Katika miaka 61 ya Uhuru, kinachoitesa Tanzania ni kukosa dira.

Awali, falsafa ya TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ilikuwa kuondoa maovu yote yaliyotokana na ukoloni na kuwafanya wananchi kujenga uchumi usio tegemezi.

Katika utawala wa kikoloni, Mswahili alikuwa raia wa daraja la tatu na alitendwa vyovyote alivyotaka mtawala.

Katika utawala wake, Mwalimu Nyerere alilenga kukusanya rasilimali zote za taifa katika ‘bwawa’ ili zimnufaishe Mswahili mwenye nchi yake.

Lakini CCM chini ya Mzee Ali Hassan Mwinyi iliingia na greda na kubomoa kuta za bwawa na mali kuanza kusambaa hovyo, kila aliye mjanja na mwenye nguvu alikwapua kwa kiwango alichotaka.

Alipoingia madarakani Mzee Benjamin Mkapa, yeye alichukua greda na kuanza kuchimba mtaro ili rasilimali hizo zilizozagaa hovyo zifuate mfereji wa kuelekea kwenye ubepari.

Hapo aliendesha ubinafsishaji wa mashirikia ya umma na vitega uchumi vya taifa kwa kasi ya ajabu. Nchi ikajielekeza kwenye uchuuzaji wa bidhaa kutoka nje.

Ilipoingia serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilitaka kukusanya yote iende nayo kwa pamoja, jambo hilo likawa gumu na kupotelea msituni huku serikali ikibaki kupiga ‘mark time.’
Alipokuja Rais Dk. John Magufuli, aliandaa mfumo wake wa kiutawala ambao haukushabihiana na yeyote aliyetangulia.

Alikuwa na faslafa yake na matakwa yake kama ‘Dk. Magufuli’ na nchi iliyokuwa mikononi mwake.

Alichoona upuuzi alikitupilia mbali, ikiwamo mradi wa umeme wa gesi kutoka Mtwara, licha ya mabilioni ya fedha kuzikwa kwenye mradi huo.

Rais Magufuli alianzisha mradi mpya wenye lengo lilelile la serikali iliyopita la uzalishaji umeme kupitia gesi na kuamua kujielekeza kwenye uzalishaji umeme kupitia maji katika Bwawa la Julius Nyerere.

Alichokipenda alikifanya hata kama kiliyastarehesha macho yake yeye peke yake tu.
Mtazamo wa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan nao umebeba miradi iliyopuuzwa bila sababu katika utawala uliopita, ikiwamo ujenzi wa nyumba za makazi kupitia mashirika ya serikali, pia ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.

Kwa lugha rahisi, kila serikali iliyoingia madarakani ilikuwa na dira isiyoshabihiana na serikali yoyote iliyotangulia katika taifa moja – kuanzia serikali ya Mwalimu Nyerere na zilizofuata – na hapa ndipo taifa lilipoanza kupotea.

Turudi nyuma kidogo. Wakati Mao Tse Tung, mwasisi wa taifa la China alipofariki dunia Septemba 1976, Wachina walilia kwa kukufuru, wakidai kuwa ‘mungu’ wao amekufa.

Kiongozi aliyemrithi Mao, Hua Goufeng, wakati wa salamu zake za maombolezo aliwaambia viongozi wenzake kuwa machozi ya Wachina yatakuwa na maana iwapo mawazo ya Mao yatageuzwa ili kukidhi hali halisi ya maendeleo duniani.

Viongozi hao waliona nafasi ya ukomunisti inamezwa na ubepari uchwara ambao mataifa makubwa yanaufanya kinara wa kuendesha mfumo wa uchumi na siasa katika nchi mbalimbali duniani.

Viongozi wa China waliamua kuyatumia mawazo ya mwasisi wao ili kuingia kwenye sera za ‘ubepari uliopangika vema’. Leo hii Wachina wanatembea kifua mbele.

Jambo kubwa walilolifanya ni kwamba, viwanda, mashamba na migodi iliyokuwapo chini ya umma wakati wa utekelezaji wa siasa za ukomunisti, haikubinafsishwa kwa wageni.

Bali waliweka mikakati ya kuwaandaa kwanza mabepari wa Kichina na kuwauzia viwanda, mali na raslimali, na ndipo baadaye waliruhusu uwekezaji wa wageni kushindana na mabepari wazawa.

Hakuna asiyejua mataifa yote makongwe ya kibepari barani Ulaya leo yanaiogopa China na kwamba, kasi yao katika maendeleo kwa nyanja zote imekuwa kubwa mno.

Wakati viongozi wa China wakitumia vema mawazo ya muasisi wao, viongozi wa Tanzania wameshindwa kabisa kubadili fikra za ‘ujamaa wa Mwalimu Nyerere’ ili ziwanufaishe wazawa.

Matokeo yake wamebaki kuimba kwa maneno kuwa ni watetezi wa sera zinazowanufaisha wanyonge kama zilivyoasisiwa na Mwalimu. Kauli hizo zimezua mvutano wa pande mbili.

Wanasiasa kwa upande wao, wanamchukulia Mwalimu kama mtaji wao kisiasa, wakati kwa upande mwingine, wananchi wanadai viongozi wao wanatelekeza maono ya Mwalimu na kwenda kinyume naye.

