Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, ametoa mwito kwa wananchi wenye kustahili kuwa na silaha kuomba wamilikishwe ili wajilinde dhidi ya wahalifu.

IGP Sirro alitoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari, ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia tukio lenye ukakasi la kutekwa mfanyabiashara Mohammed Dewji (Mo), Oktoba 11, mwaka huu. Tunampa pole Dewji kwa yote yaliyomkuta. Tunamwomba asife moyo, bali aendelee kushiriki kuujenga uchumi wa taifa letu, maana mchango wake ni mkubwa.

IGP Sirro alisisitiza kuwa pamoja na hali ya amani na utulivu iliyopo nchini, ni vizuri watu wakajihami kwa kuhakikisha wanaomba na kumilikishwa silaha.

Tunampongeza IGP Sirro kwa mwito huo, tukiamini kauli yake haimaanishi kuwa sasa Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye dhima ya kulinda raia na mali zao limelemewa. Bila shaka amesema hivyo akiamini kuwa ulinzi wa taifa unaanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja.

Hata hivyo, tuna ushahidi kuwa wapo wananchi walioomba silaha kwa miaka mitatu hadi minne sasa bila mafanikio. Wamenunua silaha, wamelipia kila kitu tangu mwaka 2016 lakini hadi sasa hawajakabidhiwa.

Kama IGP Sirro anahitaji ushahidi wa hayo, awaulize wakuu wa Kamati za Ulinzi na Usalama katika wilaya za Ilala, Ubungo, Kinondoni na kwingine katika Jiji la Dar es Salaam na mikoani.

Pamoja na nia nzuri ya uhakiki wa silaha ili zisiangukie mikononi mwa wabaya, kigezo hicho kimegeuzwa na kuwa urasimu na usumbufu mkubwa. Tupo tayari kumpa IGP Sirro ushahidi wa ucheleweshaji huo.

Pamoja na nia nzuri ya IGP Sirro kama tulivyosema hapo juu, bado tunaamini wingi wa silaha pekee nchini si jawabu la kukomesha utekaji, uporaji na mauaji ya watu. Jeshi la Polisi lisikwepe dhima yake kuu ya kuwalinda raia na mali zao.

Pia tunaamini kwa ngazi ya IGP anaweza kuwa na ushawishi kwa viongozi wakuu wa serikali ili kuhakikisha mfumo wa Nyumba Kumi unarejeshwa, maana huko ndiko wananchi wanakofahamiana. Kufutwa au kuzorota kwa mfumo huo kumeathiri ulinzi na usalama katika jamii. CCTV za kweli na za uhakika ni wananchi wenyewe kwanza.

Mwisho, tunamuomba IGP Sirro afuatilie kujua ni kwanini watu walioomba silaha wana miaka zaidi ya mitatu hawajapewa.

By Jamhuri