Na Mussa Augustine

Taasisi ya Hakielimu imeiomba Serikali kurejea upya mapendekezo yanayotolewa na wadau wa elimu kuhusu matumizi ya lugha ya kiswahili kama lugha ya kufundishia ngazi ya sekondari.

Rai hiyo imetolewa leo Machi 22,2023 na taasisi hiyo kupitia Mkurugenzi Mtendaji Dkt.Jonh Kalage wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kufuatia tukio la adhabu iliyopelekea kifo cha mwanafunzi Gloria Faustine wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Mwinuko Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.

Dkt.Kalage amesema kwamba watoto wanaotoka shule za msingi na hasa za umma kuingia kidato cha kwanza wanakua hawajawa tayari kuweza kutumia lugha ya kiingereza katika kuzungumza na kujifunzia hivyo kutumia kiswahili kama lugha ya kufundishia sekondari itatoa fursa kwa watoto kujifunza kwa ufasaha na kufundishwa vema kingereza na lugha nyingine kama lugha za kigeni.

Aidha amesema kwamba taasisi hiyo pia imependekeza dhana ya adhabu chanya kupewa mkazo katika mafunzo darasani na kazini kwa walimu ili kuwasaidia kuepukana na matumizi ya adhabu za kikatili akitolea mfano wakati wa mafunzo kwa vitendo kwa walimu utoaji wa adhabu unaweza kuwa moja ya eneo la tathmini.

“Hakielimu tunaendelea kusisitiza matumizi ya adhabu chanya na vichocheo chanya katika kuimarisha nidhamu na kujifunza,amesema Dkt Kalage.

Kwa upande wake Mshauri wa Hakielimu Mwelekezi Wilberforce Meena amesema kwamba taasisi hiyo haipingi matumizi ya lugha ya kingereza katika shule za sekondari bali lugha hiyo iwe kama lugha ya kigeni kwa ajili ya mawasiliano huku lugha ya kiswahili itumike kama lugha ya kufundishia.