Ulikuwa unafahamu kuwa faru Fausta, ambaye alifariki dunia mwishoni mwa mwezi uliopita ndiye alikuwa faru mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani? 

Kama haukuwa ukifahamu hivyo, basi haupo peke yako. Maelfu ya Watanzania wameonyesha kushangazwa kwao na taarifa kuwa faru Fausta ndiye alikuwa faru mzee kuliko wote duniani. Taarifa hiyo ilitolewa sambamba na taarifa ya kifo cha faru huyo.

Baadhi ya watu wanasema uzee wa faru Fausta haukutumiwa vizuri katika masuala ya utalii. Wanabainisha kuwa iwapo taarifa kuhusu umri wa Fausta zingetumika vema, faru huyo angeweza kuvuta maelfu na watalii na watafiti nchini, hivyo kuiongezea nchi fedha nyingi kupitia utalii.

Fausta amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 57. Kwa maisha ya faru, huu ni umri mkubwa sana na kutokana na hilo, katika siku za mwisho za maisha yake, Fausta alikuwa anatunzwa katika zizi maalumu kwa sababu aliishiwa nguvu, hivyo kushindwa kujihudumia mwenyewe. 

Faru huyo alifikia hata hatua ya kupoteza uwezo wa kuona kutokana na umri miubwa, hivyo kumfanya kuwa katika hatari ya kushambuliwa na kushindwa kujitetea akiwa porini.

Kituo cha televisheni cha EATV kilimnukuu Robert Fyumanga, ambaye ni daktari wa wanyamapori, anasema kuwa kuta za moyo wa faru Fausta zilikuwa nyembamba sana hali iliyosababisha damu ishindwe kupita kwa ufasaha.

“Kuta za moyo wake zimekuwa ni nyembamba sana, hivyo kushindwa kusukuma damu ya kutosha mwilini, kwa hiyo alikosa nguvu na kuanguka,” anasema Dk. Fyumanga.

Fausta alikuwa anatunzwa chini ya uangalizi maalumu ndani ya Bonde la Ngorongoro na ameacha rekodi ya kuwa faru mweusi mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani.

“Mara nyingi faru wanapozeeka, hupoteza uwezo wa kujilinda dhidi ya wanyama wengine kama fisi na simba, kwa hiyo ni muhimu kwa wahifadhi kuhakikisha usalama wa wanyama hawa adimu na wachache duniani,” Kamishna wa Uhifadhi katika Mamlaka ya Ngorongoro, Dk. Freddy Manongi, amekaririwa na vyombo vya habari. Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyoifanya hifadhi hiyo kutenga bajeti ya mamilioni ya fedha kwa ajili ya kugharamia matunzo ya Fausta.

Kwa mujibu wa Dk. Manongi, hivi sasa wamemtambua faru mwingine aitwaye Vicky kuwa mrithi wa Fausta kutokana na umri wake, Vicky anatajwa kuwa na umri wa miaka 49, umri ambao unamfanya na yeye kuwa mzee ambaye uwezo wa kujihudumia na kujilinda umepungua sana.

Kwa sababu faru Fausta alitengenezewa makazi maalumu ili kuhakikisha kuwa hadhuriki kwa  jambo lolote, Mamlaka ya Ngorongoro inafikiria pia kumhamishia Vicky ndani ya zizi alimokuwa akiishi Fausta ili kumsaidia na yeye katika kipindi chake cha uzee.

Vyombo vya habari vimemnukuu Naibu Waziri wa Utalii, Constantine Kanyasu, akisema kuwa baada ya Fausta kufariki dunia, wizara itashirikiana na wahifadhi pamoja na wataalamu wengine kuangalia jinsi ya kuuhifadhi mwili wake kutokana na sifa yake ya kuwa faru mzee kuliko wote duniani.

Hili ni jambo la kutiliwa maanani, kwani linaweza kuongeza kivutio kingine cha utalii nchini. Ni dhahiri kuwa wapo mamia ya maelfu ya watu duniani ambao wangependa kutembelea na kuona mabaki ya faru huyo aliyekuwa mzee kuliko wote duniani, hasa wakiwa na uhakika pia wa kumuona faru mwingine mwenye umri mkubwa, Vicky.

