Ili kukuza uchumi Tanzania isibadili tu itikadi, ibadili mbinu pia

DAR ES SALAAM

NA JOHN KIMBUTE

Mwelekeo wa sasa wa sera za nje za Tanzania una tofauti kiasi fulani na tulichozoea awali, na kwa njia hiyo imebidi viongozi serikalini wafanye kazi ya ziada ya kuainisha maeneo ya fikra au itikadi ambayo mwanzoni yalikuwa hayatiliwi maanani, licha ya kuwa yanafahamika.
Moja ya matukio ya kufafanua hali hiyo ni maelezo ambayo alitoa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, wakati akifungua Ubalozi wa Tanzania nchini Israeli takriban miaka miwili iliyopita.
Alizungumzia masuala kadhaa yanayoonyesha  mwelekeo wa Tanzania katika misuguano ya kimataifa na kama ilivyo kwa Marekani na nchi nyingine duniani, kuna umuhimu mkubwa zaidi unawekwa katika kuangalia masilahi ya taifa kuliko mifungamano ya kiitikadi ya zamani.
Licha ya kuwa suala hilo ni pana, yako maeneo mengine ya uendeshaji wa sera za nchi za nje ambayo yanaendana na kile alichosema Waziri Mahiga, mojawapo ikiwa ni uendeshaji wa ofisi za kibalozi nchi za nje.
Wazo jipya ni kuwa hulka inayotawala huko isiwe siasa, itikadi na mifungamano ya aina hiyo, ila uchumi. Diplomasia ya uchumi ina maana kuwa hakuna marafiki wa jadi na washindani au hata maadui wa jadi kiitikadi ambao hatuwahitaji kiuchumi, lakini ukiangalia kwa karibu unakuta kuwa yako maeneo ya sera zetu za uchumi na diplomasia ya uchumi kwa jumla ambayo yanakwenda kinyume cha matazamio hayo.
Kimsingi ni kuwa diplomasia ya uchumi inatakiwa iwe na jicho pevu kuangalia faida ya aina fulani ya uwekezaji, na si mpangilio imla wa kiitikadi.
Katika mazingira ya sasa, kuna itikadi moja tu ambayo inaendelea kutetewa, kwani si itikadi mpito kama zile za nyakati za ukombozi na ushindani wa mataifa makubwa yenye mifumo tofauti ya jamii, kama alivyoeleza Waziri Mahiga.
Itikadi inayoendelea kutetewa hivi sasa ni ile ya uzalendo, tena kwa kiwango fulani imeshika kasi zaidi kutokana na mabadiliko ya usimamizi wa uchumi tangu mwisho wa mwaka 2015, ambako uelekeo legelege wa kusimamia rasilimali za nchi na hata ukusanyaji wa mapato uliondolewa, itikadi hiyo ya uzalendo ikiwa ni kaulimbiu muhimu ya kuunganisha hisia kwa suala hilo.
Kwa hili hakuna suala la kubadili uelekeo ila kuna uwezekano mbinu za kutambua uzalendo chanya na uzalendo butu au hata hasi hazijaeleweka.
Tanzania hivi sasa iko katika mazingira yanayofanana na kile kilichotokea nchini China mwaka 1976 baada ya kifo cha Mwenyekiti Mao, ambapo kwa miaka miwili kulikuwa na vuta – nikuvute ndani ya Chama cha Kikomunisti (kiite chama cha mapinduzi ya China) kuhusu itikadi gani inapaswa kufuatwa.
Suala lilikuwa kwamba kuanzia kukamilika kwa vita ya ukombozi mwaka 1949 hadi 1976 kimsingi China ilibakia nchi maskini, licha ya kufikia ngazi ya kuwa na silaha za nyuklia, kama ilivyo Korea Kaskazini leo.
Katika kipindi cha miaka kumi hadi anafariki dunia Mwenyekiti Mao alifuata itikadi ya kimapinduzi ambayo ilizuia kuingia kwa mitaji nchini humo, wakitumia nguvu za umma (kuifanyia kazi serikali na sehemu kubwa ya kinachopatikana kwenda katika maendeleo yanayosimamiwa moja kwa moja na idara za serikali, si makampuni). Wengi waliona mkwamo.
Kati ya makada waandamizi waliokuwa wanataka mabadiliko alikuwamo Deng Xiaoping, ambaye miaka iliyotangulia (kuanzia miaka ya 1960 katikati) alianza kutetea mwelekeo wa kiliberali ndani ya mapinduzi, akachukua nahau ya Kichina; haijalishi kama paka ni mweupe au mweusi ilimradi anakamata panya. Alikuwa anamaanisha kuwa si tatizo maendeleo yanapatikana kwa itikadi gani. Akafaulu kuanza kuteka hisia katika chama, na alipofariki dunia Mao, jeshi likasimamia akiongoze chama.
