Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imezitaka familia zenye uhitaji wa kutoa huduma ya malezi ya kambo na kuasili kuwasilisha maombi yao kwa kamishna wa ustawi wa jamii kupitia halmashauri zao.
Wito huo umetolewa na Waziri Dkt Dorothy Gwajima , alipokuwa akihutubia mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo.
Dkt Dorothy amesema takwimu zinaonesha huduma ya malezi ya kambo na kuasili imeongezeka kutoka watoto 85 (wavulana 45 na wasichana 40) mwaka 2022 hadi kufikia watoto 562 (wavulana 279 na wasichana 283) mwaka 2025.
Amesema wizara imeandaa mwongozo wa taifa wa uendeshaji, usimamizi na uratibu wa mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa (2023).
Amedai kupitia mwongozo huo, migogoro ya ndoa iliyotatuliwa imeongezeka kutoka migogoro 12,068 kwa mwaka 2022 hadi migogoro 100,464 mwezi Juni, 2025.
Amesema utekelezaji wa kampeni za kijamii ,unalenga kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kukabiliana na kupinga vitendo vya ukatili.
‘’Serikali kwa kushirikiana na vikundi vya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii (SMAUJATA), Sauti ya Watoto Tanzania (SAWATA), Malezi Bora Network na Lemachu vimeweza kuibua, kukemea na kutoa elimu kwa jamii kuhusu vitendo vya ukatili ambapo tangu kuanzishwa kwa kampeni hizo jumla ya matukio 799 yameripotiwa na kushughulikiwa.
Kuwajengea uwezo wataalam wa sekta mbalimbali kukabiliana na vitendo vya ukatili hususani polisi jamii 4,542 (me 3,860 na ke 682), wasimamizi wa mashauri ya watoto wa kujitolea 15,255 (me 7,250 na ke 8,005),
Wahudumu wa afya 10,534 (me 8,922 na ke 1,612), maafisa ustawi wa jamii 1,342 (me 527 na ke 813), walimu wa unasihi/malezi 13,636 (me 6,509 na ke 7,127) na wasimamizi wa mashauri katika ngazi ya jamii 2,755.amesema.
Katika hatua nyingine, ameiomba jamii kuvitumia vyuo vya maendeleo ya jamii na ufundi, kupata maarifa na ujuzi utakaochangia kujiletea maendeleo kwa kujiajiri, kuajiriwa, na kuajiri wenzao.
Amesema ili kuwa na taifa lenye wananchi, wazalendo na lenye kuzingatia maadili ya kijamii ni muhimu kuwekeza kwenye malezi na makuzi bora ya watoto.
‘’katika kufikia lengo hilo, serikali inaendelea kushirikiana na wadau kutoa elimu ya malezi kupitia mwongozo wa wajibu wa wazazi na walezi katika malezi na matunzo ya watoto na familia.
Aidha amesema ni umuhimu wazazi wote wawili, kushirikiana katika kuwalea watoto ili kufikia ukuaji timilifu kimwili, kiakili na kisaikolojia na kuwa karibu nao ili kutengeneza muunganiko (bondi) na hivyo kuwezesha upendo toshelevu kwa pande zote kwani ikikosekana kunapelekea watoto kutokuwa na upendo na wazazi.
Dkt Dorothy amesema katika kuimarisha wajibu wa wazazi katika malezi ya vijana balehe,wizara imeanzisha programu ya kuwafundisha wazazi mbinu za kuwalea na kuwaongoza watoto wao ili waweze kukabiliana na changamoto za ujana balehe.
Katika hatua nmyingine amesema utoaji wa huduma ya ulinzi na matunzo kwa wazee imeendelea kutekelezwa kwa ambapo katika kipindi cha 2022 hadi 2025, wizara imetoa huduma za msingi 1256 544 ikiwemo bima ya afya sambamba na uanzishaji mabaraza 20,768 katika ngazi za kijiji/mtaa, kata na halmashauri.
Pia serikali inahimiza vyama kuandaa sera za ndani zinazohakikisha nafasi za uongozi zinakuwa wazi kwa wanawake zisizo na ubaguzi ili kuhakikisha zinawalinda dhidi ya kauli au vitendo vya udhalilishaji.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, jumla ya majukwaa 15,147 yameanzishwa na shabaha ni kufikia majukwaa 20,748,ambapo lengo kuongeza chachu kwa wanawake kujifunza masuala ya ujasiriamali, elimu ya fedha na uwekezaji.
‘’Kwa sasa ajenda ya taifa ni kuwekeza katika afya na maendeleo ya vijana balehe nchini,ambapo inahamasisha umuhimu wa huduma bora za afya na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa vijana balehe .
Hivyo nawaomba wafanyabiashara ndogondogo kujitokeza kwa wingi na kusajiliwa kwenye mfumo wa kupitia maafisa maendeleo ya jamii katika halmashauri zenu,
Amani ni msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii, hivyo, kukosekana kwa amani kunasababisha athari hasi hasa kwa makundi maalum yakiwemo wazee, wanawake na watoto,,amesema.
Dkt Dorothy amesema dira ya maendeleo (2050) ,inalenga kujenga taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea kwa kuwekeza zaidi kwenye sekta zinazoajiri watu wengi.



