Na Stella Aron,JamhuriMedia

Serikali ipo tayari kupeleka mabadiliko ya sheri ya habari bungeni baada ya kikao cha mwisho kukubaliana baadhi ya mapendekezo hayo.

Hiyo ni kauli ya Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wakati akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Waziri Nape anasema kuwa serikali ilitarajia kupeleka mapendekeo hayo lakini haikufanya hivyo kwa kuepuka mivutano kutoka kwa wadau wa habari kwa kuwa kulikubwa hakuna makubaliano kwa baadhi ya vipengele.

“Serikali ina nia ya njema kwani haikupelaka mapendekezo ya sheria ya habari bungeni kwa kuwa kulikuwa kuna maeneo ambayo wadau wa habari na serikali hawakukubaliana.

“Sisi kama Serikali hatujakaa kimya, bado tupo vizuri kwenye mchakato huu. Nia ya serikali mpaka sasa bado ni njema. Lakini Serikali ilishindwa kupeleka mapendekezo katika Bunge la Novemba kwa kuwa kulikuwa bado taratibu zingine hazikukamilika ” anasema.

Anasema kuwa katika kikao cha mwisho ndicho kitakachotoa mwelekeo wa kupelekea mapendekezo hayo bungeni hivyo Serikali haipo kimya bali ipo katika mchakato wa kufanikisha mabadiliko hayo.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa

Waziri Nape anasema Serikali ipo tayari kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari kwa watunga sheria, baada ya kikao cha wadau wa habari na serikali.

“Uhuru uliopo sasa unapaswa kutumika vizuri.Sisi kama tupo happy (tuna furaha) na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unavyokwenda, lakini pamoja na yote haya, ni vizuri uhuru uliopo tukautumia vizuri,’’ anasema.

Na kwamba, pamoja na mchakato wa mabadiliko ya sheria kuwa njiani kukamilika, serikali inaangalia pia uhalisia wa mabadiliko hayo ya sheria na mazingira ya sasa.

Akizungumzia takwa la Rais Samia Suluhu Hassan la kukutana na wanahabari alilolitoa wakati wa Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD), jijini Arusha Nape anasema, wizara ipo mbioni kuandaa mazingira ya Rais Samia kukutana na wanahabari hao.

“Katika Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Rais aliagiza wizara kutaka kukutana na wanahabari. Tunafanyia kazi hilo,’’ amesema Nape.

BAADHI YA VIPENGELE VINAVYOBINYA UHURU WA HABARI

Wadau wa habari wanapiga kelele kuhusiana na kuwepo kwa baadhi ya vipengele ambavyo vimeonekana kubinya uhuru wa habari na kukwamisha haki za upatikanaji habari ni Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016,Sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 ambayo nasimamia radio, TV na mitandao ya kijamii.

Pia Sheria ya Haki ya Kupata Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya
Mtandao ya 2015 zikiwemo kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2018 ziliyogawanywa katika vipengele mbalimbali, ni miongoni mwa maeneo ya vipaumbele ambavyo wadau wa habari wanataka maboresho ili kuongeza ufanisi katika tasnia hiyo kutokana na kuwa na dhaifu na upungufu wa Sheria.

Sheria hii ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Septemba 7, 2016 na kuidhinishwa na hayati Rais John Magufuli, Septemba 23, 2016. Kwa mujibu wa kifungu cha 2(1), Sheria hii inatumika Tanzania Bara pekee.

Kwa kifupi,hii ni Sheria inayohusu haki ya kupata taarifa, kupanua wigo
wa taarifa ambayo jamii inaweza kuipata ili kukuza uwazi na uwajibikaji wa wenye taarifa pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Kuna baadhi ya vifungu vinaingilia haki ya kupata taarifa kama ilivyoelezwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mikataba ya Haki za
Binadamu iliyoridhiwa au kusainiwa na Tanzania.

MAKUNGA AFAFANUA

Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Theophil Makunga anasema kuwa ni vyema vifungu hivyo ambavyo vinawanyima usingizi wadau wa habari vikafanyiwa marekebisho ili kuhakikisha haki ya kupata taarifa inapatikana bila vikwazo vyovyote.

