Na Stella Aron,JamhuriMedia

TASNIA ya habari inapaswa kuwa na sheria na kanuni rafiki ili kuruhusu kukua na kwamba, kuweka sheria kali na ngumu, kunaua vyombo vya habari lakini kunaacha athari hasi kwa taifa.

Kuwepo kwa vyombo vingi vya habari kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo wa kuwapasha habari wananchi inatokana na mazingira kandamizi ya kisheria na kikanuni yaliyopo nchini.

Ni muhimu Serikali ikazifanyia mapitio sheria na kanuni zote zinazoongoza vyombo vya habari Tanzania kwa lengo za kuziboresha na hivyo kujenga mazingira rafiki kwa vyombo hivyo kuweza kufanya kazi zao.

MJUMBE WA TEF

Akizungumza katika mahojiano maalumu Mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Joseph Mwendapole,anasema kuwa
sheria za habari zinapaswa kuwa rafiki kwa mazingira ya ndani na nje ya nchi kuliko kuwa na sheria mbazo ni kali na utekelezaji wake unakuwa ni mgumu.

“Hatupaswi kujifungia,tunapaswa kuwa na sheria zinazokubalika ndani na nje ya nchi.Tunawezaje kutengeneza sheria za vyombo vya habari ambazo baadaye mwenyewe uliyeshiriki kutengeneza unaanza kuomba toba.

“Tofauti na nyuma kidogo, kwa sasa vyombo vya habari vinaandika kwa uhuru, vinakosoa lakini kilichopo, kama mwandishi ama chombo cha habari kinawindwa, sheria hizi hizi zinatumika kuumiza chombo ama mwandishi.

Mwendapole anaongeza kuwa mwandishi anaweza kufungwa kwa sheria zile zile ama chombo cha habari kinaweza kuondolewa sokoni kwa sheria hizo hizo, ndio maana wadau wa habari wanasema uhuru wa habari ni lazima ulindwe kisheria.

Anaeleza kuwa,mchakato wa mabadiliko ya sheria za vyombo vya habari nchini, unalenga kujenga mazingira rafiki na bora kwa wanahabari katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Vyombo vya habari vinahitaji sheria rafiki zinazolenga kuimarisha mazingira ya utendaji, kutunga sheria ngumu na kandamizi,huchangia kuua ustawi wa vyombo vya habari,” anasema.

UMOJA WA HAKI YA KUPATA HABARI

Umoja wa Haki ya Kupata Habari (CoRI),ni kati ya wadau ambao wamekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuomba mabadiliko ya sheria ya habari ili kurahisisha utendajikazi wa wadau wa habari na kufanyakazi kwa uhuru.

Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa serikali ni pamoja na mamlaka haya ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.

Pia wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.

Aidha wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.

Mwenyekiti wa Umoja CoRI, Kajubi Mukajanga anasema kuwa mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu chake cha 7 (2) (b) (lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyoelekezwa na serikali, kwa kuwa kipengele hiki kinaingilia uhuru wa uhariri.

Baadhi ya wajumbe wa CoRi wapitia sheria mbalimbali za habari.

Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.

WADAU WAAANZA KUONA MAFANIKIO

MWENYEKITI wa Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA TAN), Wakili James Marenga amesema kuwa ni wakati mzuri ni sasa wa kufanya mabadiliko ya sheria za habari kwa kuwa,Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeonesha dhamira hiyo.

Marenga akizungumza katika Kituo cha Redio Tumaini jijini Dar es Salaam, kuhusu mwanya uliopo kwenye sheria za habari na hatari yake, anasema kuwa;

“Mchakato wa marekebisho ya sheria iliyotungwa mwaka 2016, ulichukua miaka 10. Mchakato huo ulianza mwaka 2006, ni bahati utawala uliopo umeona kuna haja ya kupitia upya sheria hizi kama ambavyo wadau wamekuwa wakipiga kelele.

“Tunaamini sheria hizi na zingine ambazo tumeorodhesha kwenye nakala yetu ya mapendekezo ya mabadiliko, wadau na serikali kwa pamoja tutapitia na kuona namna ya kunyoosha, ili mapendekezo hayo yatapopelekwa bungeni, tuwe na msimamo unaofanana,” anasema Marenga.

