Wiki iliyopita hadithi hii iliishia katika aya inayosema: “Mwanzoni nilimwona akiwa na urefu wa kawaida, lakini kadiri tulivyokaribiana alizidi kurefuka. Alikuwa anaongezeka mita moja kila hatua aliyopiga. Na baadaye nyayo za miguu yake zikawa zimeziba barabara kwa ukubwa wake,  nikaogopa asije akanikanyaga! Huwi! Huwi! Huwi!” Je, unafahamu nini kinafuata? Endelea…

Nikaanza kupiga kelele katika kuzimia/kufa. Mara nikaona jamaa zangu wakinishikilia kwa nguvu kwenye jeneza langu. Baba alikuwepo na ndugu zangu wote walikuwepo, majirani pia nilikuwa nawaona wakipita hapa na pale. Hata viongozi wa serikali walikuwa wengi, wakiwa pamoja na kina July, Ally, Ben na hata huyu wa sasa alikuwepo.

Wengine ni pamoja na kina Gaude na Kieli. Aloo! Walikuwa wengi sana. Hali hii ilinifanya nione fahari kwa vile kumbe hata mimi ninaheshimiwa na viongozi hawa wa kisiasa. Niliwapenda, lakini nikaamua niendelee na kufa/kuzimia. Basi, nikatulia kwenye jeneza langu. Niliendelea kuwaona kina mama macho yao yameiva kwa kulia. Tatizo ni kuwa sikuweza kuwaona vizuri kwa vile kulikuwa na utusitusi au kama ukungu ukungu hivi.

Bwana Bulongo Gwike, hivi jina lako huwa linaashiria nini hasa? Ni jina la kabila gani? Lina maana gani? Basi bwana, yule dada tulipishana naye nikiwa na hofu ya kukanyagwa na kusiginwa kama karanga. Bahati ilikuwa kwangu. Hakunikanyaga. Nikaendelea kukimbia sijui niendako; wala sijui nitokako.

 Sasa pale nyumbani watu walikuwa wamekazana kutayarisha kaburi langu; na matayarisho ya mazishi kwa ujumla. Hapo niligundua kabisa kuwa kweli watu ni miongoni mwa viumbe ambao hawajui lolote kuhusu nini hasa baada ya kifo.

Mlikazana wote kila mtu alifanya hiki na yule kile kuhusu kifo changu. Niliwaonea huruma sana kwa vile hamkujua mlilokuwa mnafanya, mimi nilikuwa nimechutama pale mlangoni!

Je, ni kweli kuwa mlikuwa hamnioni? Mbona mimi nilikuwa ninawaona! Kilichokuwa kinaendelea ni kuwa mlikuwa mnatayarisha shina la mgomba! Mlipomaliza kuosha lile shina mlilivalisha ile suti nzuri aliyoninunulia baba ya kuzikiwa. Halafu mkalipaka mafuta na   kulipulizia manukato ya thamani!

Nilitaka kuwacheka kwa mahangaiko yenu hayo, lakini bado sikuwa na uwezo wa kuwasiliana na watu wa dunia hii!

Muda ulipofika wa kwenda malaloni mlilibeba lile shina la mgomba na kulipeleka malaloni. Niliambatana nanyi mpaka huko malaloni, mkalisalia lile shina na kuliombea mema huko peponi. Baadaye ndugu walipewa nafasi ya kutupia mchanga – ishara ya kuniaga mara ya mwisho!

Maskini mama yangu alikuwa na wakati mgumu sana wa kuniaga. Alishikiliwa na kina mama wawili huku na huko, alikuja akatupia mchanga na oh! Nilimwona kama alikuwa anataka kutumbukia shimoni mwangu! Wale kina mama wakamshika kwa nguvu zaidi na kumzoazoa ili atoke pale shimoni. Walifanikiwa baada ya jitihada za ziada. Baadaye ikafika zamu ya kunifukia!

Vijana walifanya zoezi hili kwa nguvu na umoja wa ajabu. Je, walifanya hivyo ili watoke hapo au ndiyo ada ya shughuli yenyewe? Wengine walitania eti walifanya hivyo ili wawahi msosi! Sijui! Walipokuwa wanakaribia kumaliza kufukia kaburi langu yule bibi kizee alinijia akanigusa mabegani tukaanza kuondoka sehemu hiyo.

Mimi sikujua yakini tunakwenda wapi! Lakini tuliondoka sehemu hiyo na zile siku tatu ndizo nilizoona yale mashindano ya wale vijana na yule kijana na dada yake na yule kijana wa kuku na wale madada wenye miguu ya farasi. Na maziko yangu yakaishia hapo. Nasikia eti baba alichinja ng’ombe ili kuniaga na kutambika tambiko.

Sehemu inayofuata rafiki yangu Bulongo nilikuja kuitwa safari ya kurudi duniani baada ya kuchoropoka kule Gamboshi. Mwendo wa yule bibi ulikuwa wa kasi na hatimaye nikaacha kumwona. Hivi ndivyo tulivyopotezana na yule bibi kizee, nikabaki peke yangu kwenye nchi nisiyoijua. Miaka takriban mitatu hivi mpaka mlipokuja kunikamata nilipokuwa ninamkimbia yule kifaru kule mbugani!

