Mchekeshaji Eric Omondi wa Kenya amemuomba rais wa nchi yao, William Ruto kuwafukuza kazi makatibu mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wote wa mashirika ya umma kabla ya Alhamis wiki hii.

Omondi amesema Wakenya wamepoteza imani kwa Serikali yote ya Ruto na ndiyo sababu ameomba viongozi wafukuzwe ili kuleta viongozi wengine watakaoweza kuwapunguzia ugumu wa maisha.

Aidha Omondi ameweka wazi dhamira yake na wenzake ya kufika Ikulu kuonana na Rais Ruto.

“Mheshimiwa Rais tutakutembelea Ikulu Alhamisi saa 11 asubuhi, tutakuja kwa amani tukiwa tumevaa nguo nyeupe na tumebeba bendera” amesema.

Ni zaidi ya wiki tatu sasa wananchi wa kenya wanaendelea na maandamano ya kupinga kusainiwa muswada wa fedha wakilalamikia hali ngumu ya maisha.