Mualiko wa futari wa Biden kusherehekea mwezi Mtukufu wa Ramadhan umesusiwa, huku vikundi vya Waislamu vikisusia na kuandaa maandamano ya kupinga uungaji mkono wa Biden kwa kuzingirwa kwa Gaza na vita vya kikatili vya Israeli dhidi ya Gaza.

Ikulu ya White House ilifanya karamu ndogo ya futari kusherehekea mwezi Mtukufu wa Waislamu wa Ramadhan, huku waalikwa wengi wakisusia wito wa rais kwa sababu ya kukasirishwa kwa jamii ya Waislamu na siasa yake kuhusu vita vya kikatili vya Israel dhidi ya Gaza.

Viongozi kadhaa wa Kiislamu walitarajiwa kuhudhuria mkutano wa Jumanne na Rais wa Marekani Joe Biden, ni Makamu wa Rais Kamala Harris, na maafisa wa serikali ya Kiislamu na viongozi wa usalama wa taifa.

Baadhi ya watu ambao walikuwa wamehudhuria hafla kama hiyo katika miaka iliyopita, kama Meya Abdullah Hammoud wa Dearborn, Michigan, hawakualikwa.

Waislamu wengi, Waarabu na wanaharakati wanapinga vita wamekerwa na uungaji mkono wa Serikali ya Marekani kwa Israel na uvamizi wake wa kijeshi huko Gaza, ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kusababisha njaa katika eneo dogo la pwani la takriban watu milioni 2.3.

Thaer Ahmad alikuwa miongoni mwa walioalikwa kwenye Ikulu ya White House alisema kuwa ;

“Ilikuwa ni jambo la kushangaza kwamba nilikuwa Mpalestina pekee niliyehudhuria, huku watu wengi wakishindwa kuhudhuria, ingawa bado ndugu zetu wanaendelea kuteseka Gaza,” Ahmad aliiambia HuffPost.

Wamarekani wengi Waislamu wamekasirishwa na uungaji mkono wa Biden kwa Israel dhidi ya Gaza, Ikulu ya White House ilichagua kuandaa karamu ndogo ya iftar Jumanne jioni. Waliohudhuria walikuwa ni watu wanaofanya kazi katika serikali yake tu.

“Tunaishi katika ulimwengu tofauti,” alisema Wa’el Alzayat, anayeongoza “Emgage”, Shirika la Utetezi la Waislamu. “Ni jambo lisilo la kawaida kabisa. Na inasikitisha.”

Alzayat alihudhuria hafla ya mwaka jana, lakini alikataa mwaliko wa kufungua swaumu na Biden mwaka huu, akisema, “Haifai kufanya sherehe kama hii wakati kuna njaa huko Gaza.”

Baada ya Alzayat na wengine kukataa mwaliko, alisema Ikulu ya White House ilirekebisha mipango yake siku ya Jumatatu, na kuwaambia viongozi wa jumuiya kuwa ilitaka kuandaa mkutano unaozingatia siasa za serikali.

Alzayat bado alikataa, akiamini kwamba siku moja haitoshi kujiandaa kwa fursa ya kugeuza mawazo ya Biden juu ya mzozo huo.

Kukataa kula au hata kuwa chumba kimoja na rais ni ushahidi wazi jinsi uhusiano kati ya Biden na jamii ya Waislamu ulivyovunjika miezi sita baada ya Israeli kuanza vita vyake dhidi ya Gaza.

Rais wa chama cha Democratic alipoingia madarakani miaka mitatu iliyopita, viongozi wengi wa Kiislamu walikuwa na shauku ya kufunga ukurasa wa chuki wa Donald Trump, ikiwa ni pamoja na ahadi yake ya kampeni ya kutekeleza “kufunga na kuzuia kabisa Waislamu kuingia Marekani.”

Lakini sasa Wademokrat wanahofia kwamba kupoteza uungwaji mkono kwa Biden na baadhi ya Waislamu kunaweza kusaidia kusafisha njia kwa mpinzani wake wa chama cha Republican kurejea Ikulu ya White House. Uchaguzi wa mwaka huu unaweza kutegemea majimbo machache ya michauno, ikiwa ni pamoja na Michigan yenye idadi kubwa ya Waislamu.

Mohamad Habehh, mkurugenzi wa maendeleo wa Waislamu wa Marekani kwa ajili ya Wapalestina, aliiambia Al Jazeera kwamba Biden hawezi kudai kuwajali Wamarekani Waislamu “kama hatakomesha uungaji mkono wake kwa Israeli.”

By Jamhuri