Wilaya, majimbo si suluhu ya matatizo

JKNamshuruku Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya njema na amani. Ni vyema tukamshukuru Mungu kila wakati kwa sababu tunaendelea kuyashuhudia mapenzi yake mema kwetu.
Pili, niombe radhi kwa sababu lugha ya Kiswahili ni ngumu, hivyo katika kuandika inawezekana nikakosea hapa na pale ingawa si nia yangu kufanya hivyo. Ikitokea ikawa hivyo, basi ni bahati mbaya na tusameheane kwa wale watakaokuwa wamekwazwa.
Ni siku chache zilizopita nilisikia kupitia vyombo vya habari kuwa wilaya mpya zinaanzishwa pamoja majimbo mapya ya uchaguzi. Kwa sasa, pamoja na wilaya tano zilizotangazwa juzi tu, Tanzania inakuwa na wilaya 168.
Unaposikia suala kama hilo, kimsingi unasema si vibaya kuwa na wilaya nyingi iwezekanavyo maana huduma muhimu zitakuwa karibu na wahitaji ambao ni wananchi vijijini na maeneo ya mijini.
  Tusijali ni wilaya ngapi tutazianzisha isipokuwa tuhoji; je, wilaya hizo zinatimiza matakwa na haja za Watanzania? Au tunaanzisha wilaya kwa makusudi ya kutimiza nia tofauti na hiyo?
 Mara nyingi huwa nasikia kuwa kuanzisha wilaya mpya mahali ni kuimarisha utawala ngazi za chini; kuimarisha ulinzi na usalama na hasa iwapo eneo la wilaya fulani likiwa ni kubwa kupita kiasi; kuweza kutatua kero za wananchi; na kadhalika.


Yote haya ni sahihi na ni vyema kuyasimamia na kuyatekeleza iwapo inaonekana ni muhimu kufanya hivyo.
Kwa upande wa majimbo ya uchaguzi yanapoongezeka tunapata wawakilishi wa wananchi wengi bungeni. Vilevile, ikiwa ndivyo ilivyo ni jambo jema kupata wawakilishi au wasemaji wa wananchi wengi huko bungeni.   
 Sasa tuchukulie kuwa Tanzania ina wabunge wengi kutoka kila kona ya nchi (mathalani zaidi ya 400) na kukawapo wilaya nyingi pengine zaidi ya 150; je, matatizo au kwa maneno mengine changamoto zinazoikabili jamii ya Tanzania tutakuwa tumepata dawa yake?
 Nadhani kiuhalisia Watanzania tulio wengi tunadhani kuwa matatizo mengi yanayotukabili hayatokani na kutokuwapo wilaya nyingi au majimbo mengi, bali ni kukosekana mikakati madhubuti ya kitaifa ya kuiwezesha jamii kupata huduma bora za kijamii kama elimu, afya, maji, miundombinu, usalama wa chakula na kushindwa kudhibiti uharibifu wa mazingira.


 Wakati mwingine tunasingizia umaskini kwa kukosa kipato cha kutosha, lakini yawezekana kuwa si umaskini, bali kutokuwa na mipango madhubuti na mikakati yenye mwelekeo halisi wa kumtoa Mtanzania kwenye uduni wa maisha na kumwingiza katika hali ya kusonga mbele kwa kutumia rasilimali na fursa tulizonazo.
Kimsingi huduma za kijamii zikiimarishwa; kwa mfano, watoto wetu wakapata sehemu mzuri za kusomea na kuelimishwa vizuri, huduma za afya zikaimarika, maji yakapatikana bila shida, miundombinu ikawa mizuri, Watanzania hawatahitaji wabunge au wakuu wa wilaya wengi. Watabaki wabunge wachache tu wa kuisimamia Serikali tena wasiozidi 100 kwa nchi nzima (kupunguza gharama).


Sasa wanakuwapo wabunge wengi kwa kisingizio cha kuimarisha demokrasia nchini kupitia uwakilishi wa wananchi. Vilevile, kuna kisingizo kuwa demokrasia ni gharama sana, hivyo Serikali kuweza kutumia fedha nyingi kuweza kuliendesha Bunge wakati fedha hizo zingetumika kuwaletea wananchi maendeleo wanayoyataka.
Kwa sasa tunasema hali ya mawasiliano imeboreshwa na kwa kuwapo huduma za kifedha kupitia simu za mikononi tumeweza kutoa huduma kama hizo hadi vijijini. Hali hii imekuja si kwa kuwa wilaya ni nyingi au wabunge ni wengi, bali ni kwa kuwa na miundombinu sehemu nyingi nchini.
Kwa mfano, kama hali za shule zitaimarishwa, walimu wakawa na nyumba za kuishi, madarasa yakawa mazuri, maabara zikawapo na vifaa vyake muhimu, vitabu vya kutosha vikapatikana; maslahi ya walimu yakawekwa sawa; na miuondombinu mingine ikawapo pamoja na huduma kadhaa za kijamii kuimarika; hakutakuwapo na ‘longolongo’ ya walimu kukataa kwenda kufanya kazi vijijini.


