Serikali itatoa viwanja 21 kwa wahanga wa maporomoko ya tope katika mlima kawetere, Itezi jijini Mbeya, huku zaidi ya vifaa na vyakula vyenye thamani ya Shilingi Milioni 40 vikitolewa kwa wahanga kuanzia tarehe 14 Aprili, 2024 maafa hayo yalipotokea hadi sasa.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa kwa ajili ya wahanga, Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini ambaye pia ni Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani(IPU) Mhe. Dkt. Tulia Ackson ametoa pole kwa wahanga hao na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia.Suluhu Hassan kwa misaada ya chakula, magodoro, fedha taslimu na viwanja kwa wahanga.

Aidha Dkt. Tulia amewaomba wadau wengine watakaoguswa na jambo hili kuchangia vifaa vya ujenzi ili kufanikisha kupatikana kwa sehemu ya kujihifadhi wahanga hao, baada ya nyumba zao kufukiwa na tope.

Kwa upande wake William Lukuvi akiwakilisha ujumbe kutoka Ofisi ya Rais amesema kuwa m Rais ameguswa na kila eneo lililokumbwa na maafa hapa nchini na bado ataendelea kutoa msaada kwa wahanga.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera amekiri kupokea maelekezo kutoka kwa Rais na kuahidi kutoa viwanja sehemu nzuri kwa wahanga na utekelezaji utaanza mara moja.

Dkt. Tulia amefika Itezi leo tarehe 21 Aprili, 2024 na kuzungumza na wahanga pamoja na kutembelea eneo ulipotokea mmomonyoko wa tope katika mlima Kawetere.


Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson akimkabidhi godoro mmoja wa wahanga wa maporomoko ya tope ya Itezi jijini Mbeya alipofika kuwafariji leo tarehe 21 Aprili, 2024

By Jamhuri