Jaji wa mahakama ya New York ameamua kuwa hatia aliyopatikana nayo Donald Trump katika kesi ya kutoa pesa za kutunza siri ni halali, amekataa hoja ya rais mteule kwamba hatia hiyo inapaswa kutupiliwa mbali kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Marekani juu ya kinga aliyonayo.
Mwezi Julai, mahakama ya juu ya nchi hiyo iliamua kwamba marais wana kinga dhidi ya mashtaka ya jinai kwa maamuzi rasmi wanayochukua wakiwa madarakani.
Lakini siku ya Jumatatu, Jaji katika jiji la Manhattan jimboni New York, Juan Merchan – ambaye aliongoza kesi ya Trump – aliwaunga mkono waendesha mashitaka, akisema hukumu juu ya makosa 34 ya uhalifu iko kwenye maamuzi ya Trump yasiyo rasmi.
Uamuzi huo wa kutiwa hatia, ikiwa utadumu utamuweka Trump katika historia ya kuwa mhalifu wa kwanza kuhudumu katika Ikulu ya White House.
Katika uamuzi wake wa kurasa 41, Jaji Merchan alikataa hoja za Trump, akisema ushahidi ulioonyeshwa kwenye kesi hii ulihusu “mienendo isiyo rasmi,” aliandika.
Jaji alibainisha kuwa katika uamuzi wa Mahakama ya Juu imegundua kuwa “si kila kitu anachofanya rais ni rasmi,” hata kama kinafanywa kutoka Ikulu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, msemaji wa Trump, Steven Cheung, alikosoa uamuzi huo na kuutaja kuwa “ukiukaji wa moja kwa moja wa uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu kinga ya rais.”
Mwezi Mei, jaji wa New York alimpata Trump na hatia ya kughushi rekodi za biashara.
Hatia hiyo ilitokana na jaribio la Trump la kuficha malipo yaliyofanywa na wakili wake wa zamani, Michael Cohen, ambaye mwaka 2016 alimlipa nyota wa filamu za ngono ili asitoboe siri ya kufanya ngono na Trump.
Trump amekana makosa yote.