Sisi tunaona ya kipuuzi, wenzetu wanayachukua

Kazi ya uandishi haina tofauti na kazi inayofanywa na makasisi na masheikh. Tangu nimeanza kushiriki ibada, nimeyasikia maneno yale yale yakirejewa makanisani, na kwa kweli ni hayo hayo yanayorejewa misikitini, na kadhalika.

Msimamo wa kutetea misingi inayolenga kulinda ustawi wa Taifa letu ni mambo tunayopaswa kuyarejea hata kama yatawachusha baadhi ya watu.

Septemba 24, mwaka huu nilisema Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilichodai Uhuru wa nchi hii kilikuwa na ahadi nzuri. Baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilizirithi.

Uzuri wa ahadi hizo ni kuwa zililenga kujenga uzalendo na upendo miongoni mwa wananchi. Shabaha ilikuwa kuwafanya Watanganyika na baadaye Watanzania waone fahari ya kuipenda nchi yao na kuwa tayari kuifia.

Kwangu mimi, ahadi hizo zina sifa ya kuwa tunu ya Taifa na dira ya kutuwezesha kukijenga kizazi imara cha sasa na kijacho. Waungwana hawawezi kuzipuuza kwa sababu tu zimetokana na CCM. Tulikubali jema bila kujali linatoka upande gani. Tuwe radhi kulikubali jambo kutoka CCM au kwa upande wa Upinzani, ilimradi tu liwe na manufaa kwa Taifa letu.

Ahadi ninazozisema hapa ni hizi:

(1) Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.

(2) Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote.

(3) Nitajitolea nafsi yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma.

(4) Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa.

(5) Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.

(6) Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote.

(7) Nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu.

(8) Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.

(9) Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na raia mwema wa Tanzania na Afrika.

Kwa mtazamo wangu, marekebisho madogo yalistahili kufanywa kwenye ahadi ya tisa kwa kuondoa maneno ‘mwanachama’ na ‘CCM’ na kuwa: ‘Nitakuwa mwaminifu kwa nchi yangu na raia mwema wa Tanzania na Afrika’.

Narejea kusema kuwa tukiacha mambo ya kiitikadi yanayotugawa, ukweli ni kwamba hizi zilistahili kabisa kuwa ni ahadi za kila Mtanzania.

Nimejaribu kuzirejea ahadi hizo za wana-TANU na wana-CCM kwa lengo moja kubwa la kujaribu kuamsha hamasa ya Watanzania ya kuipenda nchi yetu na kuwapenda binadamu wenzetu.

Amri ya Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka wahamiaji haramu warejee kwao au wahalalishe ukazi wao nchini, haikulenga kuwanyanyasa, bali kulinda usalama wa Taifa letu.

Hatuwakatai wageni wala watu wa mataifa mengine kupata uraia wa Tanzania. Hakuna anayekataa. Tena basi, tunapaswa kuwahimiza wageni hao wajitokeze kuomba uraia ili baadaye tuwabane waweze kuwajibika kulitumikia Taifa hili.

Wahamiaji haramu wameingia nchini mwetu na kujitwalia maeneo ya ardhi wakijitambulisha kuwa ni Watanzania. Kwa kutumia kigezo cha kila Mtanzania ana haki ya kuishi popote hapa nchini, wamemilikishwa ardhi huku Watanzania halisi wakikosa fursa hizo. Hili haliwezi kuendelea kukumbatiwa na Serikali inayowajali raia wake.

Kuna idadi kubwa ya wahamiaji haramu kutoka Asia. Wanafanya kazi ambazo zingepaswa kufanywa na Watanzania. Wapo wanaofanya hadi kazi za kupaka rangi! Wanaishi kwenye mabohari. Kuna Wachina wengi wanaoishi nchini kwa mtindo huo. Kuna Wahindi na Wapakistani wengi wa aina hiyo.

Nimejaribu kurejea haya niliyopata kuyasema kwenye makala zilizopita kwa sababu hivi karibuni majirani zetu Wakenya wameamua kufanya kile ambacho sisi Tanzania tuliona hakina maana. Wameamua kujenga mfumo wa mabalozi wa Nyumba Kumi. Sidhani kama watakuja na jina kama hilo, lakini maudhui ya mpango huo ni kuwa na kitu kama kile ambacho Watanzania tulikuwa nacho, na kikawa na manufaa makubwa sana kwa ulinzi na usalama wa wananchi na Taifa letu kwa jumla.

Baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini, nafasi ya Balozi wa Nyumba Kumi imepuuzwa. Imepuuzwa kwa sababu imeonekana kwamba ipo kwenye mfumo wa ki-CCM.

