Hivi karibuni Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilipiga marufuku kuuzwa kwa vilainishi vya magari na mitambo kutokana na baadhi kutokidhi viwango.

 

Vilainishi vilivyopigwa marufuku ni Motor Oil (Super Plus Sae 40), Diesel Engine oil (Top Gatex super Plus SAE 40), Motor oil Gatex Super plus SAE 40) na Diesel oil (Laurence Lubricants).

Vingine ni Petro engine oil (Lubex SAE 40), Diesel Engine (Lubex SAE 40), Motor  Oil (Caltex Super Sae 40), Diesel Engine (Mohona Lubricants SAE 40), Motor oil (Duma Tech Sae 40),   Diesel  engine oil (Universal Lubricant HD 40), Diesel engine oil,  Auto Star Sae 40, Diesel engine oil na Super plus Sae.

Katika mahojiano na JAMHURI yaliyofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Joseph Masikitiko alisema kwamba vilainishi hivyo ni hatari kwa usalama wa magari, mitambo, mazingira na pia vinaweza kusababisha ajali.

“Ujumbe wangu kwa watumiaji wa vilainishi hivyo nawaarifu kuwa bidhaa hiyo si salama kwa injini za magari na mitambo yao havikidhi mahitaji ya nchini katika kupoza na kulainisha,” amesema Masikitiko.

Amesema kwamba pamoja na kupiga marufuku vilainishi hivyo bado wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiuza bidhaa hizo kwa watumiaji katika maduka na vituo vya mafuta mbalimbali nchini.

JAMHURI imeshuhudia baadhi ya wafanyabiashara wakiendelea kuuza vilainishi hivyo, katika vituo vya mafuta na maduka ya kuuza vipuri vya magari.

Wakizungumza na JAMHURI  kwa masharti ya kutotajwa majina wala vituo wanavyofanyia biashara, wafanyabishara hao wamesema kwamba hupata bidhaa hiyo kutoka katika Visiwa vya Zanzibar.

“Ni kweli tumesikia tangazo la TBS lakini tunachokiona hapa ya mawasiliano ya kiutendaji kati ya TBS na ZBS kwani ukienda Zanzibar hii bidhaa ni ruksa nasi tunapata huko na kuingiza nchini,” amesema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Amesema kwamba kutokana na wao kutokuwa na utaalamu wa kujua kipi ni hakina ubora na kipi kina ubora ndiyo sababu ya wao kuuza bidhaa hiyo.

Hata hivyo kwa upande, Kaimu Mkurugenzi huyo amekiri bidhaa hiyo kuingia nchini  kupitia Zanzibar na sasa wako katika mazungumzo kuhakikisha kwamba  zinadhibitiwa.

Amesema kwamba bila kufanya hivyo watu wananchi watapata hasara kubwa kutoka na vilainishi hivyo.

“Sisi ni kazi yetu ni mtambuka kama tusipokuwa makini na hili uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja utadondoka kutokana na matumizi kuongezeka.

“Mfano  kwa kawaida kwa gari ndogo unatakiwa kuweka kilainishi  kiasi cha lita tano hizi unatakiwa kutembela kilomita 3,000  lakini unakuta ukiweka kilainishi kisicho na ubora utatembea kilomita 500 sasa sasa ili kufikisha kilomita hizo 3,000 unatakiwa kununua mara sita huoni kwamba  hapo unatumia fedha pasipo stahili fedha hiyo ungefanya kazi nyingine ya maendeleo lakini unatumia kwa ajili ya kilainishi tu,”amesema Masikitiko.

Amesema mbali na  kupoteza fedha kwa ajili ya kununua kilainishi, pia  wapo wasio makini na kuangalia magari yao wao uharibu injini hivyo kujikuta  wakitumia fedha kwa ajili ya ununzi wa njini mpya.

Masikitiko amesema kwamba  yupo katika hatua ya kufanya masako mkali  ili kuhakikisha kuwa vilanishi hivyo na bidhaa nyingine kama nguo za ndani za mitumba zinapotea sokoni.

Amezitaja njia ambazo atazitumia kuhakikisha anapoteza bidhaa zote katika soko la Tanzania kuwa ni kushirikisha halmashauri za wilaya na pia kuzungumza na Shirika la Viwango la Zanzibar.

“Shirika la Viwango la Zanzibar bado ni changa huwezi kulinganisha na TBS ambalo lina muda mrefu katika kufanya kazi hii sasa tunafanya mazungumza nao ili tuweze kushirikiana na nao kuhakikisha bidhaa hizo haziingi kupitia Zanzibar kama walivyokueleza wafanyabiashara hao,” amesema.

Hata hivyo Masikitiko amewakumbusha wafanyabiashara na wananchi kuacha kuuza nguo na kuvaa nguo za ndani za mitumba kwa kuwa ziko chini ya kiwango.

Amesema kuendelea kufanya hivyo ni kukiuka sheria Namba 2 ya mwaka 2009 inayozuia matumizi ya nguo za ndani zilizokwishatumika.

Katika sheria hiyo inaainisha majukumu ya TBS ambayo ni kuweka, kurekebisha na kusimamia viwango vyote vya kitaifa sanjari na udhibiti wa ubora wa bidhaa za ndani na nje.

Pia kutoa ushauri viwandani juu ya uzalishaji wa bidhaa bora; kupima na kuhakiki vipimo vinavyotumika viwandani; kuelimisha umma juu ya masuala ya viwango na kutoa leseni za matumizi ya alama ya ubora kwa bidhaa za ndani na nje zilizokidhi viwango stahili.

Kwa ujumla, jukumu la jumla la Shirika ni kukuza matumizi ya viwango na kuinua ubora wa bidhaa na huduma nchini ili kupanua na kuimarisha soko la ndani na nje.

Amesema, yapo madhara makubwa yanayotokana na kuvaa nguo za ndani za mitumba kwa sababu ya yanavaliwa katika meneo nyeti.

Amesema, walio katika hatari zaidi ni wanawake ambao maumbile yao yapo wazi zaidi na ni rahisi kwa vijidudu kuingia kwa urahisi pindi wanapokaribia vitu hatarishi.

Ametoa mfano kuwa, nguo za ndani zilizovaliwa huenda zina vijidudu vya fangasi au chawa wa sehemu za siri, mwanamke anapovaa hupata maambukizi hayo.

“Endapo watavaa nguo hizo bila kuzifua kwa usahihi na kuzichemsha, kisha kuzipiga pasi, ni rahisi kupata maambukizi. Lakini pia, si vyema kimaadili kuvaa nguo zilizokwishavaliwa na watu wengine,” amesema Masikitiko.

By Jamhuri