Mjadala wa ufisadi kutokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka, huonyesha kwa kiwango gani tumetelekeza fikra za muasisi ambaye dira yake ingetoa mwelekeo kama ilivyo China ya leo.

Baada ya kuondoka Mwalimu na fikra zilibadilika, ngozi za wanasiasa uchwara zikaanza kudhihiri na hapo ndipo tukawa tunashuhudia tuhuma za ufisadi dhidi ya viongozi wetu.

Tuhuma hizo zikiwa zinaelekezwa katika umiliki wa mali na biashara uliofanywa kwa kificho na viongozi wenyewe, marafiki zao au hata familia zao, kwao haikuwa sifa kuandaa mabepari wazawa kwa ajili ya kuongoza uchumi wa taifa lao.

Tunakumbuka Kiwanda cha Makaa ya Mawe cha Kiwira mkoani Mbeya kilichokuwa mikononi mwa Rais Mkapa, kadhia hii ni miongoni mwa ithibati za kutumia cheo kufanya biashara na kujipatia mali kinyume cha maagizo pia maono ya Mwalimu.

Si dhambi kwa viongozi kutamani kufanya shughuli kubwa za kiuchumi kwa kumiliki njia kuu za uchumi, hasa baada ya ruksa ya Azimio la Zanzibar mwaka 1992.

Azimio hili liliruhusu viongozi kuanzia Rais hadi mwenyekiti wa kitongoji kufanya shughuli za kiuchumi kama kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara, umiliki wa migodi, viwanda, kumiliki hisa katika kampuni na uanachama wa asasi zisizo za kiserikali.

Hata katika enzi za Mwalimu, mazingira ya wakati wake aliendesha shughuli za kilimo akiwa Ikulu, hii ni shughuli ya uchumi pia, ila ina tofauti kubwa na ya Mwalimu na viongozi wa sasa ambao uchumi wao hutegemea rasilimali za wananchi.

Si kila rais atakayekuwa madarakani awe mkulima kama Mwalimu Nyerere, la hasha! Mazingira mapya yanaruhusu viongozi kufanya shughuli yoyote ya kiuchumi akiwa tayari.
Mzee Mkapa alichukua mgodi wa makaa ya mawe Kiwira, lakini muda mfupi alishindwa kuuendesha kwa kuwa hakujiandaa.

Kama hakuweza kujiandaa kumiliki mgodi na kuleta mapinduzi ya kiuchumi, angewezaje kuwa na mipango ya kuwaandaa wazalendo kumiliki njia kuu za uchumi kabla ya kufungulia wageni kuja kuleta ushindani?

Hata suala la ubia, nina imani laiti wazalendo wangeandaliwa kumiliki uchumi wao, wangekuwa tayari kutafuta watu wanaoweza kuwekeza nao kwa ubia.

Ubinafsishaji wetu ulikwenda kwa ujanja ujanja, hatukujipanga barabara, na zaidi madaraka tuliyaacha kwa rais akaunda Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC), lakini baadaye ilikuja kuvunjwa ili kusiwepo chombo cha kufuatiali endapo mnunuzi anafuata masharti.

Tunaona viwanda vilivvyouzwa, mashine zake zimeng’olewa na kuuzwa kama chuma chakavu. Katika miaka 61 ya Uhuru, viwanda hivi sasa ni maghala au maduka ya kuuza bidhaa zitokazo nje.

Migodi yetu japo kila siku inatoa vito mbalimbali lakini hakuna hata nchi moja inayoweza kujenga uchumi endelevu bila kuweka ‘mitego’ imara.

China ilijenga ujamaa kama sisi, kila siku viongozi wake walikuja na kuondoka. Hata Tanzania nayo viongozi wa serikali na CCM huenda mara kwa mara China kujifunza.

Hivi ni kweli hatuwezi kujifunza jinsi walivyoweza kugeuka kutoka kwenye ujamaa hadi mabepari wakubwa duniani? Nadhani kuna haja ya kumkumbuka Horrace Kolimba aliyesema mwaka 1997 kuwa CCM imepoteza dira.

Tunayo mengi ya kujifunza kutoka China ili kuweza kugeuka kutoka kwenye uchumi wa dola na kuingia kwenye uchumi wa upebari.

Tunaweza kujifunza marais wastaafu wa nchi hiyo wanafanya nini baada ya kustaafu. Viongozi wetu wasidumazwe na akili ya kutegemea China kuendelea kuwa rafiki mwema siku zote, tayari nao wanatamani rasilimali zetu.

Serikali ya Rais Samia inapaswa kwenda mbali zaidi kurudi kwenye mawazo na nadharia ya Mwalimu Nyerere, ni jambo gumu lakini kuwawezesha Watanzania wazawa kuwa sehemu ya wamiliki wa njia kuu za uchumi linawezekana.

Nchi haziongozwi na malaika bali zinaongozwa na binaadamu, kila mmoja ana udhaifu wake na uwezo wake.

Katika miaka ya utawala wa Mwalimu Nyerere, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Kikwete na Mzee Magufuli, yapo mema na mabaya. Tuchukue yenye maana.
Tunaweza kujenga uchumi imara wa kisasa na ukawa na manufaa kwa wananchi nje ya ujamaa wa Azimio la Arusha, zipo namna nyingi za kufanya.