Na BashirYakub

Kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kwamba mtu asiyekuwa na cheti cha ndoa hawezi kufumania, si sahihi.  

Usahihi ni kwamba mtu yeyote mwenye ndoa halali anaweza kufumania! Na hiyo inayoitwa ndoa halali ipo kisheria kwani imetajwa katika Kifungu cha 9 cha Sheria ya Ndoa. Hii ni sheria ya Tanzania, wala hapo kitu kinachoitwa ‘cheti cha ndoa’ hakikutajwa.

Kisheria kuwa na uhusiano nje ya ndoa ni kosa kwa mujibu wa Kifungu cha 72 cha Sheria ya Ndoa. Kwa maana hiyo, kufumania ni haki aliyonayo mwanandoa yeyote ili kupata ushahidi wa kutendeka kwa kosa hilo.

Sasa hapa maana yake ni kwamba, yeyote mwenye ndoa; awe na cheti au hata bila cheti, anaweza kufumania. Suala la msingi ni kuwapo kwa ndoa halali tu.

Kwetu hapa Tanzania ndoa zenyewe tulizonazo (zinazoitwa halali) ni ndoa za kidini, ndoa za kimila (customary marriage), ndoa za serikali (civil marriage) na ndoa inayotokana na kuishi pamoja kwa zaidi ya miaka miwili (presumed marriage). Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 160 cha sheria husika.

Watu wote hawa waliomo katika ndoa hizi, kwa mujibu wa sheria za Tanzania, wana ndoa halali na wana haki ya kufumania.

Kama kweli uhalali wa ndoa ingekuwa ‘cheti’, basi tungeweza kusema kuwa asilimia 80 ya Watanzania hawana ndoa!

Cheti, kwa mujibu wa sheria, ni ithibati tu, lakini hakitengenezi wala kuharibu uwepo wa ndoa halali na haki zake.  Kwa hiyo tusipotoshane.

By Jamhuri