Hapo awali niliandika  namna  sheria isivyowaruhusu viongozi  wa  serikali  za mitaa  (watendaji kata, wenyeviti wa mitaa, wajumbe, na ule uongozi wote wa huko chini) kuandaa  na  kusimamia  mauzo  na manunuzi  ya nyumba au viwanja, kwa ujumla ardhi. Nikasema kuwa kitu hicho  hakiruhusiwi  katika  sheria  na wanaofanya  hivyo wako  katika  makosa  makubwa.

Asilimia kumi wanayowatoza ni makosa na ndiyo maana hailipwi kwenye akaunti ya serikali bali mkononi au utapewa risiti za kuchana kwenye daftari badala ya EFD, wizi mtupu.

Leo tena tutazame kama unaweza kuruhusiwa kubadili jina la ardhi kutoka kwa aliyekuuzia kwenda kwenye jina lako ikiwa ulisimamiwa na serikali za mitaa katika ununuzi hasa wa ardhi iliyopimwa.

Sheria Namba 4 ya 1999, Sheria ya Ardhi, Kifungu cha 62(1) kinasema kuwa kila nyaraka (document) ya ardhi iliyosajiliwa ambayo itatumika katika  mauzo, rehani, zawadi, kurithi au pango ni lazima iwe katika mfumo wa fomu maalumu. Kifungu hiki kinaturejesha katika kanuni za ardhi za mwaka 2001 ili kuziona fomu zinazohusika katika manunuzi ya ardhi na mahitaji yake.

Fomu ya kwanza ni fomu namba 38 ambayo ni sawa na mkataba wa mauzo (contract for disposition). Fomu hii inalazimisha kuwa iwe imegongwa muhuri wa wakili au kushuhudiwa na wakili.

Fomu ya pili ni namba 35, ambayo kisheria ni nyaraka ya kuhamisha umiliki (transfer of right of occupancy). Fomu hii nayo inatoa ulazima wa kuwa imeshuhudiwa na kugongwa muhuri wa wakili pande mbili, yaani upande wa mhamisha umiliki/muuzaji na upande wa mpokea umiliki/mnunuzi.

Maana yake ukipeleka nyaraka (documents) za ununuzi wa ardhi uliosimamiwa na kusainiwa na serikali za mitaa bila ushuhuda wa wakili kwa lengo la kubadili jina hazitapokelewa. Iwe umezipeleka ardhi ya wilayani au wizarani kote hazitapokelewa kwa sababu zitakuwa hazijakidhi mahitaji ya kisheria.

Aidha, kwenye sheria nilizotaja hapo juu, hakuna popote alipotajwa serikali za mitaa. Kwa waliowahi kuwatumia serikali za mitaa halafu wakaenda kuhamisha umiliki (transfer) wanajua namna walivyorudishwa.

Serikali za mitaa hawaruhusiwi na nyaraka hizi za kisheria hazijaweka sehemu yao ya kusaini au kugonga muhuri.  Wakili ni mtu pekee anayetajwa na sheria hizi.

Kazi kubwa ya serikali za mitaa katika ununuzi wa ardhi ni kumtambulisha muuzaji ikiwa mnunuzi ataamua kwa hiari yake kuwatumia kutaka kumjua muuzaji huyo.

Wakati mwingine mnunuzi atawahusisha ikiwa atahitaji  kujua historia ya eneo husika. Hata hivyo hatua hizi zote za kuwahusisha ni hiari, si takwa la kisheria. Mnunuzi au muuzaji anaweza kuamua kuwahusisha au asiwahusishe.

Please follow and like us:
Pin Share