Wakati tulionao sasa inakuwa vigumu kwao na watumishi wengine wa Serikali; kufanya kazi vijijini kwa sababu hali ya maisha huko ni duni. Hii inatokana na kukosa mambo muhimu ya kijamii na si kwa sababu wilaya au wabunge ni wachache. Kama Taifa, tukijizatiti ipasavyo tukaimarisha utendaji na usimamizi na kuimarisha huduma za kijamii kama nilivyosema; maisha bora kwa kila Mtanzania yatawezekana bila ya kuongeza idadi ya wilaya au wabunge.
Huduma za kijamii zikiimarishwa hata kama wilaya ni chache, bado tutakuwa tunaweka msingi mzuri wa wananchi kujiletea maendeleo endelevu. Tumezoea kusikia Hospitali ya Wilaya au ya Mkoa kwa nini iwe hivyo? Huduma za afya ziende huko vijijini kwenye tarafa na kata ambako watu wapo na wanahitaji huduma hizo.


Kwa upande wa uhifadhi tumezembea mno maana hali ya mazingira nchini katika sekta ya misitu; na hasa misitu ya asili ni mbaya sana kiasi kwamba uhai wetu na wa viumbe wengine uko shakani kutokana na ukame; mito mingi kukauka, uzalishaji mazao kushuka kama ilivyotokea sehemu nyingi nchini mahindi yamekauka wakati yamefikia wakati wa kutoa maua na hatimaye kuanza kubeba kilichotarajiwa kiwe mahindi.
 Sasa hali imekuwa tofauti sana. Mvua imenyesha, lakini imeisha wakati mahindi hayajakomaa. Hali hiyo imesababisha wakulima wengi wahamaki wakijua kuwa hawatapata mavuno ya kutosha na itakuwa kilio cha kutokuwa na chakula cha kuhudumia familia hadi msimu mwingine wa mavuno.
Haya ni matokeo ya kuharibu mazingira hasa misitu ya asili ambayo uharibifu wake umekithiri kupita kiasi kutokana na kasi kubwa ya kukata miti. Kwa mfano, miti ya kutengeneza mkaa ni tishio kubwa la kuwapo misitu ya asili. Matumizi ya mkaa ni changamoto kubwa nchini kutokana na familia nyingi kushindwa kuzimudu gharama za nishati mbadala – gesi na umeme.


Tatizo la uharibifu wa mazingira linagusa jamii yetu si kwa uhaba wa chakula tu, bali pia na mizozo mingi kati ya wakulima na wafugaji kwa kugombea maeneo au sehemu za wafugaji kuchungia mifugo yao.
Vilevile, kati ya wafugaji/wakulima na wahifadhi kutokana na wafugaji kupeleka mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi kama mapori ya akiba au katika hifadhi za Taifa. Haishii hapo tu, pia wakulima huvamia sehemu zilizohifadhiwa kama misitu ya hifadhi au ya mazingira asilia kwa kufuata rutuba na maji. Hali kama hizo huleta ugomvi mkubwa na wakati mwingine vifo.


Nini kinachosababisha haya yote kutokea? Je, ni kwa kuwapo wilaya nyingi na majimbo ya uchaguzi mengi kutamaliza haya; au ni kwa kuimarisha huduma zinazotakiwa kwa wakulima na wafugaji? Tukitambua kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi (climate change) hazikwepeki, badala ya kuanzisha wilaya au majimbo ya uchaguzi, bora tukaimarisha uwezo wetu wa kuhifadhi maji ya mvua kwa kujenga mabwawa madogo madogo vijijini ili tuyatumia wakati wa ukame.
Shughuli kama hiyo tuhakikishe pia inafanyika kwenye maeneo ya wafugaji ili kuhakikisha nyanda za malisho zinaboreka na wafugaji wanamilikishwa maeneo ya kufugia au kuchungia mifugo yao kiuhifadhi na kwa misingi endelevu pasipo kushurutishwa.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa uhai wake aliwahi kusema “kupanga ni kuchagua”. Sasa tusipange kuongeza wilaya au majimbo, bali tuongeze nguvu kwa kuwapatia wananchi huduma bora za kijamii na masuala mengine muhimu. Hakuna lisilowezekana. Ni kufanya uamuzi sahihi na kwa faida ya Watanzania wengi.


 Rasilimali watu ipo ya kutosha. Maliasili tunazo na sasa uchumi wa gesi uko mbioni. Mwenyezi Mungu atupatie nini zaidi ya hayo? Tunahitaji uongozi bora na busara/hekima vitumike kumwendeleza Mtanzania kuliko kuendeleza zaidi siasa.
 Katiba inayopendekezwa ielekeze nguvu ya kuwapa wananchi uwezo wa kisheria wa kusimamia na kulinda rasilimali tulizo nazo kuliko ikiwa Katiba ya kuwalinda wachache.  
MWENYEZI MUNGU IBARIKI TANZANIA.