Dkt. Massawe ametoa wito kwa wadau kuitumia GST katika Tafiti za Madini

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kufanya utafiti wa madini muhimu na madini mkakati (critical and strategic minerals) katika Wilaya za Tunduru Mkoani Ruvuma na Kilwa Mkoani Lindi.

Kazi hizo za utafiti zinafanyika kupitia ushauri elekezi (consultancy) wa GST kwa Kampuni ya Mineral Access System (T) Limited kwenye leseni zake za utafiti wa madini ya nickel, shaba na cobalt zilizopo kwenye Hifadhi ya Mistu katika Kijiji cha Nanjilinji Wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi pamoja na eneo la Mbesa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo la Utafiti kwa lengo la kukagua maendeleo ya shughuli za ugani, Mkurugenzi wa Huduma za Jiolojia Dkt. Ronald Massawe amesema, GST imejipanga kikamilifu kufanya tafiti mbalimbali za madini ikiwemo kutoa ushauri elekezi kupitia wataalumu wake wa ndani wenye uzoefu mkubwa na kwamba taasisi hiyo ina vifaa vya kisasa na vilivyo na ubora mkubwa kwa ajili ya Utafiti wa Madini.

Aidha, Dkt. Massawe ametoa wito kwa wadau wa Sekta ya Madini kuitumia GST katika kufanya utafiti wa madini kwenye maeneo yao kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji ili kutambua uwepo wa madini na mwelekeo wa miamba ya madini katika maeneo ya leseni zao.

Pamoja na Mambo mengine, Dkt. Massawe amewapongeza wataalumu wa GST kwa kushirikiana pamoja kufanya tafiti za kijiolojia, Jiofizikia na Jiokemia kwa weledi na ufanisi mkubwa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Massawe ameahidi kukamilisha shughuli za Utafiti zinazoendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Mbesa lililopo Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma na eneo la Nanjilinji Wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi kwa wakati na kwa weledi mkubwa.

Awali, Dkt. Massawe alikutana na kufanya mazungumzo na Wawekezaji wa Kampuni ya Mineral Access System (T) Limited ambapo walijadili changamoto mbalimbali na kuzipatia majibu.

By Jamhuri