Kuna wakati huwa naamini hakuna sababu ya kupeana salamu kutokana na matukio yanayotokea, kwa kawaida salamu anapewa mtu muungwana na anayepokea ni muungwana, lakini sasa hivi unaweza kutoa salamu ndiyo ukawa mwanzo wa kukaribisha nyoka katika mwili wako, kwa maana ya adui kukujua na kutekeleza adhima yake ya ubaya.

Ninazidi kusikitika jinsi ambavyo hali inazidi kuwa mbaya kiusalama katika kipindi hiki ambacho watu wameongezeka na ukoo unazidi kuwa mkubwa tofauti na zamani ambapo tulikuwa wachache na ukoo mdogo. Zamani tulikuwa salama sana pamoja na kuishi vijijini hasa kusiko na umeme wala maji, majirani wala polisi lakini tuliishi na wanyama wakali kama simba na tembo, achilia mbali nyoka ambao tuliwazoea kama majirani wanaovizia milango ikiwa wazi waingie wajisitiri na baridi au joto.

Inawezekana kwa kuchelewa sana kwa taarifa huku vijijini, nimesikia wiki jana kuna binti amefanyiwa mauaji ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani kwake akitoka darasani  – akirejea nyumbani kwake, karibu kabisa na darasa lake huko mjini, imeniuma kiasi kwamba najiuliza mbona sisi tulisoma shule za kusafiri kila siku na tuliweza kurejea salama kila siku?

Najua kwamba wengi mmesoma shule hizi za serikali yetu ambazo tulibadili mfumo wa kumaliza darasa la saba badala ya la nne, najua wengi wenu mmesoma shule ambazo umbali wake hauzidi kilometa moja, najua kwamba nazungumza na watu ambao wengi wao ni wale ambao mmejengwa na mfumo wa demokrasia zaidi  – utii bila shuruti.

Sisi tuliishia darasa la nne kwa shule iliyokuwa kilometa ishirini na tulikuwa hatuna demokrasia ya kujadiliana sana bila vitendo, tulikuwa wazalendo na tulisikiliza zaidi wakubwa kuliko kudadisi, na wakubwa hao walikuwa wakweli kabisa katika mazungumzo yao na walimu walikuwa wanatufundisha mambo mema na si mambo ya ovyo kama baadhi ya walimu wa leo wanavyofanya.

Limenisikitisha sana  jambo la mauaji ya mwanafunzi asiye na hatia ndani ya nusu kilomita, tena kwa mwanafunzi ambaye alikuwa hana kitu chenye thamani ya maisha yake, ni kama vile nimeambiwa huu ndio mwisho wa dunia umefika. Nakumbuka maisha yetu na mazingira ya hatari yaliyokuwepo lakini kulikuwa hakuna mambo haya ya mauaji ya binadamu.

Hili si jambo la kwanza kulisikia, ninayasikia mengi sana yanayohusu uhai wa binadamu kufanyiwa ukatili, wapo waliokamatwa huko mikoani wakitaka kumtoa mtoto kafara, wapo waliouziana mtoto na akakatwa kiungo cha mwili na kusababisha mauti, maswali ya kujiuliza yapo mengi sana kwa nini ilitokea na tufanye nini kwa kizazi hiki cha mwisho.

Nimejiuliza sana, kwani ulinzi shirikishi ulikwisha lini? Baada ya kuona kuna tatizo katika sheria za mgambo na sungusungu? Kilichotokea ni ubora wa uundaji wa muungano wa polisi na hao walinzi shirikishi ambao wengi wao walionekana kuwa washiriki wa mambo ya ovyo?

Sungusungu iliishia wapi na kwa sababu zipi? Ninavyokumbuka ni kwamba vijana wale tulikuwa tukiwalipa ili wafanye kazi ya usalama wetu katika vijiji na mitaa, ni kitu gani ambacho kiliwafanya sungusungu wakaachishwa majukumu yao?

Vipi kuhusu JKT waliomaliza kazi zao kuwasaidia hao askari wetu ambao wako wachache? Ni kweli kwamba hawatambuliki wakitoa msaada mahali ambapo hakuna askari? Ule mfumo wetu wa uzalendo wa kila mtu kuwa mlinzi wa mali yake na ya mwenzake nao ulipitwa na wakati? Nina hofu huenda fursa hizi muhimu zilitumiwa vibaya na wachache ambao walistahili kuchukuliwa hatua.

Uelewa wa wananchi kwa polisi ni tatizo jingine na hapa ndipo unapoona maovu yakifanyika mbele ya macho yako na unashindwa kutoa msaada, inakuwaje msamaria mwema anabeba jukumu la kuwa mtuhumiwa namba moja? Hivi tunadhani ni busara kumshikilia aliyetoa msaada kwa mwathirika au mwathirika kutopata msaada?

Najiuliza, hospitalini kukoje ukimpeleka mtu aliyepata ajali au kupoteza maisha? Tufanye nini kutoka katika ujinga huu wa kisasa katika kusaidiana matatizo, ule umoja wetu wa zamani  uko wapi siku hizi za unyama uliopitiliza? Kweli tutafika tuendako kwenye maelezo ya nchi yenye amani? Hatua gani zinachukuliwa ili kulinda utamaduni wetu wa kusaidiana?

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri