DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, ameagiza waombaji na washindi wa mnada wa vitalu vya uwindaji wa kitalii kuhakikisha wana dhamana ya benki kabla ya kukabidhiwa vitalu.

Dk. Ndumbaro ametoa maagizo hayo kwa Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Misungwi, alipozungumza na wahariri jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Waziri alitoa maelekezo hayo ikiwa ni majibu yake kwa swali aliloulizwa kuhusu uwepo wa ‘bank guarantee’ kwa wanaopewa vitalu kama njia ya kuwazuia waliovipata kuvitelekeza baada ya kuvuna faida.

“Hili suala ni zuri sana. Mabuka umesikia, vitalu wanaviharibu halafu wanavirudisha, sasa hii bank guarantee itafanya kazi hiyo, kwa hiyo ni wazo zuri ambalo tumelipokea,” amesema Dk. Ndumbaro.

Waziri huyo alizungumzia pia kuwapo kwa madai ya kuchezewa kwa mfumo wa mnada wa vitalu kwa njia ya kielektroniki.

“Hili jambo na sisi tumelisikia sana. Kwenye mnada huu tukasema ebu tuweke mbele zaidi kulifanyia kazi. Tukaomba wenzetu wa e-Government waje. Ule mnada umekwenda kwa muda wa siku saba. Katika muda huo wa siku saba watu wa e-Government wame-monitor na wamesema hakuna kuingilia mfumo na wametuandikia ripoti kabisa. 

“Wangetuambia watu wa wizara tu tungesema (shaka), lakini watu wa e-Government ndio wana mamlaka ya kukagua na kudhibiti hii mitandao – wameridhika na ubora, wameridhishwa kwamba haukuingiliwa. Kama kuna ushauri tofauti tunaupokea,” amesema Dk. Ndumbaro.

Wakati waziri akisema hayo, JAMHURI limepokea taarifa kutoka kwa wadau walioshiriki mnada huo wakisema mfumo uliingiliwa ili kuwanufaisha wachache.

Wanatoa mfano kuwa baadhi ya waendesha mfumo walikuwa wakitoa siri kwa ‘watu wao’ zilizohusu kiwango kilichowekwa na washindani.

“Kwa mfano, ulipoweka kiasi cha dola 200,000 siri hiyo ilipelekwa kwa mtu wao na kutakiwa aweke dola 201,000. Ulipotaka kurudi na kuweka kwa mfano dola 250,000 system unakuta tayari haikubali kwa sababu imeshaingiliwa.

“Matokeo yake serikali imekosa fedha nyingi sana. Fikiria mtu anayeweka dola 200,000 anakataliwa na anachukuliwa aliyeweka dola 170,000. Tumemsikia waziri, lakini ajue ukweli kuwa mfumo wote umechezewa sana,” kimesema chanzo chetu.

Wanaolalamika wanasema mchezo mbaya ulikuwa kwenye vitalu vilivyo kaskazini.

“Tunashauri mnada wa vitalu vilivyo Umasaini urudiwe kwa sababu kule kuna wanyama wasiopatikana vitalu vingine nchini, lakini vimeuzwa kwenye mnada kwa fedha kidogo sana. Nakuhakikishia vikirudiwa kila kitalu kinaweza kununuliwa kwa dola 250,000 hadi 270,000. Vimeuzwa bei ya chini kwa sababu system ilikuwa tempered. Tunajua watu wana masilahi yao. Kuna vigogo wa TAWA wana ubia na baadhi ya walioshinda zabuni baada ya kuingilia mfumo wa mnada,” imeelezwa na vyanzo vyetu vya habari.

Aidha, kuna malalamiko kuwa kwenye mnada ilitangazwa kuwa wanaoshinda vitalu wanapewa siku 10 za kufanya malipo, lakini baadaye utaratibu huo umekiukwa na kuwapa muda hadi Oktoba, mwaka huu.

By Jamhuri