Akanitelekeza kusikojulikana huyu bibi kizee, lakini baadaye nilikuja kujua kuwa aliamua kuniacha kwa vile eti nilikuwa mbishi na huenda mababu zangu wa ahera hawakuridhika na namna nilivyotolewa kwetu. Eti ilikuwa nipewe na mababu na wahenga hawa cheo kikubwa cha kutawala nchi hii. Sijui, labda walitaka niwe mbunge wa eneo hili au labda niwe waziri mkuu au hata rais wa nchi, sijui.

Jamani niliachwa kusikojulikana na yule bibi kizee. Nikawa ninakimbia. Nilikimbia kutoka sehemu hiyo na baadaye nikapishana na yule dada kama nilivyosema hapo awali. Niliendelea kukimbia ninaelekea kusikojulikana na ninakotoka hakujulikani. Niliendelea kukimbia siku nzima.

Sijui nilikimbia kwa muda gani. Mimi katika kufa/kuzimia nikaendelea kukimbia. Moyo wangu ukiwa umejawa hofu kweli kweli. Nilikimbia kutwa nzima. Baadaye nikaanza kuhisi kuchoka. Nilitafuta sehemu nikalala. Usingizi ulinichukua mara moja na nililala hapo kwa muda mrefu sana, lakini sijui kwa yakini ulikuwa muda gani.

Nilipoamka nilianza kupata fahamu za kidunia. Nilisikia uchovu na njaa pia ilikuwa imenikaba. Niliamua kubaki nimefumba macho huku nikitafakari nifanye nini. Nilitulia hapo na baadaye nikaamua kufumbua macho yangu angalau nibaini kama kuna tunda pori angalau nilile.

Kufumbua kwangu  macho  niliusikia mwili wangu si wa kawaida.  Hapo tena hofu ikazidi kuongezeka! Nikapepesa macho huku na huko. Mh! Nilichokiona ni miujiza. Jamani niliona viumbe wadogo wadogo mfano wetu sisi watu wa kawaida. Ila wao walikuwa wadogo wadogo sana!

Aliyekuwa mrefu kupita wenzake alikuwa apata sentimita 10, lakini walio wengi wastani wa urefu wao, ulikuwa sentimita nane au tisa hivi. Ilikuwa ajabu! Kila kiungo na umbo lao lilifanana nasi sana, ila tu kwa udogo ndiyo tofauti kubwa. Kwa hakika nilianza kuyatilia shaka macho yangu, labda yameanza kunihuni au labda akili yangu imegoma kufanya kazi.

Hapana! Kile nilichokiona ndiyo uhalisia hasa, lakini je, na hawa viumbe niwaiteje! Wanadamu wenzangu? Hapana itakuwa ni kuchanganyikiwa. Wanadamu wana mambo yao yanayofanana na uanadamu wao na hawa viumbe kwa hakika si wanadamu.

Nilijaribu kuwahesabu haraka haraka wale waliokuwa kifuani kwangu nikapata wako kama hamsini, licha ya wale waliokuwa sehemu nyingine za mwili wakinitafiti.

Nilipepesa macho hadi miguuni kwangu, huko niliona walikuwa wameweka ngazi kwenye muundi wangu ya kupandia kuja juu mwilini kwangu.

Maskini viumbe hawa kuona hivyo wakaingiwa na hofu na kuanza kukimbia huku na huko kifuani kwangu. Ilibidi nitulie kwanza kwa sababu waliokuwa chini ningeweza kuwakandamiza wakati wa kuamka. Hapa busara ndiyo ilitakiwa. Nikatoa fursa ili wale waliokuwa kifuani waweze kutoka na waliokuwa karibu nami hapo chini wakae mbali kwenye usalama. Bila shaka nao walikuwa wananishangaa. Pia kuona jitu kubwa namna hili!

Baadaye niliamka nikawa ninajiuliza nini hasa maana ya mambo haya? Je, nilikuwa sehemu gani ya dunia? Je, hawa viumbe nitaweza kuwasiliana nao ili angalau nipate kujua nilipo? Je, wanaweza kuongea lugha yangu?

Nilipokuwa katika mawazo hayo mazito, nilijikuta ninashusha pumzi na wale viumbe maskini walikuwa karibu na pua yangu walipeperushwa na baadhi yao wakakwama kwenye malaika zangu.

Walijiwa na hofu wasiwe na hili wala lile wakingojea kudra za Mwenyezi Mungu kupona. Viumbe hawa wadogo nikaona kuwa kwa vile walifanana sana na sisi, basi niwaite watu wadogo.

Watu hawa walikuwa wadogo sana, na kwa kweli kuwako kwangu katika nchi yao, ilileta adha kwa sababu zile siku  chache nilizokaa nchini mwao ilileta kero, kwanza kwa upande wa chakula walichonitengenezea kulitosha watu hao wapatao elfu moja wakati mimi ni mlo mmoja.

Tatizo jingine ni pale nilipotaka kutembea kidogo; ilipaswa kule nilikoelekea watu wataarifiwe kuwa nitapita eneo hilo, kwa hiyo wachukue tahadhari nisije nikawakanyaga kwa bahati mbaya nikiwa katika mishemishe zangu. Hii ilikuwa kero sana kwa wenyeji wangu.

Je, unafahamu nini kiliendelea baada ya hapo? Usikose sehemu ya tatu yenye kusimulia mambo mazito kuhusu Gamboshi. Mtunzi wa hadithi hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa Na. 0755629650.

By Jamhuri