Jamii ipinge vijana wanaotangaza uzinzi wao

Mwaka 2020 umeanza na kituko cha kufedhehesha pale vijana wa kidato cha sita wa shule moja ya sekondari mkoani Mbeya walipoitaka serikali iwafanyie mpango wa kupata ‘kondomu’ ili waweze kujikinga na madhara ya uzinifu kama vile ugonjwa wa ukimwi na mimba zisizotarajiwa.

Mmoja wa mitandao ya kijamii ulitupasha tukio hili kwa kuandika:

“Wanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya sekondari … iliyopo jijini Mbeya wameomba huduma ya vituo vya afya na zahanati kuwapatia huduma ya kondomu ili waweze kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo ukimwi na zinaa.

“Maombi hayo yamewasilishwa na mmoja wa wanafunzi … wakati wa utoaji wa elimu mbalimbali kupitia michezo na asasi isiyo ya kiserikali (YES TANZANIA) ambapo … amesema suala hilo limekuwa changamoto kwao kwani umri walionao unaruhusu kuhisi hisia, hivyo inawabidi wafike kwenye vituo vya afya kuomba kupata huduma za kondomu ambazo zinaweza kuwasaidia kujikinga na ukimwi pamoja na mimba zisizotarajiwa.”

Hoja kuu katika habari hii ni kuwa vijana hawa wa kidato cha sita ambao kwa mfumo wa elimu wa Tanzania watakuwa na umri wa miaka 17 na kuendelea wanaanika hadharani tabia yao ya uzinzi na kwamba kwao tatizo si uzinifu, bali madhara ya uzinifu, yakiwemo magonjwa mbalimbali ya zinaa, ukimwi na mimba zisizotarajiwa.

Kwamba, baada ya tukio hili la kufedhehesha kimaadili tena kutoka kwa wanafunzi wa shule ya sekondari kusikika hadharani na kutokuwepo kauli yoyote ya kukemea kutoka kwa uongozi wa shule, mamlaka za elimu na jamii kwa ujumla ni ushahidi tosha kuwa jamii imefikishwa mahali kuona kilichosemwa na vijana wetu hawa ni jambo la kawaida, linajulikana, limezoeleka, kwa hiyo halishutui hata kidogo.

Kadhalika, ushiriki wa asasi isiyo ya kiserikali (NGO) kama chanzo na jukwaa la kutangaza ushuhuda huu wa mmomonyoko wa maadili katika jamii ya Watanzania ni ushuhuda mwingine wa kwa nini baadhi ya asasi zisizo za kiserikali zilifanya na zinaendelea kufanya juhudi kubwa kuona kuwa wanafunzi wanakuwa huru kufanya uzinifu bila ya kusumbuliwa na tishio la kupata mimba na endapo wakipata mimba wapewe likizo ya ujauzito na uzazi na hatimaye warudi shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua na hali ya mtoto aliyezaliwa itakapotengemaa. Kwao wao, tatizo si uzinzi wala ujauzito, bali kukatishwa masomo kwa msichana aliyepewa ujauzito.

Kwamba, pamoja na kuwepo tishio la kufukuzwa shule mwanafunzi wa kike akipata ujauzito bado mwezi Oktoba mwaka jana, 2019 kuliripotiwa wanafunzi 350 kati ya 602 wa shule moja ya sekondari katika wilaya moja iliyopo kusini mwa Tanzania walikatisha masomo kwa sababu ya utoro na mimba. 

Cha kutafakari ni kuwa, ikiwa hali ni hii ya mwanafunzi kutozingatia maadili mema na kujiingiza katika uzinifu bila kujali tishio la kufukuzwa shule endapo atapata ujauzito, hali itakuwaje pale wanafunzi wa kike watakapohakikishiwa kuendelea na masomo pamoja na kupata ujauzito unaotokana na ukware wao shuleni?

Hivi wahisani wanaozipa asasi zisizo za kiraia fedha za kuendesha kampeni hizi za kubomoa na kumomonyoa maadili mema ya vijana wetu wanakusudia nchi hii kujenga jamii bora au bora jamii ambayo hata matendo ya laana kwao ni sehemu ya maisha?

Mshairi mmoja Mwafrika (Mmisri) Ahmed Shawqi (1868-1932) akizungumzia hali ya jamii iliyokosa maadili mema (tabia njema) alisema: “Jamii ikishambuliwa katika maadili na ikayapoteza, basi kusanyikeni kuifanyia maombolezo na vilio.” Yaani, ubora wa jamii ni jamii kupambwa na maadili (tabia njema) na kinyume chake ni jamii mfu iliyopoteza vionjo vya utu…jamii isiyoona soni mambo ya ajabuajabu yanapofanywa na wanajamii wakubwa kwa wadogo… jamii ambayo haijifakharishi kwa tunu na utamaduni wake wenye mnururisho wa mafunzo ya dini bali kuwaiga wasiopaswa kuigwa… wanaume kupenda vionjo vya kike… wanawake kupenda vionjo vya kiume… wengine kutamani kugeuza mpango wa Mwenyezi Mungu katika maumbile yao na muonekano wao… jamii mfu!

Turudi katika kituko cha vijana wetu kuiomba serikali iwafanyie mpango wa kupata kondomu ili wafanye uzinifu bila ya kuathiriwa na ukimwi, magonjwa mengine ya zinaa na mimba zisizotarajiwa. Tunajua kilichotufikisha hapa kama jamii?