Alipewa nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya Kudumu ya Chama ya Jeshi, yaani kitengo cha Kamati Kuu (inayofanana na Halmashauri Kuu hapa) kinachosimamia masuala ya ulinzi na usalama, ambacho kilikuwa ndiyo ngao halisi ya utawala nchini.
Akabadili mwelekeo na kuwa na mifumo miwili, ule wa kijamaa katika eneo la bara, na ubepari wa kimataifa (utandawazi, ununuzi wa ardhi makampuni binafsi ya China yenye ubia kifedha na wazalendo), hivyo mabilioni ya dola yakaanza kuingia.
Katika muongo wa kwanza ilifikia kiasi cha dola bilioni 20 kwa mwaka, halafu ikafikia dola bilioni 30 na hadi mwaka 2008, kiasi cha dola bilioni 40 hadi 49 kilikuwa kinaingia China kwa mwaka katika uwekezaji, Wachina waliokuwa nje na wenyeji.
Kimsingi, njia hiyo ndiyo inayotakiwa kufuatwa hapa nchini ili maendeleo yafanane na yale ya China, kwani kuna njia tofauti mbili zinazoelekea lengo moja, na lazima mojawapo ichaguliwe itumike, si kukwepa kila kitu na kufuata misingi ambayo hasa ni Ujamaa, ulioboreshwa kwa biashara huria ya bidhaa.
Hatujapiga hatua katika kubadili mifumo ya msingi ya uchumi ambayo hasa inajikita katika umiliki wa ardhi, hivyo uwezo wa umiliki wa mali isiyohamishika, na uwezo wa kukopeshwa kutokana na umiliki ardhi.
Hadi sasa ni mikopo binafsi inayotegemea umiliki kwa mfano wa nyumba, shamba au kiwanja, si ujenzi wa viwanda kwani mkopo mkubwa hauwezi kuziegemea hakimiliki za jadi. Hali hii ikiendelea ujenzi wa uchumi wa kisasa ni ndoto.
Unaweza kuwa na milki binafsi nchi nzima, au ukaanza na ukanda wa mikoa kadhaa ya pwani. Ndiyo maana fikra za Deng Xiaoping ni muhimu kwani hapa nchini zinaendana na maelekezo ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye alitumia busara za hayati Shaaban Robert kuwezesha umma kukubali mabadiliko, hasa uchumi kama uliounganishwa katika dunia, licha ya kuwepo maeneo ya kujisimamia sisi wenyewe na wageni kutii sheria, kama ilivyo popote.  Busara hizo ni pamoja na kwenda na wakati; inaendana na usemi wakati ukuta usipigane nao.
Lakini suala la haki ya ushiriki wa uchumi na hasa uhitaji wa mitaji kutoka nje ambayo kimsingi inaingia ubia na wenyeji, kwani wageni hawawezi kupita Ilala na Kariakoo kutatua matatizo ya aina hii au ile, halikwepeki.
Wakati ule uelekeo huo ulibezwa, na sasa tumefika mahali tunahitaji uchumi wa viwanda kwa udi na uvumba, na waliokataa mwelekeo wa Rais Mwinyi wanaapa kuwa tutafaulu kwa mbinu zisizotofautiana kimsingi na zile zilizokwama wakati ule wa Ujamaa.
Liko eneo jingine linaloendana na hili la mitaji ya nje kufurika, kwa kuondoa ukiritimba wa makampuni ya serikali (yanaitwa mashirika ya umma) katika sekta zote muhimu za uchumi, ambalo ni mkwamo wa kilimo kinacholenga umma wa Watanzania ulioko vijijini. Kuna hatari kuwa juhudi za kuboresha kilimo hicho ili wananchi hao kwa jumla wanufaike ukakwamisha juhudi za kuinua uchumi, kwani mkulima analima kwa mahitaji ya chakula na kuuza ziada kidogo tu.
Akilima kwa mbinu za kisasa apate kuuza mara mbili au tatu zaidi, bei zinashuka na uharibifu wa mazao unafuata, kukatisha tamaa wakulima na vijana kuhamia mijini bila mitaji, kuingia biashara za kubahatisha, kutembeza nguo au mkanda mmoja mmoja, na kuanza wizi.
Pale ardhi ikiingia hakimiliki binafsi na si ya jadi, Watanzania walioko ndani na nje wenye fedha watanunua sehemu kubwa na wanaouza waanze shughuli za uchumi wa kisasa ili kuajiri watu wengi ambao sasa hawana kazi.
Kutokana na kupanuka kwa mahitaji, watu wakipata kazi na vipato vya uhakika, uchumi wa viwanda utasimama, tofauti na sasa ambapo bidhaa mpya zitadoda kama zitahitaji kushindana na zile za bei poa kutoka nje — na kutengeneza bidhaa maalumu zinazohitaji soko linalopanuka.
Litapanuka endapo ukiritimba wa dola utaondolewa na mitaji iingie, ijenge ushindani wa makampuni maridhawa katika kila sekta — dhana inayohitaji ushiriki, si ukiritimba.
 
mwisho