Marenga anasema kuwa wanaoina nia njema inayonyeshwa na Serikali katika kuelekea mabadiliko ya Sheria ya vyombo vya habari nchini kwa kuwa Serikali tayari imeonyesha nia kubwa ya kutatua changamoto hizo.

Anasema hadi sasa Serikali imepokea na kukubali kufanyia kazi vipengele mbalimbali ambavyo vimewasilisha kuhusu Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016.

“Tayari tumewasilisha serikalini vifungu vyenye utata kwenye sheria hii ambavyo vimekuwa ni changamoto, tunashukuru kwamba tunaiona nia njema ya serikali katika kufanyia kazi mabadiliko ya vifungu ambavyo tumeviwasilisha kwani imepokea vizuri maoni hayo ya wadau na imeahidi kuyafanyia kazi,” anasema Wakili Marenga.

Marenga amesema kuwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 imemtambua Mwandishi wa Habari ni nani kwani awali ya hapo alikuwa hatambuliki.

“Kabla ya kuwapo kwa sheria hiyo kulikuwa na sheria ya mwaka 2006 ambayo ilikuwa na changamoto kubwa sana ya udhibiti na uchapishaji.“Sheria hiyo ilikuwa ikimpa mamlaka makubwa sana Waziri wa Habari kudhibiti uchapishaji wa magazeti,” anasema Marenga.

Akifafanua zaidi juu ya changamoto ilipo katika sheria hiyo Wakili Marenga anasema kuwa kumekuwa na maeneo ambayo wanahabari wanaona kuna haja ya kufanyiwa kazi kama Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO),kupewa mamlaka ya kudhibiti matangazo ya Serikali.

“Awali kanuni zilikuwa zinamruhusu Mkurugenzi huyu kuangalia ni wapi atapeleka matangazo hayo baada ya kuwa ameyapokea jambo ambalo linaleta upendeleo na wasiwasi wa kupata matangazo hayo kwa vyuombo binafsi hasa ambavyo vyenye mrengo tofauti.

“Eneo jingine ni utoaji wa taarifa ambapo sheria ilikuwa inasema kwamba vyombo vya habari vitatoa taarifa kwa kuzingatia maslahi ya taifa, hivyo tunataka kama mwandishi amepata taarifa na akafanya ulinganifu wake vizuri basi tuache taarifa iandikwe,” anasema Wakili Marenga.

KAULI YA SERIKALI

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameeleza sababu ya Serikali kutopeleka bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari katika Bunge la Novemba mwaka huu, kuwa ni kutokamilika kwa baadhi ya taratibu.

Akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma anasema Serikali ilitarajia kupeleka mapendekeo hayo lakini haikufanya hivyo kwa kuepuka mvutano kutoka kwa wadau wa habari.

Kwenye kikao hicho na CoRI, Waziri Nape anasema serikali ipo tayari kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari kwa watunga sheria, baada ya kikao cha wadau wa habari na serikali kitakachofanyika Novemba 22, 2022, jijini Dar es Salaam.

‘‘Serikali tupo tayari kupeleka mabadiliko ya sheri ya habari bungeni baada ya kikao cha mwisho. Baada ya kikao hicho tutakubaliana tuliyokubaliana na ndio yataenda,’’ anasema Nape.

Amesema haikuwa vema kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari bungeni wakati kuna maeneo wadau wa habari na serikali walikuwa hawajakubaliana.

‘‘Sisi kama serikali hatujakaa kimya, bado tupo vizuri kwenye mchakato huu. Nia ya serikali mpaka sasa bado ni njema.Isingefaa kwenda na mabadishano bungeni. Mpaka sasa kuna maeneo ambayo bado hatujakubaliana na kikao hicho cha mwisho ndio kitatoa mwelekeo wa mapendekezo yote,” anasema.

‘‘Sisi kama tupo happy (tunafuraha) na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unavyokwenda, lakini pamoja na yote haya, ni vizuri uhuru uliopo tukautumia vizuri,’’ amesema.

Na kwamba, pamoja na mchakato wa mabadiliko ya sheria kuwa njiani kukamilika, serikali inaangalia pia uhalisia wa mabadiliko hayo ya sheria na mazingira ya sasa.‘‘Hata kama kuna mapitio tunayofanya, lakini lazima tuangalie uhalisia wa nchini,’’ amesema Nape.

