Hukumu ya kifungo cha maisha gerezani imetolewa kwa Moses Method (23) mkulima na mkazi wa kijiji cha Kasuga wilayani Kakonko mkoani Kigoma baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili mwenye umri wa miaka tisa.

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kakonko,  Ambilikile Kyamba akitoa hukumu kwa mshitakiwa huyo alisema kuwa mahakama imejiridhisha pasipo na shaka ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka na hatimaye kumtia hatiani mshitakiwa kwa kosa hilo.

Sambamba na kifungo cha maisha jela pia hakimu Kyamba amemuhumu mshitakiwa huyo kumlipa mwanafunzi alifanyiwa kitendo hicho fedha kiasi cha Sh milioni 1 ikiwa ni fidia kwa matendo aliyofanyiwa.

Hakimu Kyamba mbele ya  mahakama hiyo ya Wilaya Kakonko ambayo ilifurika idadi kubwa ya wananchi waliokuwa na shahuku ya kujua hatima ya kesi hiyo alisema kuwa hukumu hiyo imetolewa kuwa fundisho kwa watu wengine wanaofanya vitendo vya unyanyasaji kwa watoto wadogo.

Mbele ya mahakama Mwendesha Mashitaka Mkaguzi wa Polisi Wilaya ya Kakonko, Charles Mwakanyamale alisema kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 17 mwaka jana majira ya jioni kijiji cha Kasuga Wilaya ya  Kakonko Kigoma.

Mshitakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 21 baada ya upelelezi kukamilika na kwamba mshitakiwa huyo alikamatwa  akiwa kwenye jitihada za kutoroka.