NA MWANDISHI WETU

DAR ES SALAAM

Kitendawili cha nini kilichomsukuma Hamza Mohammed kufanya mauaji ya watu wanne na baadaye naye kuuawa kinaendelea kuwa kigumu, baada ya mamlaka inayohusika na magonjwa ya afya ya akili kukana kumtibu.

Kitengo cha Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kinasema Hamza si miongoni mwa watu waliopata huduma kituoni hapo.

Daktari wa kitengo hicho, Dk. Praxeda Swai, anasema: “Katika kitengo hiki hakuna kumbukumbu za Hamza. Hajawahi kuhudumiwa au kuletwa hapa kwa kusumbuliwa na magonjwa ya akili.”

Hatua hii inafifisha madai yaliyoenea ya kwamba kijana huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya akili. Maradhi hayo yalichukuliwa na baadhi ya wadadisi kama ndiyo chanzo cha kufanya mauaji.

Wiki iliyopita Hamza aliwaua kwa risasi polisi watatu na askari wa kampuni ya ulinzi kabla ya polisi kumuua.

Tukio hilo lilitokea nje ya Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam. Pamoja na mauaji hayo, aliwajeruhi watu wengine sita wakiwamo polisi.

Kupunguzwa makali kwa hoja ya ugonjwa wa akili kunafanya kitendawili cha chanzo cha mauaji hayo kibaki kwenye madai mengine, yakiwamo ya ugaidi, na mvutano wake na polisi.

Hoja ya mvutano wake na polisi imekanushwa na mamlaka hiyo ingawa kuna maswali yanayotaka majibu ya kwanini Hamza aliwalenga polisi na kuwaacha raia waliokuwa katika magari binafsi na ya abiria.

Video zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, video moja inasikika sauti ya mtu akitamka maneno kadhaa yanayoelekezwa kwa viongozi wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi.

Madai ya ugaidi yanapewa uzito na taarifa za awali kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinazosema japo Hamza anaelezwa kwamba alikwenda katika masomo ya kawaida ya dini nchini Misri, mafunzo hayo yalihusisha pia matumizi ya silaha; jambo ambalo Polisi wanasema si jambo la kawaida kwa mafunzo ya kiroho.

“Tumebaini Misri alipata mafunzo katika kundi la (analitaja) ambalo lina itikadi za kigaidi. Nchini Misri kundi hilo limeharamishwa kwa kutangazwa kuwa ni la kigaidi,” kimesema chanzo cha JAMHURI.

Kati ya polisi watatu waliouawa, wawili walipokwa silaha katika kibanda cha kupumzikia eneo la makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Kenyatta Drive. Silaha hizo mbili pamoja na bastola ndizo zilizotumiwa na Hamza kufanya uhalifu.

Kachero mstaafu wa polisi, Peter Madeleka, anataja tukio hilo kama miongoni mwa matukio mabaya na ya kusikitisha yaliyowahi kutokea nchini.

“Askari wanapaswa kuzingatia mafunzo waliyopewa na wanayoendelea kupewa. Silaha ina nidhamu zake, sote tunafahamu. Askari mwenye silaha ni lazima awe standby (tayari) wakati wote. Ukiwa na silaha hautakiwi kuwa na mazungumzo na raia au mtu wa kawaida.

“Bila kulaumu kilichowakuta vijana wale, ifahamike kwamba eneo la gadi (lindo) si la kusogelewa kirahisi na mtu. Kama mtu ana shida ya kipolisi, aende kituoni, si kumkaribia askari kwenye lindo lake,” anasema Madeleka.

Anasema mtu yeyote anayeonekana mwelekeo wake ni kusogelea lindo anapaswa kujitambulisha haraka kwa askari. Kutofanya hivyo kutamfanya aonekane kuwa ni adui.

“Tunafundishwa katika masuala ya ulinzi kuwa askari mwenye silaha siku zote huwa ni target (mlengwa) kwa watu wenye malengo mabaya, kwa hiyo lazima kuwa makini sana,” anasema.

Baada ya kuwaua polisi kwa bastola na kuchukua bunduki mbili, Hamza alitembea kwenda jirani na Ubalozi wa Ufaransa.

Baadhi ya watu waliozungumza na JAMHURI wameonyesha shaka juu ya tukio hilo, hasa kitendo cha Hamza kuwalenga polisi.

“Ni kweli kwamba huwa kuna ‘bifu’ (ugomvi) la muda mrefu kati ya polisi na raia, ambalo hata sijui inatokana na nini, lakini si kwa kiwango kile.

“Hakutaka (Hamza) kuua watu wengine na ndiyo maana alitembea akiwa na silaha umbali mrefu (kutoka Kenyatta Drive) hadi mbele ya Ubalozi wa Ufaransa akiyapita magari ya kiraia na daladala.

