Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Paje
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema chama kitaendelea kusimamia na kulinda misingi ya amani, umoja na mshikamano ambayo imeiwezesha Zanzibar kufikia mafanikio makubwa ya maendeleo katika miaka mitano iliyopita.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika Paje, Mkoa wa Kusini Unguja siku ya Alhamisi Oktoba 16, 2025, Dk. Mwinyi amesema sera kuu ya CCM imejikita katika kudumisha misingi hiyo mikuu ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.
Amesema katika miaka mitano iliyopita, Zanzibar imepiga hatua kubwa za kimaendeleo kutokana na mazingira tulivu na maridhiano ya kisiasa yaliyopo.
“Mpaka sasa hivi katika miaka mitano iliyopita tumekwenda vizuri, nchi yetu ina amani, ina umoja, mshikamano, na hata tuna maridhiano ya kisiasa. Hii imesababisha mambo mengi ya kimaendeleo kufanyika kwa sababu ya amani tuliyokuwa nayo,” amesema.
Dk. Mwinyi amewaomba Wazanzibari wote kuendelea kulinda na kudumisha amani iliyopo, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana katika mazingira ya mifarakano na ubaguzi.
Mbali na kuzungumzia masuala ya amani na umoja, Dk. Mwinyi ameahidi kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta ya miundombinu ya usafiri na usafirishaji, hasa Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwemo ujenzi wa mradi mkubwa wa barabara ya njia nne kutoka Tunguu hadi Makunduchi, mradi ambao utaufungua mkoa kiuchumi na kiutalii.
Amesema Serikali yake pia itahakikisha ujenzi wa madaraja mawili makubwa katika maeneo ya Kusini Unguja, yatakayorahisisha usafiri na kuongeza fursa za biashara na uwekezaji.
