Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Idadi ya waliofariki katika ajali ya moto iliyoua watoto watatu wa familia moja jijini Arusha imeongezeka baada ya baba wa watoto hao askari CRI wa TANAPA, Zuberi Hassan Msemo kufariki.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, Jeradi Nonkwe, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo marehemu huyo alikuwa ni baba wa watoto watatu waliofariki kwa ajali ya moto iliyotokea Juni 22, 2024.

Kamanda amewataja watoto waliofariki kuwa ni Mariam Zuberi (9), Salma Zuberi (7) na Bisma Zuberi (3) ambapo mama wa watoto hao, Jasmine Khatibu (33), Mariam Mussa (60), Mwanaid Aldina (50), Mussa Msemo (34), AbdulKarim Ramadhan (9) na dada wa kazi aliyefahamika kwa jina moja la Ester (20) wanaendelea na matibabu.

Kamanda amesema kuwa baba huyo amefariki jana Jumapili Juni 23, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini Arusha ambapo amesema kuwa chanzo chake ni kutokana na kumeza moshi mwingi alipokuwa akijaribu kuwaita watu waje wasaidie kuwaokoa.”

Kamanda Nonkwe amesema kuwa ajali hiyo imetokea katika Mtaa wa Olmatejoo jijini Arusha, baada ya moto kutokea ndani ya nyumba ambapo chanzo chake kimedaiwa ni kompyuta mpakato (laptop) iliyokuwa imechomekwa kwenye soketi ya umeme kushika moto na vitu vingine.