Na Isri Mohamed

Michuani ya AFCON inazidi kushangaza wengi kufuatia matokeo mabaya ya timu ambazo kutokana na ubora wa wachezaji wake zilitarajiwa kufanya vizuri ikiwemo Côte d’Ivoire, ambayo usiku wa kuamkia leo imepokea kichapo cha mabao manne kwa nunge kutoka kwa Equatorial Guinea.

Maelfu ya mashabiki wa timu ya Côte d’Ivoire walionesha kuchukizwa na namna wachezaji wao walivyokuwa wakicheza na wakaamua kuondoka katika uwanja wa Alassane Ouattara kabla ya dakika 90 kuisha, huku wengine wakimalizia hasira na machungu yao kwa kuharibu magari na kuvunja vioo vya mabasi ya timu.

Mashabiki waliosalia uwanjani nao walishindwa kuzuia hasira zao wakarusha chupa za maji na viti uwanjani, kitendo kilichowapa tabu wasimamizi waliokuwa wakijaribu kuwazuia.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Côte d’Ivoire walilazimika kusindikizwa hadi kwenye vyumba vyao vya kubadilishia nguo chini ya ulinzi mkali ili wasije wakafanyiwa fujo.

Matokeo ya jumla ya timu ya taifa ya Ivory Coast (Côte d’Ivoire) ambao ndio wenyeji wa michuano ni ushindi wa mechi ya kwanza dhidi ya Guinea Bissau, kupoteza kwa bao moja kwa bila mbele ya Nigeria na jana kumiminiwa mvua ya magoli na Equatorial Guinea.

Kwa Sasa Côte d’Ivoire wanasubiri hatma yao kwenda hatua inayofuata kwa mwamvuli wa best looser.