“Kwa nini alifanya hivyo? Alitaka kutuma ujumbe gani? Na kwa nani? Pale ubalozini ndipo alipodumu kwa muda hadi alipouawa. Kwa nini?” anahoji raia huyo.

Mmoja wa maofisa wa usalama wanaochunguza tukio hilo anasema kitendo cha Hamza kujielekeza Ubalozi wa Ufaransa kililenga dhamira yake ya kutaka tukio hilo lipate sura ya kimataifa.

“Alishaamua kufa ndiyo maana alisimama muda mrefu katikati ya barabara mbele ya lango la ubalozi, nadhani alijua atauawa kwa hiyo alijua hiyo itafanya ulimwengu ufuatilie tukio hilo,” anasema.

Hata hivyo anasema inawezekana pia alikwenda hapo akikusudia kuingia ndani kuomba hifadhi, maana alijua baada ya mauaji aliyofanya asingebaki hai.

Wanaomfahamu Hamza wanasema alikuwa kijana mpole, mwenye maadili ya kidini, na msimamizi wa migodi ya dhahabu ya familia iliyopo Chunya mkoani Mbeya.

Kutokana na Hamza kwenda Misri kusoma, ndiyo maana kumekuwapo shaka kuwa alipata mafunzo ya kijeshi.

“Hata namna alivyokuwa amezishika zile bunduki mbili alizochukua kwa askari aliowaua, utafahamu kwamba anajua nini cha kufanya. Taarifa za kiintelijensia zinaonyesha alikuwa na mafunzo. Kama si ya hali ya juu, basi walau ya awali,” kinasema chanzo chetu.

Ofisa mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, amezungumzia hatua zinazopaswa kuchukuliwa na wananchi kwenye matukio ya hatari kama hilo lililotokea Agosti 25, mwaka huu. Kwenye tukio hilo wananchi kadhaa walionekana kuwa na shauku ya kusogea eneo la mapambano.

“Yapo mambo matatu ambayo raia asiye na mafunzo ya kijeshi anapaswa kuyafanya katika tukio kama hili.

“Kwanza, ni kukimbia haraka sana kutoka eneo la hatari au kulala chini mara moja anaposikia milio ya risasi kutoka kwa mtu asiyeaminika kama Hamza. Hii tunaiita self protection.

“Jambo la pili ni kujificha mbali na eneo la hatari; na tatu ni kutoa ushirikiano wa kila aina kwa askari wenye mafunzo waweze kudhibiti usalama wa eneo hilo.

“Sina uhakika kama Watanzania walikimbilia kwenda kuona kuna nini kule Selander Bridge. Kama walifanya hivyo ni makosa,” anasema.

Kuhusu Hamza kwenda mbele ya Ubalozi wa Ufaransa, ofisa huyo amekuwa na mtazamo kama alivyosema mmoja wa wachunguzi wa tukio hilo. “Kuna mambo mawili; mosi, huenda wala hakuwa akikumbuka kama hapo kuna ubalozi -kwamba hakudhamiria chochote.

“Lakini suala la pili ni kwamba huenda alifanya kwa makusudi. Kwamba akiwa mbele ya ubalozi wa taifa kubwa ujumbe aliodhamiria utafika dunia nzima. Kama ni hivyo, alifanikiwa,” anasema.

Dhamira yake ni nini?

Video moja kwenye mitandao ya kijamii inasikika sauti ya mtu akitaja kwa sauti jina la Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na kufuatiwa na maneno mengine. Bado polisi hawajatoa taarifa rasmi kuhusu video hiyo.

Hamza alikuwa akiishi jirani na Kituo cha Zimamoto (Fire). Mkazi wa Mtaa wa Mfaume, Upanga, Yassin Jumbe, anapinga dhana ya ugaidi kwa Hamza.

“Hakuwa Muislamu mwenye msimamo mkali kama inavyodaiwa. Nadhani wakati umefika kwa polisi kutafakari na ikiwezekana kuangalia dosari iko wapi,” anasema Jumbe.

Anamtaja Hamza kuwa ni kijana maridadi, mpole na aliyependa kuzungumza na watu. Hakuonyesha dalili za ukatili au kuishi maisha tofauti na vijana wengine.

“Tunaoishi Upanga tunamjua vizuri Hamza. Imani yake ya dini haina shaka. Kijana wa kawaida kabisa. Anajichanganya na wenzake na shabiki wa muziki wa disko,” anasema.

Mkazi wa Mtaa wa Mazengo, Upanga, Arya Kassamal, anasema ana imani kuwa Tanzania hakuna Waislamu wenye mrengo wa siasa kali.

Anasema ni mtazamo hasi kuwa mtu mwenye ndevu na anayevaa suruali fupi ni mujahidina anayeweza kujitoa mhanga wakati wowote.

