Siku kadhaa zilizopita Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa, amenukuliwa akisema polisi wataanza msako wa kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote wanaotarajia kujinyonga mwaka huu.

Kamanda Mwakalukwa anatukumbusha kuwa kazi yake ni kutekeleza sheria au kuchukua hatua za kudhibiti ukiukwaji wa sheria. Hilo halipingiki, ingawa uamuzi wake unafungua mjadala mpana zaidi juu ya matukio ya kujiua.

Sheria iko wazi kabisa. Mtu yeyote anayejaribu kujiua anakiuka sheria. Aidha, mtu yeyote anayejaribu kumshawishi mtu mwingine kujiua na ushawishi wake ukatekelezwa au atakayemsaidia mtu mwingine kujiua, naye atakuwa ametenda kosa la jinai.

Sheria zinatofautiana baina ya nchi moja na nyingine. Zipo nchi ambapo baadhi ya vitendo vinatajwa kuwa ni makosa kama ilivyo Tanzania. Lakini zipo nchi ambapo makamanda wa polisi hawana tatizo la Kamanda Mwakalukwa kwa sababu kosa la kujaribu kujiua au la kusaidia mtu mwingine kufanya hivyo hayapo kwenye vitabu vya sheria au utaratibu maalumu unaosimamiwa na daktari kuruhusu anayetaka kujiua kufanya hivyo. Nchi hizi ni pamoja na Uholanzi, Luxembourg, Ubelgiji na Canada.

Tofauti hii ya kisheria inatokana na uamuzi wa kuliona tatizo kuhitaji suluhisho la afya ya akili; kwamba zipo sababu za kisaikolojia ambazo zina uzito wa kutosha wa kutufanya tusimame na kutafakari kuwa inawezekana suluhisho ni tiba na si kifungo.

Litakuwa kosa kuwaweka kwenye kundi moja watu wote wanaojaribu kujiua, nikiamini kuwa sababu zinazowashawishi kufanya hivyo hazifanani.

Wapo watu wanaojaribu kwa dhati kujinyonga mpaka kujiondolea uhai, na wapo watu ambao hawana nia ya kujiondolea uhai lakini wanaonekana kujaribu kujinyonga kwa sababu ambazo hazina uzito. 

Wataalamu wa saikolojia wataniwia radhi kama maelezo yangu yataonekana hafifu au kama yapo makundi zaidi ya hayo, lakini ipo mifano inayoabainisha kuwepo kwa hayo makundi mawili.

Mtu anayekusudia kujitoa uhai hufanya hivyo bila dibaji, bila taarifa na bila utangulizi. Anafanya hivyo na akawaacha watu wanahoji sababu za kufanya hivyo. Wengine wa aina hiyo wanaweza wakafanya hivyo na kuacha ufafanuzi wa uamuzi wao.

Binadamu tunatofautiana kwa jinsi gani tunaweza kuhimili misukosuko ya maisha. Mafundisho ya dini yanatuasa kuwa hata kama tunakabiliwa na matatizo ya aina gani ni kosa mbele ya Muumba kujitoa roho. 

Lakini hata mafundisho ya dini yanashindwa kuzuia yanayotokea. Na sababu hiyo pekee inaweka uzito juu ya hoja kuwa uamuzi wa kujiua ni tatizo la kisaikolojia, kama tunakubaliana kuwa wengi wetu tunaongozwa na imani hizo za dini.

Kundi jingine ni lile ambalo mimi naliita la wababaishaji, watu ambao wanakabiliwa na tatizo ndani ya jamii na pengine si kubwa sana, na kuamini kuwa wakijaribu kujiua watapata huruma ya jamii.

Matukio ya hawa wa kundi hili nimewahi kuyashuhudia. Katika mfano mmoja ambapo mojawapo alijaribu kujiua kwa kumeza vidonge na taarifa hiyo kumfikia baba yake mkubwa, baba huyo, badala ya kumhurumia aliyetaka kujitoa uhai akakasirika na kuhoji kwanini hakununua na kumeza vidonge vya kutosha badala ya kusumbua familia yake. Aliyetaka kujiua alifanya hivyo baada ya kutuhumiwa na kusemwa kwa tabia yake ya wizi.

Anayekusudia kwa dhati kujiua angejaribu tena na tena mpaka afanikiwe. Huyu ndugu tuko naye mpaka hii leo anaishi na amejaliwa watoto kadhaa na wajukuu. Kwa lugha ya siku hizi, alikuwa ana-beep.

Kama nikiombwa maoni juu ya nani anastahili kusamehewa adhabu ya aina yoyote kwa mujibu wa sheria na badala yake kupewa huduma ya tiba, ningeshauri kundi la wale ambao wameona dunia imewaelemea sana mpaka wakaamua kujitoa maisha. Hawa wengine wangepewa kifungo tu kwa kusumbua watu halafu wakiwa gerezani watafakari upuuzi wa uamuzi wao.

Kwamba unawezaje kutambua nani ni mkweli na nani ni mbabaishaji, ni suala la taaluma ya tiba ya akili. Aidha, ni suala ambalo katika kuamua kesi iliyopo mbele yake, jaji au hakimu huangalia mazingira yote ya kesi na kuamua ni kwa uzito gani suala la hali ya akili ya mtuhumiwa wakati wa kutenda kosa inaweza kuwa chanzo cha kosa linalomkabili.

Bila kuangalia iwapo ni kosa kisheria kujaribu kijiua, nadhani ni wachache ambao watapinga kuwa mtu yeyote mwenye nia hiyo (kuacha wale wababaishaji) anakabiliwa na matatizo ya kisaikolojia. Anakabiliwa na suala ambalo ameshindwa kulivumilia. Ni mtu aliyekata tamaa na haoni njia nyingine ya kumaliza tatizo bali kwa kujiua.

Njia muafaka ya kuwasaidia wanajamii hawa ni kuwepo kwa mpango wa elimu kwa jamii kusaidia wanajamii wenzao kubaini mapema dalili za watu wenye mwelekeo huo, elimu ambayo pia itapendekeza hatua za kuchukua ili kuepusha matukio ya kujaribu kujiua.

Na hili si tatizo wala kazi ya Kamanda Mwakalukwa, au la Jeshi la Polisi kwa ujumla. Ikiwa hivyo tutakuwa tumewapa kazi isiyowalipa mshahara. Ipo haja pia ya kuangaliwa upya kwa sheria kuihamisha kutoka kwenye adhabu na kuielekeza kwenye tiba.

Barua pepe: [email protected]

By Jamhuri