Maisha ya Fausta

Fausta, ambaye katika muda wote wa maisha yake alikuwa akiishi katika Bonde la Ngorongoro, alifariki dunia usiku wa Ijumaa, Disemba 27, mwaka jana. Ingawa bado chanzo hasa cha kifo chake hakijaelezwa, lakini askari waliokuwa wanamwangalia faru huyo kwa karibu wanaamini kuwa kifo hicho kimetokana na uzee.

“Huyu ndiye alikuwa faru mzee zaidi duniani, hiyo ni historia kwa Tanzania, tunahisi kifo chake ni cha kawaida kutokana na umri wake mkubwa. Madaktari wapo njiani watatueleza hasa sababu ya kifo chake baada ya kufanya vipimo,” Dk. Manongi anakaririwa na vyombo vya habari.

Hata hivyo, licha ya umri wake mkubwa, Fausta hakupata kuzaa, hivyo hajaacha mtoto. Lakini wataalamu wanasema kushindwa kwake kuzaa huenda ikiwa moja ya sababu ya yeye kuishi maisha marefu namna hiyo. 

Inaelezwa kuwa kubeba mimba kunaambatana na uchovu wa mwili, hivyo kupunguza umri wa kuishi. Aidha, faru jike mwenye mtoto anapaswa kutumia nguvu nyingi sana kumkinga mtoto wake dhidi ya maadui. Hivyo, hilo nalo huchukua nguvu nyingi za faru jike, hivyo kupunguza umri wake wa kuishi.

Kwa kawaida, faru jike huzaa kila baada ya miaka mitatu, lakini Fausta hakuwahi kupata mtoto tangu mwaka 1984. Faru akishazaa, hunyonyesha mtoto wake katika kipindi cha miezi 18. Katika kipindi hiki chote faru anawajibika kuhakikisha ulinzi wa mtoto wake, hivyo suala la kupambana na wanyama wengine katika kipindi hicho huwa ni la kawaida kwake.

Kwa kawaida, faru wanakadiriwa kuishi kwa muda wa kati ya miaka 35 na 40, akiwa anaishi porini huku akijihudumia mwenyewe porini, lakini huishi zaidi ya miaka hiyo iwapo atakuwa anatunzwa katika bustani ya wanyama akiwa chini ya ulinzi maalumu.

Faru mwingine mweusi na jike ambaye anatajwa kuwa na umri mkubwa alijulikana kama Solio. Huyu alifariki dunia nchini Kenya mwaka 2016, akiwa na umri wa miaka 42. Hivyo, wakati anafariki dunia alikuwa hajafikia hata umri wa Vicky. Hii inaifanya Tanzania bado kuwa na historia ya kuwa na faru wenye umri mkubwa.

Rekodi ya umri iliyowekwa na Fausta ni ya kipekee duniani, kwa sababu katika miaka 57 aliyoishi, Fausta aliishi porini kwa muda wa miaka 54. Ni katika miaka yake mitatu ya mwisho wa maisha yake ndiyo alikuwa chini ya matunzo maalumu.

Faru anayemfuatia Fausta kwa umri mkubwa duniani anaitwa Sana, ambaye naye alikuwa jike aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 55. Huyu alikuwa akiishi Afrika Kusini. Wapo faru ambao kwa muda mwingi wanakuwa chini ya uangalizi maalumu, lakini hawajawahi kuishi na kufikisha miaka mingi kama Fausta.

Umaarufu wa Fausta

Afya ya Fausta ilianza kupata matatizo mwaka 2016 baada ya kudhoofika kutokana na uzee kiasi cha kuanza kushambuliwa na wanyama wengine kama vile fisi. Mashambulizi hayo yalimuacha na majeraha makubwa. Hapo ndipo maofisa wanyamapori walipoamua kumchukua Fausta na kumweka chini ya uangalizi maalumu. 