Tuna matatizo na changamoto nyingi katika kinachoitwa malezi ya watoto na vijana. Ni dhahiri kuwa wazazi tumejivua jukumu la kuwalea watoto na vijana wetu kimaadili na tumejibakishia uwajibikaji katika kuwatimizia mahitaji yao muhimu ya kibinadamu (chakuka, mavazi na malazi) na yale yanayohusiana na maendeleo kama kuwapatia elimu na mengineyo. Wazazi, wengi wetu, hatufuatilii mabadiliko ya kimakuzi kwa watoto wetu na kila siku tunachelewa ‘kumkunja samaki angali mbichi’ au ‘kuuwahi udongo ungali maji’.

Mzazi, mlezi anapozembea katika malezi ya kimaadili ya mwanawe, anasaidia uharibifu wa walimu wa uharibifu katika jamii kupitia mitandao ya kijamii, ulimwengu uliofanywa kijiji kupitia maendeleo ya teknolojia ya habari na wasio na maadili miongoni mwa wanajamii. 

Mzazi anaweza kudanganywa na utulivu wa mwanawe aliye chumbani eti akiamini mtoto ni mwema, anajisomea wakati mtoto huyo amevunja kuta nne zinazomzunguka na anavinjari duniani na kuharibiwa na waharibifu wa maadili na wakati mwingine na makundi ya wasio na utu (radicalization).

Katika hali hii ni lazima wazazi watenge muda wa kutimiza jukumu lao la malezi ya kimaadili wakizingatia ukweli aliousema Khalifa wa Nne katika Uislamu – Sayyidinaa Ali Bin Abi Twaalib (Allaah Amridhia) kuwa: “Akili ya mtoto ni kama ardhi mpya (virgin soil), hukubali mbegu yoyote itakayopandwa.” 

Wazazi hawana budi kuzifanyia tathmini akili za watoto wao ili kubaini magugu na mbegu mbaya zilizopandwa na waharibifu ili wazing’oe mara moja, hususan wakati huu ambao mharibifu wa mtoto wa chini ya miaka kumi anapokuwa ni mwalimu uliyemkabidhi amfundishe!

Wazazi wapate muda wa kuvunja ukimya na kuwarudisha vijana wao katika maadili mema na kuwazindua kutowaona wamefanikiwa wale wakosefu wa maadili hata wakiwa ni mashuhuri katika jamii kwa kazi zao, utajiri wao na kingine chochote kile. Thamani ya mwanadamu ni utu wema na tabia njema na si kingine chochote.

Wazazi wawanasihi vijana wao kuepuka uzinifu na kukaa kinyumba, kwani hayo ni kinyume cha mafundisho ya dini zote za Ibrahimiyya (Uyahudi, Ukristo na Uislamu). Wajenge hoja juu ya ubaya wa uzinifu kama Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alivyojenga hoja kwa yule kijana aliyeomba ruhusa ya kwenda kufanya uzinifu. Acha nikukumbushe.

Kijana mmoja alimwendea Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akamwambia: “Ewe Mtume wa Allah, nipe idhini ya kuzini.” Watu wakamzunguka na kuanza kumuonya. Vipi anamuomba Mtume wa Mwenyezi Mungu ruhusa ya kufanya maasi? Mtume akawaambia: “Hebu mleteni karibu yangu.” Yule kijana akamsogelea Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akakaa.

Mtume akamuuliza: Je, utaridhia zinaa kwa mama yako?

Kijana akajibu: Hapana Wallaahi.

Mtume akamwambia: Vivyo hivyo na watu wengine hawaridhii kwa mama zao.

Mtume akamuuliza: Je, utaridhia kwa binti yako?

Kijana akajibu: Hapana Ewe Mjumbe wa Allaah.

Mtume akamwambia: Na watu wengine hawaridhii kwa mabinti zao.

Mtume akamuuliza: Je, utaridhia kwa dada yako?

Kijana akajibu: Hapana Wallaahi.

Mtume akamwambia: Na watu wengine hawaridhii kwa dada zao.

Mtume akamuuliza: Je, utaridhia kwa shangazi yako?

Kijana akajibu: Hapana Wallaahi.

Mtume akamwambia: Na watu wengine hawaridhii kwa shangazi zao.

Mtume akamuuliza: Je, utaridhia kwa ndugu wa kike wa mama yako (mama mdogo/mkubwa)?

Kijana akajibu: Hapana Wallaahi.

Mtume akamwambia: Na watu hawaridhii kwa ndugu wa kike wa mama zao (mama mdogo/mkubwa).

Kisha mtume akaweka mkono wake katika kifua cha kijana huyu na kumuombea dua: “Ewe Allah Msamehe madhambi yake, na uusafishe moyo wake, na ikinge tupu yake.”

Kijana akawa baada ya hapo hageuki kutizama chochote (miongoni mwa maasi).

Kwa hakika tukio la wanafunzi wa Mbeya wakiwa mabalozi wa sauti za wanafuzi wengine nchini lituzindue kuwa uzinifu sasa ni janga kubwa kwa jamii yetu na linaathiri vibaya kabisa mchakato wa kuitengeneza jamii kitabia na kisaikolojia na tusipochukua hatua sasa kwa serikali kuonyesha kwa vitendo kuwa inachukia uzinifu shuleni na katika jamii kwa ujumla, basi tutarajie kuendelea kujenga jamii mfu kimaadili, isiyo na utu wala ustaarabu, jamii ya kishetani inayoongozwa na matamanio ya kila mwanajamii na uhuru usio na mipaka na hatima yake ni mbaya sana.

Shime, jamii ipinge mmomonyoko wa maadili,

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata). Simu: 0713603050/0754603050