Vyovyote iwavyo, mfumo wa kuwa na Mabalozi wa Nyumba Kumi ulitufaa sana. Ongezeko la uhalifu nchini pamoja na wimbi kubwa la wahamiaji haramu sina shaka kabisa kuwa ni matokeo ya kupuuzwa kwa kitu hiki.

Nafasi hiyo ni muhimu maana ilisaidia mno kuwatambua wageni katika eneo la nyumba kumi. Wakenya wameliona hilo baada ya kulemewa na mashambulizi ya magaidi. Wamekaa, wametafakari, wameona dhima ya ulinzi wa taifa lao inaanzia kwa wananchi wenyewe huko huko wanakoishi.

Uamuzi wa Wakenya ni uthibitisho mwingine kuwa Tanzania tumekuwa waasisi wa mambo ya maana sana, lakini tumeyaacha, ama kwa ulevi tu wa wimbo wa demokrasia, au kwa kuvimbiwa na amani, utulivu na mshikamano tulivyokuwa navyo.

Tulikuwa na Siasa na Kilimo. Tukaiua. Tukaibuka na Kilimo Kwanza! Kilimo Kwanza ni mvinyo ule ule ndani ya chungu kipya cha Awamu ya Nne.

Sisi Tanzania ndiyo tuliokuwa waasisi wa Elimu kwa Wote (Universal Primary Education-UPE). Tulifanikiwa sana kwenye jambo hilo kiasia cha Taifa letu kupewa tuzo kubwa ya Umoja wa Mataifa mwanzoni mwa miaka ya 1980.

Tulifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana kufuta ujinga. Mfumo huo wa elimu ya Tanzania ndiyo ulioifanya dunia nzima ikaanza kuufuata kwa kuamini kuwa elimu ni haki ya kila mtoto. Tulienda mbali zaidi kwa kuimarisha Elimu ya Watu Wazima (EWW).

Mambo haya ya maana tulipoyapa kisogo, wenzetu wakayachukua. Sasa wanatucheka kwa sababu idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika nchini mwetu ni kubwa mno. Watoto wanahitimu elimu ya msingi, na hata sekondari wakiwa hawajui kusoma wala kuandika. Tumeuvaa utandawazi kichwa kichwa kwa kuamini kuwa dhima ya kumsomesha mtoto ni ya mzazi au mlezi — kama hawana uwezo, basi shauri yao! Hilo ni kosa.

Wakenya kwa kuona mafanikio ya UPE Tanzania, licha ya wao kufuata siasa na sera za kibepari, na kwa mshangao wa wengi, wakatangaza nao kuanza kutoa elimu bure kwa watoto wao. Hilo wamelisimamia vizuri na sasa wanaenda nalo kwa kasi.

Wakenya kwa miaka mingi hawakuwa na miiko ya uongozi. Waliliona Azimio la Arusha kama kitu kisichofaa. Ukweli umeendelea kuwa ukweli. Wameandika Katiba mpya na kuchukua mambo mengi ya maana kutoka kwetu na kuyaingiza humo. Muda si mrefu Wakenya watatuacha mbali kwa sababu mazuri ya kwetu wameyachukua, ilhali sisi tukiona hayana maana (Wewe ukiona cha nini mwenzako anasema atakipata lini) tusisahau msemo huo.

Sikushangaa kuona sasa wanataka kuanzisha mfumo wa Mabalozi wa Nyumba Kumi. Wameona mbali. Wamejua faida zake. Haitashangaza kuona wakianzisha mafunzo ya Chipukizi ili kuwajengea uzalendo watoto wao hatimaye wawe raia wema kwa nchi yao.

Sisi hapa, kama ilivyokuwa kwa Mabalozi wa Nyumba Kumi, tuliamua pia kuua mafunzo ya Chipukizi kwa sababu yote haya ni mambo ya CCM! Tumebaki na mafunzo ya halaiki ambayo kwa kweli hayawezi kusaidia kuwaweka pamoja watoto na kuwajengea uzalendo.

Tunapaswa kurejesha mafunzo ya Chipukizi ili watoto waimbe nyimbo za kujivunia nchi yao, nyimbo za kuwafanya wawe tayari kuifia Tanzania, nyimbo za kuwapa ujasiri wa kukabiliana na hali yoyote na adui yeyote; nyimbo za kuwafanya Tanzania kwao ndiyo kiwe ‘chama chao kikuu’.

Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana wanaotoka sekondari na vyuo hayawezi kujenga uzalendo. Samaki anakunchwa akingali mbichi. Kumfunza uzalendo mtu aliyekwisha balehe au kuvunja ungo wakati mwingine unaweza usipate kile unachokusudia.

Tuanze na watoto wadogo. Mafunzo ya Chipukizi yanaweza kurejeshwa kwa mtindo mwingine. Yawe mafunzo yanayoweza kutolewa katika shule zote za awali, msingi na sekondari. Tuwe na nyimbo za kitaifa ambazo mtoto au kijana wa Mtwara akikutana na mwenzake wa Kagera wanaweza kuziimba kwa pamoja.

Matukio mengi tunayoyaona sasa katika nchi yetu yanahitaji mwamko mpya wa mabadiliko. Kwanini watumishi wa umma ndiyo majangili? Kwanini Watanzania wanauana hovyo? Kwanini miundombinu ya umma inahujumiwa? Kwanini tunawakaribisha wahamiaji haramu? Kwanini Polisi na Usalama wa Taifa ndiyo wanaosimamia wageni kutorosha madini yetu? Kwanini vibali vinatolewa Uhamiaji kwa wageni wasiostahili kufanya kazi fulani fulani nchini mwetu? Kwanini  tumekuwa na mioyo mibaya kiasi cha kuwapiga-sachi hata maiti wakati wa ajali? Kwanini tumekosa utu?

Kuna mahali tumekosea. Tunapaswa kurekebisha kasoro hii kabla mambo hayajawa mabaya zaidi.

Mwarobaini wa haya nauona umo kwenye zile ahadi kenda nilizozitaja hapo juu. Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja: Tukiamiani kuwa binadamu wote ni ndugu, hatutafanyiana dhuluma. Tutasaidiana na tutaheshimiana.

Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote: Tukiitumikia nchi yetu, tutaipenda, tutailinda, na tutasaidiana.

Nitajitolea nafsi yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma: Tukijitolea, hawa maadui ambao ni kikwazo kikubwa kabisa katika maendeleo ya mwanadamu, watatoweka na kwa hiyo tutakuwa na maisha mazuri kabisa.

Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa: Tukiamini na kutekeleza kwa dhati ahadi hii, hatutakuwa na mpango wa kupanua magereza, hatutakuwa na msongamano wa wafungwa na mahabusu, hatutakuwa na watu wanaoishi miaka 20 hadi wanakufa wakihangaika kupata haki zao, na kwa kweli hata Mahakama zitapumua. Muda wa kuhangaika mahakamani na polisi tutautumia kujiletea maendeleo.

Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu: Hili likitekelezwa hakutakuwapo kiongozi atakayekuwa juu ya sheria. Hatutakuwa na mamangi-meza. Mwananchi ataheshimiwa kama mwajiri mkuu. Uonevu utakoma.

Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote: Elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Taifa lenye watu walioelimika lina fursa kubwa ya kupiga hatua kimaendeleo. Taifa lenye watu waliosoma haliwezi kuwa na mauaji ya vikongwe wala kuamini kuwa mtu anaweza kushinda mitihani kwa kupewa dawa kutoka kwa matapeli waganga wa kienyeji.

Nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu: Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Nchi inajengwa kwa umoja. Kila mmoja akiamua kutekeleza wajibu wake, na kwa kushirikiana na wenzake, nchi itapiga hatua kimaendeleo. Hili linaweza kuanzia kwenye kaya hadi Taifa.

Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko: Ahadi hii ikitekelezwa vyema, hata idadi ya makanisa na misikiti itapungua. Ukweli ni uhuru. Tukiwa na Taifa la watu wasema kweli, tutaondoa migongano katika jamii. Siku zote mtu mkweli anakuwa huru.

(Ahadi ya tisa niliyoirekebisha) Nitakuwa mwaminifu kwa nchi yangu na raia mwema wa Tanzania na Afrika’. Tukiwa waaminifu kwa nchi yetu na raia wema kwa Tanzania na Afrika, hakika hatutaweza kuwa sehemu ya wahujumu wa rasilimali zetu; tutakuwa tayari kuifia Tanzania na Afrika.

Kwa upande wa usalama wa Taifa letu, tunaweza kuifanya ngazi ya Balozi wa Nyumba Kumi kuwa ya kiserikali kabla ya ngazi ya pili ya Kitongoji au Mtaa. Kama kazi za mabalozi kwa miaka hiyo ilionekana kuwa na tija, sioni ni kwanini sasa tuipuuze. Suala la ulinzi na usalama wa nchi yetu halipaswi kuwa la kiitikadi.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika


2243 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!