Mathalani, mume anatuhumiwa kwa kutenda kosa fulani. Upande wa upelelezi wakiwamo polisi na wengine wanaamini mke ni mtu pekee anayejua tukio, hivyo kuwa shahidi muhimu kwao.

Au mke anatuhumiwa kwa kutenda kosa na mume ndiye mtu pekee anayeweza kuwa shahidi.

Swali ni je, polisi au mamlaka nyingine inaweza kumshurutisha/kumlazimishi mke au mume huyu kuwa shahidi dhidi ya mwenza wake?

Tutaona hapa, lakini kwanza tujue nani ana sifa za kuwa shahidi.

1. Sifa za shahidi

Kifungu cha 127(1) cha Sheria ya Ushahidi kinataja sifa za kuwa shahidi. Shahidi ni mtu aliyeona, kusikia, kuhisi, kunusa nk.

Lakini akawa ni mtu ambaye kwa uwezo wake anaweza kuulizwa swali na akatoa jibu linaloendana na kile alichoulizwa, hata kama ni mdogo au mkubwa sana kwa umri, au ana ugonjwa wa mwili au akili.

Mtu akiwa wa namna au na sifa hiyo, basi anaweza kuwa shahidi.

2. Ulazima wa kuwa shahidi

Hakuna hiari katika kuwa shahidi, hasa katika kesi za jinai, kama mtu ni mmoja kati ya walioshuhudia tukio, ni wajibu kuisaidia mahakama kutoa haki.

Kukataa kutokea kutoa ushahidi pale unapotakiwa na mahakama ni kosa la kuingilia shughuli za mahakama ambalo unaweza kuadhibiwa.

3. Mke halazimiki kumtolea ushahidi mume wake

Kifungu cha 130(1) Sheria ya Ushahidi kinasema mke halazimiki (compelled) kumtolea mume wake ushahidi pale mume huyo anapokuwa ameshtakiwa na mtu mwingine mahakamani. Halikadhalika mume halazimiki kumtolea mke ushahidi.

Ushahidi unaosemwa hapa ni ule wa upande wa mashtaka  ambao ukitolewa utakuwa dhidi ya au utakuwa unamfunga mke au mume huyo.

Hata hivyo, ikiwa anatakiwa kuwa shahidi wa kumsaidia mume/mke wake asifungwe, hapo analazimika kuja kutoa ushahidi.

Na akitakiwa kuwa shahidi wa kumfunga/kumtia hatiani mke/mume hapo halazimiki kuja kutoa ushahidi. Hapo juu tumeona kuwa ukitakiwa na mahakama kuja kutoa ushahidi ni lazima kufanya hivyo la sivyo utakuwa umetenda kosa.

Lakini haitakuwa lazima kuja kutoa ushahidi  ikiwa mke au mume ameitwa  kutoa ushahidi wa kumfunga mwenza, yaani ushahidi unaousaidia upande wa mashtaka. Na hakutakuwa na kosa ikiwa atakataa.

Ila kama mke au mume atahitajika kuja kutoa ushahidi wa kumtetea mwenza asifungwe, yaani ushahidi upande wa utetezi, hiyo ni lazima kuja na asipokuja ni makosa.

Pamoja na hayo hapo juu, mume/mke wanalazimika kutoleana ushahidi wa kufungana ikiwa  makosa yaliyotendwa ni:

(a) Yale yaliyo kwenye Sheria ya Ndoa.

(b) Yale yaliyo sehemu ya 15 ya Kanuni za Adhabu, ambayo ni makosa dhidi ya maadili, mfano kubaka, kulawiti, kunajisi nk.

(c) Yale ambayo mke amemshtaki mume wake mwenyewe, au mume amemshtaki mke wake mwenyewe.

4. Kuambiwa kuhusu uhiari wa kuwa shahidi

Kifungu cha 130(3) kinasema kuwa ikiwa mke/mume atafikishwa mahakamani kutoa ushahidi unaomfunga mwenza, yaani kuusaidia upande wa mashtaka, basi mahakama inalazimika kumwambia shahidi huyo uhiari wa yeye kutoa ushahidi wake.

Na ushahidi wake hautakubaliwa/kupokelewa mpaka ameambiwa uhiari huo, ili akubali atoe ushahidi au akatae.

Please follow and like us:
Pin Share