Hivi kati ya Spika Sitta na Kubenea nani ‘Court Jester’?

Akiwa ameketi kwenye kiti chake cha enzi Jumanne iliyopita, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), Samuel John Sitta, alimshambulia Mkurugenzi Mtendaji wa HaliHalisi Publishers, Saed Kubenea, kwa kitendo chake cha kufungua shauri mahakamani kupinga Bunge hilo.

Sitta alikwenda mbali na kumfananisha Kubenea na mchekeshaji wa mfalme huku akimtuhumu kuwa wapo wafadhili nyuma yake katika hatua yake hiyo.

Sitta, msomi wa sheria, alirejea hadithi za karne ya 15, 16 na 17 akisema kwamba enzi hizo kulikuwa na wafalme barani Ulaya waliowateua baadhi ya watu kufanya kazi ya kuwachekesha. Watu hao walifahamika kwa jina la court jesters.

“Eneo la mfalme lilikuwa kama mahakama halafu kuna mchekeshaji,” alisema na kuongeza: “Sasa wafalme wa Ulaya walikuwa wanaajiri wachekeshaji kwa malengo mawili. Moja ni kumsifia mfalme kwa kila kitu na jingine ni kuwasema wote wale ambao mfalme anahisi ni wabaya wake.

“Kwa hiyo kuna watu wa aina hiyo, tunawaona hadi sasa kama kina Kubenea, ni mchekeshaji wa mfalme tu. Yeye kuna mfadhili na wafadhili wako nyuma yake.”

Amesema wafadhili hao wanamsogeza kwa sababu wamemwona ana vipaji vya kufanya kazi kama hizo. Tuwaone nao kuwa kuna njia nyingi za kupata riziki tuwasamehe tu waendelee na shughuli zao.”

Akasema jukumu jingine la watu wale lilikuwa ni upambe na kutumika na watawala wale kupata umbeya kutoka mitaani. Basi, katika hoja hiyo akamfananisha Kubenea na wachekeshaji wa zamani.

Hoja ya mfano aliyoitoa Sitta ni kwamba Kubenea anatumika. Anafanya hivyo kwa sababu ya kutafuta riziki, lakini kwa bahati Kubenea alijibu haraka, akisema: “Situmiki.”

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Kubenea alisikika akisema: “Nimemsikia Sitta, lakini sijafahamu kama alikuwa anazungumzia kesi niliyofungua mahakamani au kazi zangu za uandishi wa habari, lakini madai kwamba natumika, yeye (Sitta) anajua kwamba sijawahi na sitawahi kutumika. Ninafanya kazi zangu kwa uadilifu na uaminifu mkubwa kwa maslahi ya umma.”

Amesema hata pale gazeti lake lilipokuwa linamwandika Sitta vizuri si kwa sababu alikuwa amewalipa, bali wakati huo alikuwa anasimamia haki na hata sasa anapomwandika upande wake wa pili, ndiyo ukweli wa jinsi alivyo.

Kubenea amesema Sitta anapingwa wakati huu kutokana na kitendo chake cha “kutumia Bunge la Katiba kunyofoa maoni ya wananchi katika kazi takatifu iliyofanywa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.”

Suala la Sitta kumfananisha Kubenea na Court Jester haliwezi kupita bila kujadiliwa hasa kwa kile ambacho kila mmoja amekizungumza kwa siku hiyo.

Mjadala unaanzia hapa, kwamba Sitta hakutaja moja kwa moja watu wanaomtuma Kubenea, ilhali kwa upande wake Sitta anayetetea kuendelea kwa Bunge hilo, hawezi kukwepa lawama kwamba anafanya hivyo kwa sababu ya kutumwa na chama chake, ambako wajumbe wake wameegemea upande wa kupindua kabisa rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.

Sitta aliwezaje kumtaja mtu aliyemtuhumu kuwa anatumiwa na kushindwa kutaja aliyemtuma? Sitta ni kada wa CCM, kwanini tusiamini kama naye ametumwa na chama chake?

Kwanini tusiamini kwamba anataka kutumia nafasi hiyo ya uenyekiti wa Bunge Maalum kubeza wengine ili yeye apate nafasi ya juu zaidi ambayo bila shaka ameisaka kwa muda mrefu?

Nani asiyejua kuwa Sitta anataka kuwa rais wa nchi mwakani? Kwani hata pale aliposhutumiwa kuwa kwa jinsi anavyoendesha Bunge Maalum, amepungukiwa na sifa za kuwania urais mwaka 2015, alikuja juu huku akijipigia debe kiaina katika nafasi kuwania nafasi hiyo.

Kwani Kubenea akisema kwamba Sitta anataka hayo ili kumfurahisha Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ili ampiganie kuwa rais wa nchi atakuwa amekosea? Ndiyo maana najiuliza, hivi kati ya Kubenea na Sitta nani Court Jester?

Sitta anasema watu wanaojaribu kumpima kama anafaa kugombea urais 2015 kwa kuangalia yale yanayotokea katika Bunge Maalum la Katiba wanampima kwa hoja duni na kuongeza kuwa iwapo Watanzania watahitaji rais makini na mwadilifu mwaka 2015 basi wamfikirie pia yeye.

Anadai, “Wanaochagua rais ni wananchi. Inawezekana mwakani wananchi wa Tanzania wakatamani mtu mzima, aliyetulia, asiyewaogopa wapuuzi, wakatamani hilo. Kama watahitaji mtu makini, mwadilifu basi wajue tu kuna sisi wengine tunaweza kufikiriwa kwa mambo kama hayo.”

Kauli hiyo ya Sitta imekuja wakati makundi mbalimbali ya jamii wakiwamo wasomi, wanasiasa, viongozi wa dini na wanaharakati wakipaza sauti kutaka Bunge lisitishwe. Msingi wa kutaka kusitishwa kwa Bunge hilo ni kutaka kutafutwa kwanza kwa maridhiano kati ya CCM na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao wamesusia Bunge hilo.

Wajumbe wa UKAWA walisusia Bunge hilo tangu Aprili mwaka huu, wakipinga kitendo cha Bunge kuacha kujadili rasimu iliyobeba maoni ya wananchi na kuingiza mambo mapya waliyosema yana nia ya kubeba masilahi ya CCM.