Uamuzi wa Busara ni jina la kitabu kilichochapishwa na Ofisi ya Katibu Mtendaji Mkuu wa TANU, kimebeba mambo muhimu yaliyoamuliwa kuhusu taifa kabla ya kupata uhuru.

Yapo mambo ambayo kama yasingefanyika ingekuwa vigumu kujua historia ya nchi hii ingekuwaje leo. Mathalani, kama TANU ingekataa kushiriki katika Uchaguzi wa kura tatu mwaka 1958, sijui tungekuwa wapi.

Hali kadhalika kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere asingeamua kuacha kazi ya ualimu, historia ya nchi yetu huenda ingekuwa tofauti na ilivyo sasa.

Kupitishwa kwa Azimio la Arusha, kuukubali Mwongozo wa Chama na mengine mengi. Hivyo kitabu hiki ni cha maana sana kwa historia ya nchi yetu kwani bila uamuzi uliomo humu kitabuni, historia yetu isingekuwa kamili. Endelea…

Uamuzi wa Mwalimu Nyerere kuacha kazi ya ualimu

Siku ya Jumapili tarehe 22/3/1955 Mwalimu Julius K. Nyerere alifanya kitendo kimoja kikubwa cha ushujaa na busara, ambacho kama hakingefanyika, labda historia ya nchi yetu ingekuwa tofauti kabisa na ilivyo leo.

Kitendo hicho ni uamuzi wa kuacha kazi ya ualimu aliyokuwa akifanya katika Shule ya Sekondari ya Pugu, ambayo iko maili 12 tu kutoka mjini Dar es Salaam. 

Mwalimu Nyerere alipewa kazi ya kufundisha katika shule hiyo tarehe 9/10/1952 baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Edinburgh, Uingereza, na kujipatia digrii ya M.A. mwezi Julai, lakini kuanza kazi hasa alianza mwezi Feburuari 1953.

Na tangu wakati huo akaanza kujishughulisha na Chama cha Tanganyika African Association (TAA) mjini Dar es Salaam. Baada ya miezi miwili tu, yaani mwezi Aprili, 1953, kulikuwa na uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

Aliyekuwa rais wa chama mpaka wakati huo alikuwa Abdul Sykes, ambaye alisimama tena kugombea uchaguzi, na Mwalimu Nyerere naye akasimama. Kura zilipopigwa Mwalimu Nyerere akapata ushindi, kwa hiyo ikawa amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha TAA.

Wale ambao wamepata kusikia habari za Chama cha TAA wanajua kwamba chama hicho hakikuwa chama cha siasa. Hali hii haikumridhisha hata kidogo Mwalimu Nyerere, kwa hiyo jitihada yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa kukiongoza  chama hicho ikawa ni kukibadili kiwe chama cha siasa. Akaanza kuichunguza kwa umakini Katiba ya TAA na kutafuta njia za kuibadilisha iwe na madhumuni ya kisiasa.

Tarehe 10/10/1953 kulikuwa na Mkutano wa TAA katika nyumba iliyoko Mtaa wa Lumumba, mjini Dar es Salaam. Kulikuwa na viti viwili tu ndani, Mwalimu Nyerere akakalia kimoja, mzee John Rupia akakalia kingine, wajumbe wengine kina Abdul Sykes, Ally Sykes na Dossa Aziz ikawabidi wakae kwenye masanduku tu yale ya kusafirisha mizigo.

Rashidi Kawawa alikuwa mtumishi wa serikali wakati huo, na tarehe 1/8/1953, Gavana Twining alikuwa amepiga marufuku watumishi wote wa serikali wasiwe wanachama wa TAA wala wasiwasaidie shughuli zake.

Katika mkutano huo ndipo Mwalimu Nyerere akawaeleza wenzake mawazo yake juu ya umuhimu wa kubadilisha TAA kiwe chama cha siasa. Wenzake waliyafurahia mawazo hayo, na wakakubaliana wafanye matayarisho yaliyohitajika ili waweze kupendekeza mabadiliko hayo katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa TAA ambao ungefanywa mwezi Julai, 1954.

Jambo mojawapo lililozungumziwa kwa kirefu lilikuwa ni jina la chama hicho, baada ya kukibadilisha na kukifanya chama cha siasa, kiitweje?