Alijengewa zizi maalumu akawekwa humo, akipatiwa chakula na kupatiwa matibabu hadi majeraha aliyoyapata kutokana na mashambulizi ya fisi yakapona.

Fausta alianza kufahamika kwa watu wengi baada ya kufariki dunia kwa Solio nchini Kenya. Solio alikuwa ni faru aliyekuwa na umri mkubwa wa miaka 42, akiwa amepitisha muda wa wastani wa faru mweusi kuishi. Faru mweusi anakadiriwa kuishi kwa kati ya miaka 30 hadi 35 akiwa porini wakati akiwa kwenye matunzo maalumu anawea kuishi hadi miaka 50.

Hivyo, Fausta naye amepitisha mno muda wa makadirio wa faru kuishi.

Jambo jingine lililomfanya Fausta afahamike kwa watu wengi ni mgogoro uliotokana na gharama za matunzo yake. Mwaka 2017, baadhi ya wabunge walihoji kwa nini fedha nyingi zinatumika kumtunza faru Fausta. 

Hilo liliibuka baada ya Bunge kuelezwa kuwa Sh milioni 64 zilikuwa zikitumika kwa mwezi kwa ajili ya matunzo ya faru huyo aliyekuwa amejengewa zizi maalumu. Hata hivyo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) baadaye ikatoa ufafanuzi ikisema kuwa ni kiasi cha Sh milioni 1.4 ndicho kilikuwa kinatumika kwa ajili ya matunzo ya faru huyo na si Sh milioni 64 kama ilivyokuwa imedaiwa.

NCAA ilisema kuwa gharama hizo zinajumuisha chakula, matibabu na ulinzi wa faru huyo ambaye alikuwa ameshapoteza uwezo wa kuona kutokana na uzee.

Akitetea gharama za kumtunza Fausta, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, aliliambia Bunge mwaka juzi kuwa gharama hizo ni ndogo sana ukilinganisha na thamani ya mnyama huyo.

Aliyasema hayo wakati akijibu swali la Suzan Mgonokulima, aliyesema serikali inamhudumia faru huyo kwa gharama ya Sh milioni 64 kwa mwezi, ambaye hazalishi kutokana na kuwa mzee sana.

“Lakini serikali hiyo haiwezi kumhudumia mwananchi aliyezeeka ambaye hawezi kufanya shughuli zozote za kujikimu maisha na hana mtu wa kumsaidia. Je, ni kipi kilicho muhimu zaidi kwa serikali kati ya faru Fausta au mwananchi mzee asiyeweza kufanya lolote na hana wa kumsaidia?” alihoji mbunge huyo.

Hasunga alisema katika majibu yake kuwa faru huyo amekuwapo eneo la Hifadhi ya Ngorongoro tangu mwaka 1965 na alikuwa ndiye mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani.

“Kutokana na uadimu wa wanyama hao, uwepo wa faru Fausta umekuwa kivutio kikubwa kwa watalii na watafiti wa ndani na nje ya nchi, hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa mapato katika Hifadhi ya Ngorongoro na serikali kwa ujumla,” alisema.

Kutokana na uzee, alisema faru huyo alijeruhiwa na fisi Septemba 4, 2016, hivyo kulazimu atunzwe kwenye kizimba kwa ajili ya uangalizi maalumu ambao unahusisha matibabu, chakula na ulinzi.

Takwimu zinaonyesha kuwa faru ni mmoja wa wanyama wanaoongoza kuuawa na majangili barani Afrika. Idadi ya faru imekuwa ikipungua kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na ujangili. Hilo limezilazimisha serikali na taasisi kuja na mikakati maalumu ya kuwalinda wanyama hao. Kumweka Fausta kwenye zizi maalumu na kupewa ulinzi, chakula na matibabu ni moja ya mikakati hiyo.

Faru anawindwa sana na majangili ikiaminika kuwa pembe zake zina thamani kubwa. Pamoja na kuwa mapambo, lakini wapo wanaoamini kuwa pembe hizo zinatumika kwa ajili ya matibabu ya maradhi kadhaa.

