Kijana na Ajira ni maneno mawili yenye maana tofauti katika istilahi ya lugha ya Kiswahili. Lakini ni maneno yenye uhusiano na ushirikiano mwema katika mazingira ya kufanya kazi ambayo huleta kipato kizuri na maendeleo mema kwa kijana. Kijana anapofanya kazi hupata heshima kwa jamii ya watu. 

Nazungumzia kijana – awe ni mtoto wa kiume au wa kike, ni mtu wa makamo mwenye nguvu na uwezo wa kufanya kazi na mtukutu wa kutafuta kipato kizuri na kujenga maisha yake bora. Binafsi najaa furaha ninapoona kijana anachapa kazi. Nashadidia kusema, kijana ni nguvukazi. 

Ninapoangalia ajira ambayo ni kazi itolewayo au ifanywayo kwa malipo – yaani ujira, katika serikali, kampuni, kundi la watu au mtu binafsi ina uhusiano mkubwa na wa karibu na kijana katika kazi. Nasema ujira humwezesha kijana kufikia maendeleo anayokusudia. 

Taifa la Tanzania linamtambua na linamthamini kijana kuwa ni nyenzo kuu mojawapo katika kufanya kazi na kulipatia taifa maendeleo.

Daima kijana anajulikana kwa watu kuwa ni mwenye mawazo mapya, yenye mabadiliko ya hali, maarifa, nguvu na ujasiri wa kauli na matendo. Kijana ni tiba mpya ya jambo. 

Hivi sasa serikali inapiga la mgambo kumtaka kila kijana ajiajiri au aajiriwe kufanya kazi katika fani aijuayo au aiwezayo, ambayo italeta manufaa kwake na kwa taifa. Ukweli suala hili kwa Watanzania lipewe mfuo mkubwa kutoa nuru kwa kila kijana kuchapa kazi. 

Mfuo wa kutoa nuru usitoke kwa wazazi na walezi tu, utoke pia kwa Umoja wa Vijana katika vyama vya siasa na vijana wenyewe huko majumbani, vijiweni na michezoni, kwa kuhamasishana kufanya kazi badala ya kuhamasishana kutoa kebehi, dharau na ufukufuku kwa watu na viongozi. 

Umoja wa Vijana katika vyama vya siasa upige mbiu kuhamasisha kila kijana afanye kazi, iwe ya kujiajiri au kuajiriwa.

Using’ang’anie tu kuhamasisha kujiunga na chama cha siasa, kuelewa itikadi ya chama na kutambua msimamo wa chama chao. 

Kijana mwenye uwezo wa hali na mali, atumie elimu na utaalamu wake kujiajiri au kuajiri kijana mwenzake. Ufundi, uchuuzi na ujasiriamali hauna budi kupewa msukumo na nafasi pana kwa kijana.

Awe kijana wa kiume au wa kike, awe chachu mwenyewe kufanya kazi yenye masilahi kwa taifa. 

Si busara wala uungwana kwa kijana kushinda kutwa nzima kijiweni, saluni au nyumbani kuangalia runinga, kusikiliza redio au kuburudika na muziki.

Mazungumzo makubwa ni kusifu mafanikio ya watu au kubeza juhudi za viongozi mbalimbali na vijana wenzao wanaofanya kazi. 

Kijana wa Tanzania una wajibu wa kufanya mabadiliko katika hali ya maisha kwa kuyakabili mazingira yako kwa kufanya kazi ya kukuwezesha kupata ujira halali.

Uzuri wa umbo lako, upevu wa mawazo yako na utu wako utakuwa na heshima na thamani kubwa kwa kufanya kazi. 

Kijana unapofanya kazi unatunza mambo muhimu kama vile nguvu na siha nzuri, heshima na utu wako, hadhi na upendo na unajenga mvuto na urembo kwa jamii. Kijana mwenye kazi ni almasi na kijana asiye na kazi ni kamasi. 

Kazi ni suluhisho la tatizo la kupambana na mazingira ya hali ngumu ya maisha. Mafanikio na maendeleo ya kijana yanapatikana kwa kufanya kazi. Kuna methali ya Kiswahili isemayo: “Kazi mbaya si mchezo mwema.”

Kijana tambua fika kwamba kazi mbaya ni ile uliyonayo mikononi. Kazi nzuri si yako, ni ya mwenzako. Si vema kujivunia kazi ya mwenzako, jivunie kazi yako hata kama ni kijungu jiko.

Zingatia sana msemo huu kwa sababu kazi ni kazi alimradi mkono unakwenda kinywani. Wito wangu, kijana fanya kazi.

Please follow and like us:
Pin Share