Yasimika mtambo wa kisasa unaopatikana nchi tatu tu Afrika

Tanzania sasa kupokea mamia ya wagonjwa kutoka nje

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

JITIHADA zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kuigeuza Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba zinaendelea kupata mafanikio makubwa baada ya ya Hospitali ya Kairuki ya Mikocheni jijini Dar es Salaam kuanza kutoa matibabu ya kuondoa vimbe mbalimbali bila upasuaji kwa  kutumia mtambo tiba unotumia mwangwi wa sauti (Ultrasound).

Rais Samia amekuwa akifanya jitihada kubwa kuzipa vifaa hospitali za Serikali na kuziwekea mazingira rafiki hospitali binafsi ili ziweze kununua vifaa tiba vya kisasa na kutoa tiba za kibingwa ambazo awali wagonjwa walilazimika kuzifuata Ulaya, Marekani na India.

Mtambo mpya na wa kisasa ambao umenunuliwa na Hospitali ya Kairuki  unaoitwa High Intensity Focused Ultrasound (HIFU), umeelezwa kuwa mkombozi mkubwa kwa watu waliokuwa na matatizo ya uvimbe hawa wanawake ambao wamekuwa wakipata changamoto ya uzazi.

Wataalamu wakimwandaa mgonjwa kuingiza kwenye mtambo mpya na wa kisasa ambao umenunuliwa na Hospitali ya Kairuki  unaoitwa High Intensity Focused Ultrasound (HIFU), ambao unatibu uvimbe bila upasuaji kwa kutumia mwangwi wa sauti.

Mtaalamu mwendeshaji wa mtambo huo, Dr. Fredy Rutachunzibwa, amesema mtambo huo tiba unatibu vimbe za aina mbalimbali kwenye kizazi, figo kongosho, ini, mifupa, matiti na uvimbe wowote unaoweza kuonekana kwenye mtambo huo.

“Tunamshukuru sana Rais wetu kwasababu haya yote ni mafanikio ambayo yametokana na jitihada zake za kuigeuza Tanzania kuwa kituo cha utalii tiba,  tiba kama hii si kwamba itawanufaisha watanzania pekee tunatarajia wagonjwa wengi Afrika watamiminika kupata tiba hii Tanzania kwasababu hii ni teknolojia mpya,” amesema.

Amesema kuwa mtambo huo ambao ulianza kufanyakazi Januari mwaka huu, unao uwezo wa kutibu hadi wagonjwa 10 kwa siku.

Amesema faida za tiba kwa kutumia mtambo huo ni kwamba mgonjwa hapati maumivu makali,  anapata nafuu haraka, kutopoteza damu na kuepukana na makovu ya upasuaji.

Amesema tayari wagonjwa wanne (4) wamefanyiwa matibabu hayo tangu kuwasili kwa  mtambo huo ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi hivi karibuni.

“Mtambo huu mbali na kuwa na uwezo huo utawanufaisha sana wanawake wenye kusumbuliwa na vimbe zinazosababisha changamoto za uzazi sasa vimbe zikiondolewa watapata ujauzito kwa urahisi,” amesema.

Wataalamu wakimwandaa mgonjwa kuingiza kwenye mtambo mpya na wa kisasa ambao umenunuliwa na Hospitali ya Kairuki  unaoitwa High Intensity Focused Ultrasound (HIFU), ambao unatibu uvimbe bila upasuaji kwa kutumia mwangwi wa sauti.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kairuki, Dk. Asser Mchomvu, amesema mtambo huo ni wanne (4) kwa Afrika na kwamba uko pia kwenye nchi za Misri, Afrika Kusini, Nigeria na sasa uko Tanzania kwenye hospitali hiyo.

Amesema hospitali hiyo imewapeleka nje ya nchi wataalamu wake wawili kupata mafunzo na tayari wamemaliza na wameshabobea kuendesha mtambo  huo.

 “Uwezo wa mashine ni kutibu hadi wagonjwa 10 kwa siku ila inategemea aina ya vimbe aliyonayo mgonjwa.  Kwasababu kuna mwingine anakuwa na vimbe hata nne,” amesema na kuongeza

 “Zamani tulikuwa tunafanya upasuaji kwa kufungua tumbo, tukahamia kwenye njia ya upasuaji kwa kutumia matobo na sasa hivi tumeendelea zaidi tunatoa uvimbe huo huo bila kupasua wala kuweka matobo hiki nikiwango cha juu zaidi cha matibabu,” amesema.

Dk. Mchomvu amesema tayari Hospitali hiyo imeunda timu maaalum ya kutibu bila kufanya upasuaji inayoitwa HIFU Kliniki itakayokuwa inaendeshwa na wataalamu wabobezi wa hospitali hiyo.

Wataalamu wakimwandaa mgonjwa kuingiza kwenye mtambo mpya na wa kisasa ambao umenunuliwa na Hospitali ya Kairuki  unaoitwa High Intensity Focused Ultrasound (HIFU), ambao unatibu uvimbe bila upasuaji kwa kutumia mwangwi wa sauti.

By Jamhuri