Akizungumzia takwa la Rais Samia Suluhu Hassan la kukutana na wanahabari alilolitoa wakati wa Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD), jijini Arusha Nape amesema, wizara ipo mbioni kuandaa mazingira ya Rais Samia kukutana na wanahabari hao.

TAMWA YAWATAKA WADAU KUTOA MAONI

Dk. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), anasema, wadau wa habari wanapaswa kutoa mawazo yao ili ifike mahali wakubaliane katika utungaji wa sheria.

‘‘Tunapaswa kutoa mawazo yetu lakini ili tufike mahali ambapo tunaweza kukubaliani ili kuufanya huu mchakato wa mabadiliko ya sheria uende haraka. Sheria itakapoanza kufanya kazi, tutaanza kuona mabadiliko katika uandishi wa habari ambao ni wakitaaluma,’’ anasema.

MCHAKATO WAANZA KUZAA MATUNDA

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile anasema kuwa yapo matumaini makubwa ya mchakato huo kwa kuwa Serikali imechukua sehemu kubwa ya mapendelezo ya wadau kuhusu mabadiliko ya sheria ya habari.

Balile anasema, wadau wa habari nchini wanasubiri matokeo ya vikao vya serikali na wanahabari kuhusu mabadiliko sheria ya habari nchini.

“Kwa hakika sisi kama wadau wa habari tumefika hatua nzuri na hata kuwa na matumaini chanya hasa baada ya kikao cha mwisho kati ya wanahabari na Serikali.

“Wakati unaofuata ni wa serikali na hatua zake katika kuelekea mabadiliko sheria ya habari, lakini mpaka hapa tulipofika, tunaamini kuna jambo linakwenda kutokea,’’ alisema.

Balile anasema, jambo linalofurahisha zaidi ni ushirikishwaji wa taasisi zote za habari nchini katika mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari.

“Kwa kuwa wadau wa habari tunapigania kitu kimoja, tuliamua kwa pamoja kujiweka chini ya mwavuli tunaouita CoRI (Wadau wa Kupata Habari).

“Jambo hili limerahisisha kuwa na sauti moja lakini pia limerahisisha Serikali kujua wanazungumza na watu gani. Tusingekuwa pamoja pengine mambo yasingekwenda kwa namna tulivyoona,” anasema Balile.

WAZIRI NAPE AWAPA TAARIFA WADAU

Hivi karibuni, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape aliwahakikishia wadau wa habari kwamba, Serikali itakamilisha mchakato wa mabadiliko ya vipengele vya sheria ya habari.

Alitoa kauli hiyo kwenye kikao chake na wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Nape anasema, Serikali imepokea maoni yao kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016.

“Niwahakikishie kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayo nia ya dhati katika jambo hili. Nimekuja mwenyewe kuwasilikiliza na imani yangu ni kuona sekta inaendelea kukua” anasema.

WABUNGE WABAINISHA

Wabunge wa Bunge la Tanzania wamebainisha kwamba sheria na kanuni kandamizi zinazozuia vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa uhuru zinapaswa kurekebishwa ili waandishi waweze kutimiza wajibu wao kama mhimili wa nne wa dola.

Watunga sheria hao walitoa wito huo wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tan) yaliyofanyika Februari mwaka huu, yaliyolenga kuwafahamisha wawakilishi hao wa wananchi vifungu vya sheria na kanuni vinavyominya uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Baadhi ya wabunge wakipitia baadhi ya vifungu vya sheria ya habari

Kauli za wawakilishi hao zilikuja siku chache tu baada ya Serikali kuyafungulia magazeti manne ya MwanaHalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima huku Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akibainisha nia na utayari wa Serikali wa kuyafanyia kazi maoni na mapendekezo ya wadau yanayolenga kuboresha sheria na kanuni zinazoongoza uandishi wa habari Tanzania.

Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Abdallah Shangazi anasema kuwa marekebisho ya sheria na kanuni ni hoja za msingi ambazo zinapaswa kutazamwa kwa mawanda mapana.

Mbunge huyo anasema kuwa sheria na kanuni zinazolalamikiwa kuminya uhuru wa vyombo vya habari nchini ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambayo, pamoja na mambo mengine, inaruhusu Serikali kufungia magazeti.