“Pamoja na hayo naona kuna mwanga, kwenye jambo hili,tayari Serikali imekwishaonesha nia ya kuzungumza na vyombo vya habari ili kuviondoa au kuvirekebisha vipengele na vifungu ambavyo vinabana vyombo vya habari.

“Wanaweza (Serikali) kukubaliana na sisi ili tubadilishe au tuondoe vile vifungu ambavyo tunafikiria vinatubana,vilevile kuvirekebisha ili kazi ya uandishi wa habari iwe rahisi,” anasema.

Makunga anasema kuwa,licha ya changamoto za hapa na pale pia sheria imekasimisha mamlaka makubwa kwa mtu mmoja.

“Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 imempa mamlaka makubwa sana kufanyakazi dhidi ya vyombo vya habari na ukiangalia hiyo sheria kifungu cha 50, kifungu kidogo cha (i) inampa mamlaka yeye kufungia, kufanya usajili wa magazeti.

“Kwa sababu ile sheria nyingine kuhusu radio, televisheni imeenda TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania). Lakini kwenye magazeti Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO amepewa hayo mamlaka, sisi tunasema amepewa mamlaka
mengi sana kwa mfano kuhusu usajili kila mwaka unatakiwa ulipie usajili.

“Sasa kulipia kuna leseni nyingine mfano leseni ya biashara ukiipata sasa kwenye chombo cha habari ukitaka kuanzisha gazeti lako lazima usajiliwe, sasa tunaona likishasajiliwa liachiwe ili mradi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria.

“Lakini sasa Mkurugenzi amepewa yale mamlaka ya kusajili, kufungia vyombo vya habari kwa wakati wote yeye anapofikiria vinakwenda kinyume, hapo tunaona ni kuminya uhuru wa vyombo vya habari, waandishi wa habari watakuwa wameminywa kufanya kazi kwa uhuru, sababu ile sheria inawanyima haki kufanya kazi kwa uhuru wao.

“Tukasema apunguziwe mamlaka ambayo anapewa na hiyo sheria ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 2016 mambo mengi sana yapelekwe kwenye mahakama kama kuna haja ya kufanya hivyo,”anafafanua Makunga.

UENDESHAJI VYOMBO VYA HABARI TANZANIA

Kuhusu jinsi ambavyo vyombo vya habari vya Tanzania vinavyojiendesha, Makunga anafafanua kuwa, “Ukiangalia uendeshwaji wa vyombo vya habari vya Tanzania asilimia zaidi ya 50 ya matangazo yanayotolewa kwenye vyombo vya habari yanatoka serikalini, kwa hiyo uendeshwaji wa vyombo hivi vya habari unategemea sana matangazo toka serikalini.

“Sasa unapompa mamlaka Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo achague vyombo gani Serikali huko ndiko kunakochangia kubinya vyombo vingine ‘kusavivors’ na kujiendesha.

“Idara za Serikali ziwe huru kutangaza kwenye vyombo vya habari bila kupitia mtu mmoja. Halafu inapita kwa mtu mmoja kwa mfano kama kuna gazeti ambalo ni ‘critical’ kwa serikali halafu haipewi matangazo na kama halipewi matangazo
uendeshwaji wa kile chombo utakuwa mgumu sana ni kama vile kuliua kwa kutolipa matangazo.

“Kifungu cha 50 hata huko nyuma kwenye Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kosa la defamation unapelekwa mahakamani ulipe fidia. Sasa kulifanya jinai ni kama kitisho kwa waandishi wa habari kutokuwapa nafasi kufanya kazi yao vizuri kwa sababu wao wana misingi yao ya kufanya kazi ambayo wanafundishwa kwenye vyuo.

