Bravo Kikwete, lakini agizo lako lisilenge mahindi, Njombe pekee

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, anastahili pongezi kutokana na hatua yake ya kutengua msimamo wa muda mrefu wa Serikali kuwazuia wakulima kuuza mahindi nje ya nchi.

Ameagiza kuanzia sasa wakulima waruhusiwe kuuza zao hilo nje ya mipaka ya nchi yetu, kama hatua mojawapo ya kuwawezesha kujiinua kiuchumi.

Kiongozi huyo wa nchi ametoa agizo hilo katika mazungumzo na watendaji wa Mkoa wa Njombe wakati wa majumuisho ya ziara yake mkoani humo, wiki iliyopita.

Hata hivyo, Rais Kikwete hakufafanua kama agizo lake hilo linalenga zao la mahindi pekee na Mkoa wa Njombe pekee.

Ninasema hivyo kwa sababu tunafahamu kwamba wakulima mkoani Njombe hawazalishi mahindi pekee, wanazalisha pia chai na viazi mviringo, miongoni mwa mazao mengine ya biashara na chakula.

Tunakumbuka pia kwamba zamani Wilaya ya Makete mkoani humo ilikuwa mzalishaji mkubwa wa pareto, lakini baadaye kilimo cha zao hilo kilipukutika kutokana na kuyumba kwa soko husika.

Hali kadhalika, zao la mahindi linalimwa karibu katika mikoa yote hapa nchini. Kwa mfano Shinyanga, Mara, Mbeya, Kagera, Mwanza, Kilimanjaro, Manyara na Morogoro ni miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wingi zao la mahindi.

Lakini pia, kilimo cha mpunga, mtama, ngano, alizeti, ulezi, pamba, korosho, ndizi, kahawa, muhongo, tumbaku, viazi vitamu, mbogamboga, matunda, na kadhalika kinatekelezwa katika mikoa mingi hapa Tanzania.

Kwa mantiki hiyo, Rais wetu anapoagiza wakulima wa mkoani Njombe waruhusiwe kuuza mahindi nje ya nchi ili kuinua kipato chao, akumbuke pia kwamba na mikoa mingine ina wakulima wa mahindi na mazao mengine lukuki wanaozuiwa kuyauza nje ya Tanzania.

Ni vizuri agizo hilo la Rais Kikwete likalenga mazao yote badala ya mahindi pekee, lakini pia mikoa yote hapa nchini badala ya Njombe pekee. Wakulima wote nchini wanastahili kunufaika na agizo hilo.

Inakumbukwa kwamba kwa muda mrefu sasa uchumi wa wakulima wengi wa mazao ya chakula na biashara hapa nchini, haujaimarika kutokana kikwazo cha zuio la kuuza mazao nje ya nchi. Kutokana na hali hiyo, wakulima wengi wamekata tamaa ya kuendelea kujikita katika kilimo cha mazao mbalimbali baada ya kuona kinawadhoofisha badala ya kuwainua kiuchumi.

Agizo la Rais Kikwete la kuwaruhusu wakulima wa mahindi mkoani Njombe kuuza zao hilo nje ya nchi, likitekelezwa sambamba na kuruhusu mazao mengine katika mikoa yote litafungua ukurasa mpya wa matumaini kwa wakulima hapa nchini.

Wakati fulani mwanahabari mwenzangu, Manyerere Jackton, aliandika makala akitaka wakulima nchini wasiingiliwe na Serikali kwa kupangiwa muda wa kuvuna, kuuza na mahali pa kuuza mazao wanayozalisha kwa kuwa siku zote wamekuwa ni watu wa kujizatiti wenyewe bila kusaidiwa pembejeo na nguvu-kazi shambani.

Wakulima wamekuwa wakizuiwa kuuza mazao nje ya nchi kwa bei nzuri inayowarudishia gharama za uzalishaji na kuwapatia faida. Wengi wamekuwa wakilazimishwa kuuza mazao yao ndani ya nchi, na wakati mwingine ndani ya wilaya na mikoa yao pekee. Huu ni unyanyasaji na uonevu uliovuka mipaka dhidi ya wakulima.

Binafsi nimefurahi kusikia Rais Kikwete ameshabaini kwamba msimamo wa kuwazuia wakulima kuuza mazao nje ya nchi umekuwa ukitoa mwanya kwa watendaji wachache wa Serikali wasio waadilifu kujinufaisha binafsi, huku wakulima wengi wakizidi kudidimia kiuchumi.

“Kuwazuia wakulima kuuza mahindi yao nje ya nchi ni kuwatajirisha wanaokaa kwenye vizuizi na kufanya ulanguzi.

 

“Ni lazima mkoa uhakikishe kuwa wakulima wanawekewa utaratibu mzuri ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu kuuza mazao yao nje ya nchi,” amesema kiongozi huyo wa nchi, akisisitiza kwamba kufanya hivyo kutatoa nafasi kwa wakulima kuinua kipato chao.

Lakini, hatua nyingine itakayofanikisha utekelezaji wa agizo hilo la Rais ni ufuatiliaji. Hii ni kutokana na kasumba mbaya iliyojengeka miongoni mwa watendaji wengi wa Serikali. Wengi wanapoachwa kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Serikali bila kusimamiwa na mamlaka ya juu ama huyapuuza, au huyageuza miradi ya kujipatia maslahi binafsi.

Kwa sababu hiyo, Rais mwenyewe, na au kupitia kwa wasaidizi wake wa karibu akiwamo Waziri Mkuu na Waziri wa Kilimo, Ushirika na Chakula, afuatilie kwa karibu utekelezaji wa agizo lake hilo kwa manufaa ya wakulima na Taifa kwa jumla.

Kikubwa zaidi, viongozi watakaobainika kukwaza utekelezaji wa agizo hilo kwa namna moja au nyingine wasifumbiwe macho, wachukuliwe hatua kali za kinidhamu na kisheria kutokana na kosa la kutoheshimu agizo halali la Mkuu wa Nchi.

Kwa kufanya hivyo, ruhusa ya kuuza mazao nje ya nchi itakuwa mkombozi wa wakulima wengi ambao kwa muda mrefu wameendelea kuelea katika lindi la umaskini licha ya kilimo kutajwa kuwa ni uti wa mgongo wa Taifa letu.


By Jamhuri