Sheria hiyo pia inaweka sharti kwa gazeti kuwa na leseni ambayo inapaswa ihuishwe kila mwaka. Pia, inaweka sharti kwamba ili mtu afanye uandishi wa habari Tanzania ni lazima awe na elimu ya kiwango cha stashada au shahada ya uandishi wa habari au taaluma inazohusiana nazo.

Halima Mdee ni Mbunge wa Viti Maalum ambaye anaamini kwamba sheria na kanuni “zilizotungwa kwa makusudi, na siyo kwa bahati mbaya” zinapaswa kubatilishwa kwani “zimekuwa zikiipa Serikali mamlaka ambayo imekuwa ikiitumia vibaya.”

Mdee anaamini kwamba ni muhimu kwa wadau kutumia mwanya huu ambapo Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha nia ya kutaka kuweka mazingira safi kwa kazi za waandishi wa habari nchini kufanikisha mabadiliko ya sheria hizi.

Mnamo Aprili 6, 2021, ikiwa ni siku 18 tu baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kufunguliwa kwa vyombo vyote vya habari vilivyokuwa vimefungiwa, akisema: “Tusiwape mdomo mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa habari na nataka kanuni ziwe wazi, ili mtu akifungiwa ajue kosa na adhabu yake. Tusifungie tu kibabe.”

Mbunge wa Momba Condester Michael (CCM) alieleza kwamba wao kama watunga sheria na watu wanaoisimamia Serikali wanatambua mchangao wa vyombo vya habari, akisema wanaifanya jamii kujua kinacho endelea na hivyo wataunga mkono juhudi za kufanya maboresho ya sheria na kanuni zitakazowawezesha waandishi kufanya kazi kwa uhuru zaidi.

WAHARIRI WANENA

Salehe Mohamed ni mhariri wa habari gazeti la Mwananchi, anasema kuwa wangependa kuona Waziri Nape anatimiza ahadi yake ya kuwasilisha mapendekezo ya wadau kuhusu mabadiliko ya sheria za habari katika bunge lijalo.

“Wadau wangependa kuona ahadi ya Waziri Nape ya kupeleka Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari yanafanikiwa kwenye Bunge lijalo huu ili mchakato wa mabadiliko hayo ukamilike,” anasema Salehe.

Anasema kuwa mjadala wa Serikali na wadau wa habari unahusu Sheria ya Huduma za Habari 2016 na kwamba, kuna baadhi ya vipengele tayari Serikali imeonyesha mwelekeo wa kukubali.

“Tunaona kuwa Serikali imeonyesha nia ya kufanya mabadiliko hayo hivyo ni vyema sasa ikaendelea na jitihada hizo ili kuhakikisha kuwa mchakato huo unapata majawabu,” anasema.

Naye Joyce Shebe ambaye ni Mhariri wa Clouds FM Radio anasema kuwa Serikali imeonyesha usikivu na hata kutoa nafasi kwa changamoto zinazotukabili kufanyiwa marekebisho ni hatua nzuri kwa wadau wa habari nchini.

“Kwa kuwa imeonyesha nia ya kufanyiakazi vipengele mbalimbali hivyo mchakato huo utapata majibu yatakayomaliza kiu sekta ya habari,” anasema.

Anasema kuwa si kwamba sheria yote ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 havifai bali ni kuwepo kwa baadhi ya vifungu vinavyotishia waandishi na uhai wa tasnia ya habari nchini.

Joe Nakajumo anasema kuwa michakato mbalimbali ya mabadiliko ya sheria ya habari inayoendelea kwa awamu hii kumeonyesha dhamira njema ya wanahabari hivyo ipo haja ya kumaliza kiu cha muda mrefu kwa wana habari.

Anasema kuwa Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 iliacha mambo ya msingi katika kukuza tansia ya habari na badala yake ikawa ni sheria ambazo ni ngumu kutekelezeka.

Mhariri wa Gazeti la Mwanahalisi, Jabir Idrisa anasema kuwa kutokana na uwepo kwa mazingira magumu ya habari na wanahabari nchini, tansinia ya habari iliyumba kwa kiwango kikubwa.

Anasema kuwa uhuru wa habari ni moyo wa kidemokrasia ya nchi yoyote kwa kuwa hutoa mwanga maendeleo.

Jabir anasema kuwa jamii inapaswa kuendelea kupiga kelele kwa kushirikiana na vyombo vya habari juu ya marekebisho ya sheria zinazokwaza uhuru wa habari.

Please follow and like us:
Pin Share