Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Bukoba
MBUNGE wa Jimbo la Bukoba Vijijini (CCM), Dk. Jasson Rweikiza, ametoa chakula kwaajili ya fukari kwa waumini wa dini ya kiislamu kwa Misikiti 113 iliyoko Wilaya ya Bukoba Mkoa wa Kagera.
Chakula hicho kilikabidhiwa mwishoni mwa wiki na msaidizi wa Dk Rweikiza, Jasson Lwankomezi, kwa Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Bakwata, Wilaya ya Bukoba, Ahmed Baitu, ambaye alipokea kwa niaba ya misikiti yote ya Wilaya hiyo.
Akizungumza kwenye makabidhiano hayo, Lwankomezi, alisema imekuwa kawaida kwa Mbunge huyo kutoa chakula cha futari kila unapofika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Tunaomba mpokeee futari kutoka kwa Dk. Rweikiza ambayo ameitoa kwa waumini wote wa Jimbo hili kwa hiyo kwa heshima kubwa naomba niwakabidhi na tutasafirisha mpaka kufika kwenye maeneo husika,” alisema
Akizungumza mara baada ya kupokea chakula hicho, Katibu wa Bakwata, Baitu alisema waislamu wamepokea kwa mikono miwili sadakata hiyo na kutoa shukrani kwa mbunge huyo kwa msaada huo ambao umekuja wakati mwafaka wakati huu wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
“Kwa dhati kabisa kwa niaba ya Wilaya yetu tunamshukuru sana mheshimiwa Mbunge na tunamwomba Mwenyezi Mungu amwongezee zaidi kwa wema huu aliouonyesha kwetu, tunamwomba Mungu amwongezee alipotoa na aendelee kumwongezea pale alipotoa,” alisema Katibu wa Bakwata.
Imamu wa Msikiti wa Katoma Wilaya ya Bukoba Vijijini, Yakub Abdalah, alisema msaada huo unaonyesha namna Mbunge huyo anayojali imani za wengine na kuiomba jamii kuishi kwa upendo wa namna hiyo.
“Unaweza kuwa na mali lakini usiwe na mapenzi na wenzako lakini mheshimiwa Dk. Rweikiza ana upendo wa dhati kwetu na si kwa leo tu siku zote kila mwezi wa Ramadhani amekuwa akitoa msaada kama huu kwa hiyo sisi kazi yetu ni kumwombea dua,” alisema Imamu Yakub
Mwenyekiti wa Vijana Bakwata Wilaya ya Bukoba Vijijini, Shaf Abdulkadiri, alisema msaada huo ambao Dk. Rweikiza amekuwa akiutoa mara kwa mara unaonyesha upendo alionao kwa watu wenye imani nyingine na kuomba jamii kuiga mfano huo.
“Kwa niaba ya vijana wa Jimbo hili napenda kumpongeza na kumshukuru Mbunge wetu kwa kweli amefanya kitu kikubwa sana na cha kuigwa na jamii nzima tunamwomba Mungu amzidishie na aendelee kumwongezea pale aipotoa,” alisema