Na Mary Margwe, JamhuriMedia, Simanjiro

Wachimbaji wadogo na wa kati wa Madini ya Tanzanite katika Mji Mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wanatarajia kunufaika baada ya Taasisi ya jiolojia na utafiti wa madini Tanzania (GST) iiyotumia ndege nyuki kufanya utafiti wa kubaini maeneo yenye madini ya Tanzanite mji mdogo.

Utafiti huo utasaidia kuwaepusha wachimbaji wadogo na wakati kuepuka hasara kwenye uchimbaji wao kwani watachimba kwa kutumia taarifa ya utafiti huo unaoonyesha miamba ya uzalishaji madini yalipo.

Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi mkuu wa GST, Dkt. Mussa Budeba, wakati akizungumza baada ya kufanyika kwa utafiti wa awali ambapo amesema Utafiti huo utasaidia urahisi wa upatikanaji wa madini ya Tanzanite katika maeneo husika.

Dkt. Budeba amesema utafiti huo utawaepusha wachimbaji wadogo na wa kati juu ya hasara ya kuchimba kwa mazoea, maeneo yasiyo na madini kwani kwa awamu ya kwanza wamepima kwenye eneo la Kitalu C na D.

Aidha Dkt. Budeba amesema wanatarajia kufanya utafiti kwa asilimia 50 kwenye maeneo yote nchini hadi ifikapo mwaka 2030 ambapo kwa sasa Utafiti umefanywa kwa asilimia 16 kwa baadhi ya maachimbo.

“Waziri wa Madini Anthony Mavunde amekuja na vision ya 2030 madini ni maisha na utajiri, kwa kufanya utafiti na pia tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea bajeti,” amesema Dkt. Budeba.

Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Nchagwa Marwa amesema utafiti huo wa awali uliofanywa na GST, umehusisha vitalu viwili vya C na D na utafiti ujao utahusisha maeneo mengine yaliyobaki.

Marwa amesema GST watarejea tena kwa kuongeza wigo wa kufanya utafiti kwenye maeneo yote ya machimbo ya amadini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani.

” GST itarejea tena Kwa kuongezawigo wa kufanya Utafiti kwenye maeneo yote ya Machimbo ya Madini ya Tanzanite katika Mji wetu mdogo wa Mirerani” amesema Marwa.

Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya Franone Mining Ltd, Vitus Ndakize amesema utafiti huo utatanua wigo wa uchimbaji madini kwa kuepuka uchimbaji wa kubahatisha.

Ndakize amesema utafiti utakuwa chachu kwa wachimbaji madini ya Tanzanite, kwani utapunguza gharama kwa kuchimba huku wakifuta taarifa zilizopatikana kupitia GST.

Mchimbaji mdogo wa madini ya Tanzanite wa kitalu D, Paulo Mwanache amesema utafiti huo utakuwa njia rahisi kwao ya kufanya uchimbaji usiokuwa na hasara tofauti na mwanzo.

“Utafiti umetuonyesha maeneo yenye miamba iliyolala na wapi penye madini mengi na wakatueleza sababu ya madini kuungua chini kabla ya uzalishaji wake,” amesema Mwanache.