Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songwe

Mahakama ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe imemhukumu mshtakiwa Stanford Theobert (19), Mkulima, mkazi wa Maporomoko, Tunduma kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 23, 2023 maeneo ya Kata ya Maporomoko Mjini Tunduma ambapo alituhumiwa kumdanganya kuwa atamuoa mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16 na kumbaka jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 130 (2) (e) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura 16 ya mwaka 2022.

Akisoma maelezo ya hukumu ya kesi hiyo yenye kesi namba 23/2023 Hakimu mkazi wa Wilaya ya Momba Timothy Lyon, amesema Mahakama imejiridhisha pasipo na shaka ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri na kumtia hatiani mtuhumiwa kwa kosa la kubaka na kumhukumu adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.

“Mahakama imejiridhisha pasipo na shaka hivyo utataumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa wengine wenye kukatisha ndoto za mtoto wa kike,” amesema hakimu.

By Jamhuri