Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.6 unakamilika kwa wakati na ufanisi uliokusudiiwa.

Amesema hayo Wilayani Kasulu alipokutana na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na viongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kusisitiza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ndio utakuwa ukombozi wa uchumi wa mkoa wa Kigoma na kanda ya magharibi kwa ujumla.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akisisitiza jambo kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Bw, Ludovick Nduhiye na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila alipokagua barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.6 Mkoani Kigoma.

“Wananchi wengi wa Kasulu, Kibondo na Kakonko wanafanya biashara nyingi Kahama, Shinyanga na Mwanza hivyo kukamilika kwa barabara hii kutakuza uchumi wa wakazi wengi wa mkoa wa Kigoma”, amesema Dkt. Mpango.

Amesisitiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuongeza kasi ili kukidhi matarajio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuufungua Mkoa wa Kigoma katika Nyanja zote za usafiri.

Naye Mwenyekiti wa PIC Mhe. Jerry Silaa amemweleza Makamu wa Rais kuwa Kamati yake imekagua uwekezaji wa Serikali mkoani Kigoma na imeridhika kwa kazi nzuri zinazofanywa katika usafiri wa reli, bandari, barabara na anga na kumhakikishia Makamu wa Rais kuwa kamati hiyo itakagua miradi hiyo mara kwa mara ili kuhakikisha uwekezaji unaofanywa unakuwa na tija kwa wananchi.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila akifafanua jambo kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango alipokagua barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.6 Mkoani Kigoma.

“TANROADS hakikisheni ujenzi wa barabara licha ya kutoa fursa kwa wananchi bali uwezeshe wakandarasi wetu kupata ujuzi na hivyo kumudu kujenga na kusimamia miradi mikubwa siku za usoni”, amesesitiza Mhe. Silaa.

Aidha, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya ujenzi), Bw, Ludovick Nduhiye amesema Wizara imejipanga kuhakikisha mkoa wa Kigoma unafikika kwa urahisi kupitia barabara zake zote, reli, bandari na anga ili kuuunganisha na masoko ya nchi za Congo, na Burundi kwa urahisi na hivyo kukuza shughuli za kilimo, biashara na uwekezaji.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Rogatus Mativila amesema barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.6 ni sehemu ya barabara kuu ya Nyakanazi-Kibondo-Kasulu-Manyovu inayounganisha mkoa wa Kigoma na mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga na Mwanza na pia inaunganisha Tanzania na Burundi kupitia mpaka wa Manyovu.

barabara ya kikanda yenye lengo la kuufungua ukanda wa magharibi na kuiunganisha Tanzania na Burundi.

Eng. Mativila amesema katika kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo ya kikanda unakwenda kwa haraka mradi umegawanywa katika sehemu nne ambapo zaidi ya shilingi bilioni 325.6 zinatarajiwa kutumika katika kuwalipa wakandarasi wanne wanaojenga barabara hiyo wakati takriban shilingi bilioni 15.37 zikitengwa kuwalipa wasimamizi wake.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), iko mkoani Kigoma kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali ambapo pamoja na mambo mengine imekagua, imeelekeza na kuelezea kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unatarajiwa kukamilika baadae mwaka huu.

Muonekano wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.6 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Kigoma.

By Jamhuri