Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imesaini mkataba wa mradi wa kuboresha miundombinu katika jiji la Dar es salaam (DMDP)awamu ya pili utakao gharimu bilioni 988.83.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo leo februari 20,2024 jijini Dar es salaam Waziri wa fedha Mwigulu Nchema amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha miundombinu katika jiji inaimarika.

Amesema mkataba huo wa DMDP II unaashiria dhamira ya serikali ya kuimarisha miundombinu na kukuza ustawi wa kiuchumi kwa wakazi wa jiji hilo.

“Hatua hii itawezesha serikali ya Tanzania kupata mkopo kutoka benki ya Dunia wenye thamani ya dolla za kimarekani milioni 361.1 sawa na shilingi bilioni 988.093 kutekeleza mradi DMDP kwa awamu ya pili”amesema.

Amesema mradi huo wa DMDP II ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango wa tatu wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano 2021/22 mpaka 2025/26,lakini pia ni utekelezaji wa irani ya uchaguzi ya CCM na ajenda ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa(TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amesema watahakikisha fedha hizo zinaenda zilipokusudiwa kwani ni dhamira ya Rais kuona jiji la Dar es salaam linakuwa jiji la kibiashara.

Amesema fedha hizo zitaenda kujenga miundombinu ya barabara,ujenzi wa madampo makubwa ya takataka,masoko 18,vituo vya mabasi 9 pamoja na mifereji ya maji ya mvua ili kuzuia mafuriko pindi mvua kubwa zinaponyeesha.

“Tunakwenda kufanya usimamizi wa hizi fedha ili zilafanye lililokusudiwa na kazi ianze mara moja lakini pia tutafanya ushawishwi kwa Rais ili kurudisha hadhi ya jiji la Dar es salaam”Amesema.

Naye,Mkurugenzi mkaazi wa benki ya Dunia nchini Nathan Belete amesema wataendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika kuinua uchumi wa nchi kwani kwa zaidi ya miaka 15 wameweza kufanya mambo mengi ya maendeleo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa wabunge wa Dar es salaam Dkt Faustine Ndugulile amesema hawatakubali upotevu wa fedha hizo wala kazi zilizokusudiwa kufanywa chini ya kiwango hivyo ametoa rai kuanza kwa mchakato wa kazi hizo mapema ili ifikapo mwezi April wakandarasi waangie kazini.

“Asilimia 10 ya watanzania nyumbani kwao ni Dar es salaam lakini pia asiliamia 70 ya uchumi wa nchi unatokea hapa hivyo kipaumbele lazima kiwe barabara kwani hakuna mashamba hapa”Amesema Ndugulile.

By Jamhuri