Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Sadani

Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii imeiagiza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Saadani kuandaa mpango mahususi wa kuainisha maeneo yote ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji na kuiongezea hifadhi hiyo mapato.

Kauli hiyo imetolewa leo Machi 19, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii Timotheo Mnzava wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na hifadhi hiyo yenye sifa ya kipekee inayokutanisha fukwe na nyika.

Mnzava alisema, “Nawaagiza Menejimenti ya Hifadhi hii kufanya ukarabati wa miundombinu hasa ya barabara, ujenzi wa gati na uwanja wa ndege katika eneo la hifadhi ili wageni wanapofika wasikose huduma za msingi.”

Aidha, wajumbe wa Kamati hiyo waliitaka TANAPA kutangaza maeneo ya uwekezaji hususani fukwe pamoja na maeneo mengine ambayo hayajapata wawekezaji ili kupata wawekezaji ili watalii wakiwa wengi wasikose malazi.

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema, “Serikali imeona umuhimu wa kuwa na mpango wa maeneo ya uwekezaji hivyo, hifadhi zimeshaelekezwa kuandaa mpango mahususi wa muda mrefu wa maeneo ya uwekezaji kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza katika Hifadhi za Taifa.”

Vile vile, Mhe. Kairuki aliongeza kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii inaangalia namna ya kuweka fedha zaidi katika kuboresha Uwanja wa ndege, barabara za ndani ya hifadhi na kufuatilia ujenzi wa gati.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa Serikali inaandaa mkakati wa kuendeleza zao la utalii wa fukwe ambao utaainisha maeneo yote ya fukwe kwa ajili ya uwekezaji.

Hifadhi ya Taifa Saadani ni miongoni mwa Hifadhi za Taifa 21 zinazosimamiwa na TANAPA huku ikiwa na mazao mengi ya utalii ambayo ni utalii wa fukwe, safari za boti katika mito na bahari, Utalii wa kutembea kwa miguu, Utalii wa kutumia gari na Utalii wa usiku.

By Jamhuri