Tajiri namba moja barani Afrika, Aliko Dangote, ameuaga mwaka 2019 kwa kuongeza zaidi utajiri wake kwa dola bilioni 4.3 za Marekani.

Dangote, mwenye umri wa miaka 62, raia wa Nigeria ni mfanyabiashara anayemiliki viwanda kadhaa barani humo, alikuwa na utajiri uliofikia dola bilioni 15 za Marekani hadi mwishoni mwa mwaka jana.

Hilo linamfanya Dangote kuwa tajiri namba 96 duniani, kwa mujibu wa orodha iliyoandaliwa na Bloomberg.

Dangote ana viwanda katika nchi kadhaa za Afrika vikizalisha saruji, unga na sukuri. Hapa nchini, Dangote anamiliki kiwanda cha saruji mkoani Mtwara na saruji yake imeshaanza kushika umaarufu kwenye soko. 

Ana mtandao mpana wa usambazaji wa bidhaa yake hiyo, ikihusisha mamia ya malori ambayo hutumika kusafirisha saruji yake katika mikoa yote nchini.

Dangote alizaliwa katika familia ya wafanyabiashara matajiri kaskazini mwa Nigeria na alifanikiwa kuanzisha biashara yake ya kwanza ya saruji akiwa na umri wa miaka 21.

Baadaye alijikuta katika sekta ya uzalishaji wa zana na ujenzi katika miaka ya 1990  akisaidiwa na sera za serikali, ambazo zililenga kupunguza uagizaji wa bidhaa nje ya nchi yake.

Hata hivyo, bado kuna watu ambao wanamtuhumu kwa kutumia ukaribu wake na viongozi wa serikali kupata faida katika biashara zake, hasa kwa kupata masoko kiurahisi, jambo ambalo amekuwa akilikanusha mara kwa mara.

Kampuni yake, Dangote Industries, inahusisha kampuni kubwa ya kuzalisha saruji barani Afrka ambayo imesajiliwa katika Soko la Hisa la Lagos, Dangote Cement Plc.

Hiyo ni moja ya kampuni kubwa nne ambazo zinauza hisa zake chini ya Kampuni ya Dangote Industries, ambayo kwa pamoja yana thamani ya moja ya tano ya thamani ya kampuni zote zinazouza hisa katika soko la Lagos.

Mwaka 2020 unaweza kuwa na maana sana kwa bilionea huyo, ambaye anakaribia kukamilisha ujenzi wa moja ya viwanda vikubwa vya kusafisha mafuta, anachokijenga nchini mwake.

Kitakapokamilika, kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mafuta ambayo ni zaidi ya yale yanayohitajika nchini Nigeria na hilo linaweza kuleta fanaka kwenye uchumi wa nchi hiyo, kwani Nigeria inaweza kuacha kuagiza mafuta kutoka nje.

Dangote pia anajenga kiwanda cha mbolea katika eneo hilohilo analojenga kiwanda cha kusafisha mafuta.

452 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!