Abdul Sykes akatoa wazo kwamba kiitwe Tanganyika African Union, lakini wenzake wakakataa kwamba jina hilo lingefanana  mno na Kenya African Union (KAU) ambayo ilikuwa imepigwa marufuku Kenya, ikaonekana pengine kwa sababu hiyo serikali ingekataa kukiandikisha chama kwa jina hilo la Tanganyika African Union.

Mwalimu Nyerere akatoa wazo kwamba labda liongezwe neno ‘National’ baada ya Tanganyika, hapo bila  shaka litakubaliwa. Yaani chama kiitwe Tanganyika National African Union.

Hapo Ally Sykes akapinga, akasema kifupi cha Tanganyika National African Union ni T.N.A.U na haipendezi hata kidogo kutamka, kwa  hiyo akashauri maneno yapangwe vizuri zaidi yawe Tanganyika African National Union, ambayo kifupi chake kitakuwa T.A.N.U kila mtu akatamka TANU na akaona imependeza, basi wakakubaliana wapendekeze jina la TANU. Na hivyo ndivyo jina letu lilivyopatikana.

Mkutano wa mwaka wa T.A.A ulipofanyika tarehe 7/7/1954, mapendekezo ya mabadiliko hayo yakatolewa na kukubaliwa, na TANU ikawa IMEZALIWA. Vilevile chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere. Wakati huo wote lakini alikuwa anaendelea na kazi yake ya ualimu katika Shule ya Pugu.

Mwezi Februari, 1955, Mwalimu Julius Nyerere, Kiongozi wa TANU alisafiri kwenda New York, Amerika kwenye Umoja wa Mataifa kuhutubia Baraza la Wadhamini la Umoja wa Mataifa.

Nyakati hizo Tanganyika ilikuwa chini ya Umoja wa Mataifa, na Uingereza ilikuwa inatutawala kwa niaba tu ya Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa ulikuwa na mtindo wa kutuma ujumbe kuja Tanganyika karibu kila miaka miwili kukagua utawala wake unavyoendeshwa na kutoa taarifa kamili kwenye Baraza la Wadhamini la Umoja wa Mataifa.

Mwezi Agosti 1954 ulikuja ujumbe wa aina hiyo hapa Tanganyika, na taarifa yao ni kama ilivyoelezwa hapo awali. TANU ilifurahishwa na taarifa hiyo. Kwa hiyo ikaamua kupeleka ujumbe wake huko huko kwenye Umoja wa Mataifa wakati ambapo taarifa hiyo ingejadiliwa ili aweze kutilia mkazo zaidi na kueleza kwa kirefu zaidi nia na matumaini ya watu wa Tanganyika, na juu ya chama kipya cha TANU kilichokuwa kimeanzishwa, na kueleza makusudio ya chama chetu ya kuwatayarisha Watanganyika kujitawala wenyewe.

Mwalimu Nyerere akachaguliwa kwenda kufanya kazi hiyo. Gavana alipopata habari hizo akashituka sana. Yeye na Serikali ya Uingereza kwanza hawakuipenda taarifa ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa, hivyo kusikia TANU inapeleka mjumbe New York, na mjumbe mwenyewe ni Julius Nyerere, gavana akaamua naye apeleke ujumbe mzito wa watu watatu wakubwa sana kumpinga Mwalimu Nyerere huko kwenye Mkutano wa Baraza la Wadhamini.

Jambo hilo likapitishwa haraka katika Baraza la Kutunga Sheria (Legco), lakini wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria wakakatazwa kabisa wasitoe siri hiyo kwa Mwalimu Nyerere au kwa kiongozi yeyote wa TANU.

Baada ya mkutano huo wa Baraza la Kutunga Sheria, wajumbe watatu Waafrika wakapanda gari moja kurudi pale ‘Chiefs Quarters’ walipokuwa wamefikia.

Hiyo ilikuwa ni Februari tarehe 10, 1955. Walipofika Morogoro Road, wakamuona Mwalimu Nyerere anatembea kwa miguu…Nini kilitokea baada ya wajumbe hao kumuona Mwalimu Nyerere? Tukutane wiki ijayo…

1462 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!