“Sikuwa na mazoea naye, lakini tumeonana mara nyingi na kupishana naye njiani. Kuna nyakati tumesalimiana pia ingawa hakuonekana kama mwenye malezi ya kuendekeza mapenzi na wasichana,” anasema Arya.

Arya anatoa mwito kwa polisi kufanya uchunguzi na kutoa taarifa za kweli kuhusu chanzo cha tukio lililofanywa na Hamza.

Kumekuwapo madai kwamba Hamza aliyekuwa akimiliki bastola alikwisha kuripotiwa polisi kuhusu mwenendo wake usiofaa. Polisi waliozungumza na JAMHURI wamekanusha kuwapo kwa taarifa za aina hiyo.

“Kwa kawaida tukiambiwa mwenendo wa mtu anayemiliki silaha si mzuri, mara moja huwa tunachukua silaha na kufanya upelelezi. Ikithibitika amepoteza sifa tunamnyang’anya kwa mujibu wa sheria,” anasema polisi wa Kituo cha Msimbazi.

Wakati Dar es Salaam ikizizima, mkoani Mbeya, hasa wilayani Chunya, operesheni maalumu inaendelea kukagua maeneo ya uchenjuaji dhahabu.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, ameliambia JAMHURI kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama imeshatoa maelekezo hayo Chunya.

“Tunafanya upekuzi maalumu na wa aina yake katika maeneo ya uchenjuaji dhahabu. Kuna maeneo ya uchenjuaji zaidi ya 40. Huko kuna watu wengi sana kutoka ndani na nje ya nchi.

“Lengo ni kuhakikisha matendo kama haya hayajirudii na Mbeya kunakuwa na amani. Ninawahakikishia wakazi wa Mbeya kuwa tupo makini na usalama wao na wa taifa zima,” anasema Homera.

Anasema ukaguzi na udhibiti wa silaha zilizopo mikononi mwa raia umeanza kwa mkoa mzima.

Katika hatua nyingine, Homera anasema ndugu na watu walio karibu na Hamza wanaendelea kuhojiwa na vyombo vya dola hufahamu ukweli wa mambo.

“Ni mahojiano muhimu ili kuondoa hofu iwapo kuna ‘washirika’ wa Hamza bado wapo,” anasema Homera.

Matukio mengine

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Tanzania imewahi kukumbwa na matukio ya kuuawa kwa askari polisi wakiwa kazini.

Juni 11, 2014

Watu wenye silaha za jadi walivamia Kituo cha Polisi cha Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani na kumuua kwa kumshambulia kwa mapanga askari Joseph Ngonyani kisha wakapora bunduki tatu aina ya SMG na risasi 50.

Mwaka 2015

Askari wanne wa Kituo cha Polisi Ikwiriri walivamiwa na kuuawa na watu ambao Jeshi la Polisi wakati huo lilisema ni majambazi. Askari hao ni Koplo Yahya Malima, Koplo Tito Mapunda, Koplo Gaston Lupanga na Koplo Khatib Ame Pandu.

Machi 30, 2015

Usiku wa saa moja usiku wa kuelekea Sikukuu ya Pasaka, askari wawili waliuawa kwenye kizuizi cha barabarani katika Kijiji cha Kipara, maeneo ya Vikindu, Pwani. Waliouawa ni Sajenti Michael Aaron Tuheri na Koplo Francis Mkinga.

Agosti 26, 2016

Askari wa kikosi cha kupambana na majambazi, SSP Thomas Njiku, aliuawa katika Kijiji cha Vikindu, Mkuranga mkoani Pwani akiwa katika operesheni ya kuwasaka watu waliodaiwa kufanya uhalifu maeneo ya Mbande, Temeke jijini Dar es Salaam.

Februari 22, 2017

Mpelelezi wa Wilaya ya Kibiti, SP Peter Kubezya, aliuawa kwa kupigwa risasi ya tumboni na watu wanaosadikiwa kuwa ni wahalifu baada ya kuvamia Kituo cha Kutoza Ushuru wa Mazao ya Kilimo na Misitu Kijiji cha Jaribu Mpakani.

Aprili 13, 2017

Askari polisi wanane waliuawa kwa kushambuliwa na watu wenye silaha katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani. Askari hao walikuwa wakitoka kubadilishana doria na walishambuliwa kwa kupigwa risasi wakiwa wanasafiri kwa gari katika barabara ya Dar es Salaam – Lindi kisha wakaporwa bunduki saba na watu waliodhaniwa wakati huo kuwa ni majambazi.

Oktoba 16, 2018

Mkuu wa Kituo cha Polisi Nguruka, Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Ramadhani Mdimi na askari wengine wawili waliuawa wakati wakiwaondoa wananchi wanaodaiwa kuvamia eno la ufugaji la Ranchi ya Taifa Narco na kufanya shughuli za kilimo kinyume cha sheria.