Katika kipindi cha miaka kadhaa sasa, Watanzania wengi wanaishi kwa manung’uniko yanayotokana na kukosa haki zao za msingi huku waliopatiwa jukumu hilo wakiwabeza.
Tumeshuhudia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) iliporatibu upatikanaji wa vitambulisho hivyo, huku wananchi wengi wakishindwa kuvipata.


 Hakuna ubishi kwamba vitambulisho hivyo viliibua vurugu na hata kuhatarisha amani kwa baadhi ya maeneo. Ilikuwa ni mshikemshike. Shukrani kwa NIDA, walielewa na kuanza kujisahihisha ingawa changamoto bado zipo.
  Kutokana na nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ililazimika kuandikisha upya vitambulisho vya kupigia kura.
 Katika harakati za utoaji vitambulisho hivyo kwa ajili ya kupigia kura, kumekuwa na changamoto zinazodhalilisha utu wa mtu, manyanyaso na kila aina ya karaha kwa Mtanzania.


 NEC ndiyo inayohusika na jambo hili ambalo limerasimishwa kwa halmashauri nchini. jambo hili hapa nchini limekuwa kama anasa; siyo halali kwa wananchi wenye haki ya kupatiwa vitambulisho hivi huku wengine wakiishia kutoa malipo ili kuweza kuvipata.
Ni jambo lililo wazi kuwa NEC haikujipanga ipasavyo kwa hili. Kutokana na umuhimu wa vitambulisho hivi, ilitakiwa kuwa imejipanga na siyo kukurupuka na kusababisha mateso kwa ndugu zetu bila sababu za msingi.  
Watanzania sasa wanalala nje ya nyumba zao, wanakesha kwenye foleni za kujiandikisha kupiga kura, hawana tena uhalali wa kukaa na familia zao huku kula yao ikiwa ya kubahatisha.


NEC imesababisha kusambaratika kwa upendo katika familia zetu; imesababisha kuondokewa na ndugu yetu huku wapiga kura wakinyanyasika katika vituo vya kujiandikisha kwa siku kadhaa sasa tangu uandikishaji ulipoanza.
  Uchaguzi wa mwaka huu ulifahamika tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu miaka mitano iliyopita, hivyo hakuna kushtukiza. Serikali ilipaswa kujipanga katika hili kuliko kutesa watu wake huku uandikishaji ukiwa kama anasa na kuwanyima haki zao za msingi.
Tanzania imekuwa na viongozi wasio na uchungu na watu wao, ambapo wamejiweka mbali na waongozwa huku wanaoongozwa wakidhaniwa kutokuzijua haki zao, jambo linalowalazimu wananchi kutafuta mbinu mbadala hata kama ni kulala kwenye vituo vya kujiandikishia ili kupata haki yao hiyo ya msingi.
Katika hili NEC inabaka haki za wapiga kura. Inalo jukumu la kuwaomba radhi Watanzania kutokana na kuwadhalilisha katika kuwapatia haki yao ya kikatiba.


Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, anatakiwa kuwaomba radhi Watanzania kutokana na manyanyaso wanayoyapata kila siku huku wengi wao kutokuwa na uhakika wa kupata haki yao ya msingi.
Watanzania wanafanyiwa utani na dhihaka isiyo na maana. Wanadhihakiwa katika kupatiwa haki yao ya msingi; wanadhihakiwa na watu wa hovyo hovyo kutokana na kufanyiwa vitendo vya hovyo hovyo.
Jaji Lubuva analo jukumu la kujiuliza mustakabali wa Taifa letu, anatakiwa kutambua ya kuwa iwapo hatakuwa makini anaweza kuwa chanzo cha misuguano na hatimaye vurugu zinazoweza kuepukika.
Ni vyema akawa na msimamo thabiti katika kipindi hiki. Asimame kwa kuhakikisha kila mpiga kura anapata haki yake ya kuandikishwa katika daftari za mpiga kura ili kuepuka visababishi vya uvunjifu wa amani katika kipindi hiki ambacho wananchi wengi wamekuwa na mwamko mkubwa wa kujiandikisha na hatimaye kupiga kura.


Watanzania wanailalamikia NEC na kuilaumu Serikali kwa kuwa na utaratibu mbovu wa utoaji wa vitambulisho hivyo. Wengine kutokana na kutokuwa na uhakika wa kupata haki yao hiyo, wanalazimika kulala vituoni huku wengi wao wakifika katika vituo hivyo vya kujiandikisha kuanzia saa sita za usiku ili kuwahi foleni. Haijawahi kutokea.


Natambua kutokana na busara za NEC, pamoja na kuongeza siku hizo nne wataweza kutafakari hali ilivyo na kutoa muda wa kutosha kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao ya msingi, ikiwa ni pamoja na kuondokana na malalamiko yasiyo na sababu kwa Tume hiyo kuwa inahujumu.
Watanzania wanahitaji mabadiliko, mabadiliko ya utendaji katika taasisi zote nchini, hivyo basi ni jukumu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa moja ya taasisi za Serikali zitakazosimamia mabadiliko hayo kwa kufanya kazi zake kwa ufanisi, na kuondoa manung’uniko ya aina yoyote kutoka kwa Watanzania.
Watanzania wanayo haki ya kupata haki zao za msingi bila kubughudhiwa kiasi cha kuzigeuza na kuwa anasa kwao. Tanzania ni nchi yetu sote, tunalo jukumu la kuilinda na kuijenga kwa pamoja bila kuzidi kuongeza chuki, misakamo na mpasuko usio wa lazimia.
Mungu ibariki Tanzania

 
2504 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!