“Kwa nini Serikali iwe na mashaka kuhusu utendaji kazi mpaka uitungie sheria kosa linalofanywa na chombo cha habari liwe jinai? Sababu wenyewe kupitia taaluma yao wana namna ya kufanya kazi,hiki kiwe hivi na hiki kisiwe hivi, kwa hiyo mashaka ya serikali mimi siyaoni kwamba wanahamisha defamation kuwa jinai.

“Kama wadau wa Vyombo vya habari hiyo sheria ifutwe kabisa badala yake irudi nyuma kama ni defamation iwe hivyo,”anasema Makunga.

MKURUGENZI TAMWA

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dkt. Rose Reuben,anasema, wadau wa habari wanapaswa kutoa mawazo yao ili ifike mahali wakubaliane katika utungaji wa sheria.

“Tutoe mawazo yetu ili tufike mahali ambapo tunaweza kukubaliana ili kuufanya huu mchakato wa mabadiliko ya sheria uende haraka.

“Sheria itakapoanza kufanya kazi, tutaanza kuona mabadiliko katika uandishi wa habari ambao ni wakitaaluma,’’ anasema.

MAKAMU MWENYEKITI MISA-TAN

James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), anasema kuna maeneo kadhaa yanapaswa kufanyiwa kazi ili wanahabari wafanye kazi zao kwa uhuru.

Anasema kuwa anaamini kuwa katika mabadiliko wanayoyataka wadau wa habari yatakayopelekwa bungeni yatakidhi matakwa ya wanahabari kwa ajili ya kunufaishi wananchi,Serikali na tasnia kwa ujumla.

Anasema kuwa sheria ya huduma ya vyombo vya habari ya sasa pamoja na kwamba kuna maeneo muhimu na mazuri lakini kuna vifungu vyenye changamoto kubwa na zenye ukakasi katika utekelezaji wa majukumu ya mwanahabari.

“Vifungu vyenye utata vipo vingi,ni pamoja na kile kuweka adhabu kwa makosa ambayo hayako wazi kinyume na Ibara 13 (6) (c), kufifisha uhuru wa kupokea na kusambaza habari kinyume na Ibara 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” anasema.

Marenga anasema kuwa maeneo mengine yenye ukakasi katika sheria hiyo ni kuathiri uhuru wa faragha kinyume na Ibara 16(1) ya Katiba ya Tanzania.

“Kifungu 3.5 kinaathiru haki ya kusikiliza kinyume na Ibara 13 (6) (a) ya Katiba ya Tanzania.Mfano mwingine kuna kifungu cha 38 (2) (b) cha sheria usikilizwaji wa shauri la mtu bila mtuhumiwa kuwepo.Hivi vifungu na vingine mfano wa hivi vinatakiwa kufanyiwa marekebishi,” amesema.

MWENYEKIKTI TEF

Deodatus Balile,Mwenyekiti wa TEF anasema kuwa majibu ya Serikali yanayotolewa hivi sasa yanaleta matumaini hivyo wadau wa habari wanaamini kuwa katika Bunge lijalo mchakato huo unaweza ukatua bungeni.

“Rais Samia ana dhamira njema na tasnia ya habari, lakini changamoto mara nyingi huwa ni kwa baadhi ya watendaji ambao utekelezaji wa majukumu yao, huwa hauendani na kasi ya mkuu wa nchi.

“Tunathamini na kuheshimu sana maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhusu maboresho sekta ya habari, lakini tunashauri maagizo hayo yaendane na uundwaji wa sheria na kanuni kwa
haraka ili vyombo vya habari nchini viendelee kuheshimiwa,”amesema.

Anasema kuwa sasa mwamko wa uhamasishaji wa mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari umeongezeka na umetoa matokeo mazuri na anaendelea kuishukuru Serikali kwa kuonesha utayari.

“Lazima tuwe na moyo wa shukurani kwa Serikali, tumeona magazeti ya Mawio, Tanzania Daima na Mseto yakifunguliwa na kuna juhudi mbalimbali zinaendelea ili kuhakikisha sheria ambazo zinaonekana kubinya uhuru wa vyombo vya habari
zinafanyiwa maboresho,”anasema.

By Jamhuri