Kwa mujibu wa taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na mazingira na wanyama, WWF, hapo zamani faru walikuwa ni kati ya wanyama waliokuwa wakizurura maporini kwa wingi katika nchi za Ulaya, Asia na Afrika.

Lakini hadi kufikia mwaka 1970, idadi ya faru ilishuka hadi kufikia 70,000 na hivi sasa idadi hiyo imeshuka zaidi hadi kufikia kama faru 29,000 ambao wanaishi porini. Maisha ya faru wengi yamekatishwa na majangili.

Ilifika wakati faru weupe iliaminika kuwa wametoweka Afrika, lakini baadaye alikuja kuonekana na uamuzi ukafanyika kumweka faru huyo kwenye bustani chini ya uangalizi maalumu.

Fausta alikuwa miongoni mwa faru weusi ambao asili yao ni kusini mwa Afrika. Tofauti na faru wengine wenye umri mkubwa duniani, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Fausta aliweza kuishi kwenye mazingira ya asili, tofauti na wengine katika nchi tofauti duniani, ikiwamo Kenya, wanaoishi katika mazizi maalumu au maeneo yaliyotengwa kwa faru yajulikanayo kama ‘Rhino Sanctuary’. Baadaye, kutokana na hatari zilizokuwa zikimkabili, Fausta naye akajengewa zizi lake na kutunzwa humo.

Kwa mujibu wa Dk. Manongi, Fausta angeweza kuachiwa kutoka kwenye banda hilo iwapo angeonyesha uwezo wa kujitegemea. Lakini kwa bahati mbaya, alipoteza uwezo wa kuona na hilo liliwapa hofu waliokuwa wakimtunza kuwa akiachiwa anaweza kuuawa kirahisi.

Fausta alikuwa miongoni mwa faru 50 ambao wanaishi katika Bonde la Ngorongoro kwa sasa.

Faru John naye

Matukio mawili yaliyotokea Disemba, mwaka juzi nchini Tanzania na Kenya, yaliibua mijadala mizito na kuwafanya faru kutawala mijadala kadha wa kadha.

Nchini Tanzania, ziliibuka taarifa zilizodai kupotea kwa faru maarufu kwa jina la John, aliyekuwa akiishi Ngorongoro, ambaye awali ilidaiwa aliuzwa kwa mwekezaji Kampuni ya Grumeti.

Lakini baadaye ilibainika kuwa John hakuuzwa, bali alihamishwa baada ya taratibu zote kufuatwa kutoka Ngorongoro na kupelekwa eneo la Sasakwa, Grumeti, ambako Agosti 21, mwaka juzi alifariki dunia kutokana na maradhi na umri.

Kwa upande wa nchi jirani ya Kenya, Disemba 5, mwaka juzi, faru mzee kuliko wote nchini humo aliyejulikana kwa jina la Solio (42), alifariki dunia.

Solio alikuwa amehifadhiwa eneo maalumu la uhifadhi  liitwalo Lewa, ambalo linatajwa kuwa hifadhi kubwa maalumu (si ya asili) ya faru barani Afrika. Katika hifadhi hiyo kuna faru weusi 84 na weupe 72.

Faru ni miongoni mwa wanyamapori ambao wamo katika tishio la kutoweka duniani, kutokana na majangili kuwaua kisha kuuza pembe zao kwa bei kubwa, soko kubwa likiwa Mashariki ya Mbali.

Tangu mwaka 1998, Tanzania imekuwa na mpango mkakati maalumu wa kuongeza idadi ya faru ili kuwa na zaidi ya faru 100 ifikapo mwaka 2018.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Save the Rhino ya nchini Uingereza, kulikuwa na faru 500,000 barani Afrika na Asia mwanzoni mwa karne ya 20, lakini kwa sasa wanakadiriwa kusalia 29,000 tu.

Faru Fausta katika siku za mwisho za uhai wake.

78 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!