NA ANGELA KIWIA

Serikali imetoa maagizo kwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na kuyataka kuyatekeleza ndani ya mwezi mmoja.
Napenda kuipongeza serikali kwa hatua hii muhimu. Natambua wapo baadhi ya ndugu zetu hawatafurahia hatua hii ya serikali kuzibana NGOs, kwa kuwa walikuwa wanufaika wakubwa wa mashirika hayo kwa kuyatumia isivyo.
Baadhi ya mashirika hayo yamekuwa yakijihusisha na uhamasishaji wa vitendo vilivyo kinyume cha tamaduni zetu, huku yakipokea fedha kwa ajili ya uhamasishaji wa mambo ya ovyo, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ushoga nchini.
Serikali sasa imeamka kutoka usingizini na ‘kuyashukia’ mashirika hayo yaliyokuwa yakisababisha mmomonyoko wa maadili uliokuwa ukihamasishwa na baadhi ya yale yanayopata ufadhili kutoka nje ya nchi.
Miongoni mwa maagizo hayo ya serikali ni kuyataka mashirika hayo kutuma taarifa zao za kifedha na miradi za kila mwaka kwenye Ofisi ya Msajili wa NGOs. Hii itasaidia kufahamu vema kazi za NGOs husika na malengo yake, kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Nchi yetu iligeuzwa kuwa shamba la bibi na jalala. Tumekubali kutumiwa kutokana na njaa zetu huku kizazi chetu kikiishia kupokea kila aina ya tamaduni kutoka nje.

Tunashuhudia mmomonyoko wa maadili kutokana na tamaa ya fedha kutoka kwa baadhi ya wafadhili kupitia baadhi ya NGOs. Ubinadamu umetutoka kwa tamaa ya kuishi maisha mazuri huku kizazi chetu kikiangamia.
Ikumbukwe nchi yetu ni miongoni mwa nchi zinazozingatia misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo uzingatiwaji wa masuala ya uwazi na uwajibikaji ni jambo la msingi kwa mashirika haya.
Baadhi ya NGOs zimekuwa zikilalamikiwa kwa kujihusisha na mambo yaliyo kinyume cha malengo ya uanzishwaji wake. Hata hivyo zipo ambazo zimekuwa kichocheo cha maendeleo katika nchi yetu.
Wapo baadhi ya wageni wamekuwa wakipitia kwenye NGOs na kusababisha kutoelewana katika jamii zetu, kwa kuwatumia baadhi ya Watanzania wenzetu kutokana na njaa yao isiyokwisha.

Naipongeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuliona hilo na kuamua kuchukua hatua. Ninaamini kuwa zoezi hili litakuwa endelevu na lenye tija kwa taifa.
Vilevile ni imani yangu kwamba huu utakuwa mwanzo mzuri kwa jamii yetu kuyatumia mashirika hayo kutimiza malengo husika na kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja bila kutumiwa na wasioitakia mema nchi yetu.
Huu utakuwa mwisho wa baadhi ya watu ambao waliamua kuyapaka matope mashirika hayo yasiyo ya kiserikali na kuonekana yote hayafai, jambo ambalo si kweli.

Natambua yapo yaliyokuwa yakiumizwa na hali hii kutokana na serikali kutochukua hatua. Sasa nchi yetu itakuwa na NGOs zinazotekeleza na kutimiza lengo la uanzishwaji wake, huku zikifurahia uwepo wake.
Vilevile ni wakati muafaka sasa kwa serikali kuwa karibu na mashirika haya ili kutambua uwepo wake na kuyaunga mkono, hasa pale yanapohitaji msaada wake katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Serikali na mashirika hayo wote kwa pamoja wanategemeana, hivyo ni wakati sasa wa kufanya kazi pamoja na kumsaidia Mtanzania mmoja mmoja anayehitaji kufikia lengo.
Tanzania inajengwa na Mtanzania mwenyewe.

Please follow and like us:
Pin Share