HALMASHAURI YA WILAYA YA KISHAPU INAVYOBORESHA HUDUMA ZA ELIMU KUPITIA USHIRIKISHAJI WA NGUVU ZA WANANCHI

 Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga (kushoto) akiwa na wataalamu Afisa Mipango, Mang’era Mang’era na Afisa Elimu Msingi Wilaya, Sostenes Mbwilo wakipata maelezo kutoka kwa Afisa Elimu Ufundi, Moshi Balele kuhusu hatua za ujenzi wa chumba cha darasa shule ya msingi Migunga unajengwa pia kupitia nguvu za wananchi.
 Mradi wa vyoo vya wanafunzi katika shule ya msingi ukikaguliwa na maafisa elimu kutoka Halmashauri ukiwa katika hatua za umaliziaji mbali ya kutumika kwa fedha za Serikali pia mradi huo umechangiwa na nguvu kazi ya wananchi.
Sehemu ya vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Migunga ikiendelea kujegwa katika shule ya msingi Migunga ikiwa ni muendelezo wa mradi wa kuboresha huduma za sekta ya elimu. 

Serikali ya Tanzania imeweka mkazo kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi katika kujifunza ambayo ndiyo chachu ya mabadiliko na kufanya sekta hiyo nyeti ipige hatua.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ongezeko la uandikishaji, kuleta usawa wa kijinsia kwenye shule za msingi na sekondari nchini.Kumekuwa na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu na hivyo kufanya hamasa katika utendaji wa walimu ishuke na vivyo hivyo kwa wanafunzi.
 
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa pamoja ikishirikiana na Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu (Equip-Tanzania) imewekeza katika maendeleo ya sekta hiyo.Huu ni mpango unaotekelezwa na Serikali ili kuboresha mazingira ya mwanafunzi katika kujifunza ambao kwa sasa upo katika mikoa mitano ikiwemo Shinyanga, Tabora, Dodoma, Simiyu na Kigoma.
 
Itakumbukwa Equip-Tanzania ilianzishwa kwa malengo ya kutoa mafunzo na utendaji kazi kwa walimu pamoja na uongozi wa shule ambao tunashuhudia unavyoendelea kutekelezwa kupitia kwa walimu wakuu.

Pia inalenga kutekeleza mipango ya usimamizi wa elimu katika ngazi ya wilaya na mkoa kupitia kwa maofisa wake wa elimu ambao wanasimamia ngazi za chini yake zikiwemo kata.Mpango huo unalenga kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa taarifa mbalimbali, takwimu na uwajibikaji katika suala zima la elmu mashuleni unafanyika ili kuboresha sekta hiyo.
 
Lengo lingine la mpango huo ni ushirikishwaji wa jamii wa moja kwa moja katika masuala ya uchangiaji wa elimu katika miradi mbalimbali mashuleni ambayo inaendelea kutekelezwa.Hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu katika Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mpango huo wa kuboresha sekta yake ya elimu.
 
Ni dhahiri mpango huu unafanya kazi na uongozi wa mkoa na wilaya ili kuleta ufanisi na tija katika shule na pia kuimarisha mifumo inayozalisha shule. Kwa kifupi inasogeza rasilimali zaidi darasani na kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.Ushirikishaji wananchi Kwa vile shule zinategemea jamii ndiyo maana mpango huu unafanya kazi na asasi za kijamii kuelimisha jamii umuhimu wa elimu na uendeshaji wa shule hizo.
 
Ushirikiano huu unawafanya wazazi waweze kuona shule zinavyofanya kazi, jamii kupata taarifa sahihi za mapato na matumizi ya fedha za shule na hivyo waweze kutoa maoni ili kusaidia kuziboresha.Tukitupia macho namna ambavyo wazazi katika shule ya msingi Mhunze kata ya Kishapu tunaona namna ambavyo walivyoweza kutumia nguvu kazi zao katika ujenzi wa vyoo vya wanafunzi.Awali wakati wa changamoto hiyo kulisababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na harufu mbaya maeneo ya shule kutokana na wanafunzi kujisaidia vichakani.
 
Pia muda wa mapumziko ulikuwa mrefu tofauti na ilivyo kawaida ili kuwawezesha kupata muda wa kujisaidia huku wengine wakirudi majumbani kwa ajili hiyo.Aidha pamoja na hayo lakini pia kwa baadhi ya wanafunzi ilikuwa ikiwaathiri kisaikolojia ambapo wanafunzi hao waliona shule si sehemu salama tena kwa mustakabali wa afya zao.
 
Hivyo wanafunzi hao walikacha shule na hivyo kusababisha hali ya utoro huku wengine wakishindwa kuzingatia masomo wanayofundishwa hivyo kuchangia kushuka kwa taaluma.Hatua zilizochukuliwa Kutokana na hali hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kupitia idara zake za Mipango na ile ya Elimu Msingi zimekuja na mkakati wa kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa.
 
Mchumi kutoka Ofisa Mipango Kishapu, Noela Levira anasema kuwa halmashauri inatekeleza miradi mbalimbali ya elimu kwa kushirikisha nguvu za wananchi.Anasema kuwa wananchi wanapokusanya nguvu zao na kujenga japo maboma ya majengo mfano madarasa, nyumba za walimu au vyoo wanapofikia hatua hiyo Serikali inamalizia kujenga.  
 
Kama ilivyo mojawapo ya malengo ya mpango huo yaani ushirikishwaji wa wananchi, shule hiyo iliitisha kikao cha wananchi kujadili kuhusu utatuzi wa changamoto hiyo.Hivyo wananchi hao wakiwemo wazazi kwa umoja wao waliazimia kuchangia nguvu kazi katika kutekeleza mradi wa ujenzi wa vyoo kwa ajili ya wanafunzi hao.Jitihada hizo zimesaidia ukamilishaji wa jumla ya matundu 15 ya vyoo yamejengwa ambapo kati yake manane kwa ajili ya wasichana na saba ya wavulana.
 
Pia Uwiano wa wanafunzi na matumizi ya vyoo kwa wanafunzi umekuwa wa wastani na hivyo kumpa kila mmoja nafasi ya kujisitiri tofauti na ilivyokuwa zamani.Kutokana na uborekaji huo wa miundombinu ya vyoo shuleni mahudhurio ya wanafunzi yameongezeka kutoka asilimia 80 ya awali hadi kufikia asilimia 95 hivyo taaluma kupanda.Wadau wanazungumzia hali ya kuchangia elimu?
 
Mwakilishi wa wananchi, Isaka Maige anasema wazo la wazazi na wananchi kwa ujumla kuchangia nguvu kazi katika suala la elimu ni zuri na limekuwa na tija.Anatolea mfano wazo la kushirikisha wananchi katika ujenzi wa matundu ya vyoo lilipokelewa kwenye vikao na kutekelezwa ingawa kulikuwa na changamoto chache.
 
Anasema baadhi ya wananchi walikacha kuchangia na wengine wakidai kamati ya shule inatumia fedha bila kuzifanyia kazi inayopaswa kufanyika katika utekelezaji miradi.Hata hivyo, mzozo huo ulitatuliwa baada ya kamati hiyo kuonesha orodha na idadi ya wachangiaji na fedha zilizopatikana.

 

Ni dhahiri kuwa mafanikio katika shule zetu nchini yanayaweza kuchangiwa na ushirikishaji wa jamii na wadau mbalimbali na si tu kusubiri kila kitu kifanywe na Serikali.    Pia elimu ya darasani pekee haitoshi kumpatia mtoto ufaulu mzuri bali na afya yake ikiwa ni pamoja na mazingira yaimarike shuleni na nyumbani.