Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema ujumuishaji wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu, elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi utawajengea wanafunzi na wahitimu uwezo wa kusimamia fedha, kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kutumia fursa za kiuchumi kwa tija.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mwongozo wa Ujumuishaji wa Elimu ya Fedha katika mitaala uliofanyika Oktoba 2, 2026 jijini Dar es Salaam, Mhe. Ameir amesema elimu hiyo itawaandaa wahitimu kukabiliana na changamoto za kifedha wanapoingia katika soko la ajira, ikiwemo kupanga mapato na matumizi, kuweka akiba, kukopa kwa uwajibikaji na kutambua fursa za uwekezaji.
“Nazielekeza taasisi za elimu ya juu, TCU, NACTVET na VETA kusimamia ujumuishaji wa elimu ya fedha katika mitaala na mifumo ya udhibiti wa ubora, huku taasisi za fedha na washirika wa maendeleo wakishirikiana na vyuo kutoa mafunzo kwa vitendo, ushauri wa kitaalamu na programu za ujasiriamali,” amesema Mhe. Wanu.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya mwongozo huo yatapimwa kwa uwezo wa wanafunzi na wahitimu kutumia maarifa hayo kufanya maamuzi yenye uwajibikaji wa kifedha, kujiajiri, kuajiri wengine na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Sauda Msemo, amesema mwongozo huo unakamilisha juhudi za Serikali za kujumuisha elimu ya fedha katika mfumo rasmi wa elimu, huku Benki Kuu ikiendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu na taasisi nyingine kutoa utaalamu, kujenga uwezo wa wahadhiri na kufuatilia utekelezaji wake.
Mwongozo huo unalenga kuwawezesha wanafunzi na wahitimu kusimamia fedha zao kwa ufanisi, kujenga ustahimilivu wa kifedha na kutumia maarifa hayo kuchangia maendeleo yao na uchumi wa taifa.







