Day na Karume Day. Tunaweza kuwa na Waasisi Day (au jina lolote) inayoweza kuwajumuisha mashujaa hao na wengine wengi waliohangaika kwa ajili ya kuwakomboa Watanzania. Sikukuu ya Wakulima haina sababu ya kusherehekewa hata na watu wasio wakulima! Pamoja na umuhimu wa wakulima, dhima ya kusherehekea mafanikio yao iwe yao.

 

Ndugu zangu, maendeleo ya dunia yanakwenda kasi mno. Ulaya, Marekani na Asia pamoja na kuwa wana maendeleo makubwa, hawapumziki. Wanafanya kazi kwa shift kwa saa 24. Wafanyakazi wanalipwa kwa saa wanazofanya kazi. Hawalipwi kwa mwezi kama hapa kwetu.

 

Tunapaswa kuanzisha utaratibu wa kuwalipa wafanyakazi kwa saa wanazofanya kazi. Hatua hiyo itapunguza udhuru, utoro, uzembe na visingizio vingi kutoka kwa wafanyakazi. Tukilipana kwa saa hakuna atakayeunga mkono utitiri huu wa mapumziko. Wakristo wataingia makanisani na wakimaliza misa watakwenda kazini!

 

Dunia ya leo maisha ya mtu yeyote asiye mlemavu yanatokana na bidii yake kwenye kazi. Hiyo ndiyo fomula ya utandawazi na ubepari. Hapa kwetu yameanza. Leo Kariakoo ina watu wanaojibidiisha kwa saa zote 24. Hawalali maana wanajua maisha bora kwao yatatokana na juhudi zao, na si kwa kutaka kuongezwa siku za mapumziko. Hao wakisia siku ya uchaguzi inawekwa katikati ya wiki, watanuna, nami nasema nitawaunga mkono.

 

 

1117 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!