Jenerali Waitara atafuta mrithi Mlima Kilimanjaro

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi mstaafu, Jenerali George Waitara, ametumia maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru kutangaza rasmi kustaafu kupanda Mlima Kilimanjaro. Waitara amekuwa akipanda mlima huo kwa kipindi cha miaka kumi mfululizo.

Waitara ametangaza azima hiyo wakati wa mkutano wake na wanahabari, mkutano huo aliufanya katika kituo cha Mandara muda mfupi kabla ya kuagana na timu ya wapanda mlima 52 kutoka taasisi mbalimbali, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru wa Tanganyika.

Jenerali Waitara alianza rasmi zoezi la kupanda mlima huo mwaka 2008 akipokea kijiti kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Mirisho Sarakikya, ambaye ameshiriki kupanda mlima huo kwa zaidi ya miaka 30.

Kabla ya kuzungumza na wanahabari, Jenerali Waitara alishiriki zoezi la uzinduzi wa upandaji wa mlima kwenye lango kuu la Marangu na baadaye kuanza safari kuelekea kituo cha Mandara.

Timu hiyo ya wapanda mlima inashirikisha maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanahabari, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, maofisa kutoka Tanapa, Taasisi ya Mkapa Foundation na Chama cha Urafiki wa Tanzania na China.

Jenerali Waitara alitumia mkutano huo kuwahamasisha Watanzania kujenga utamaduni wa kupenda kutembelea vivutio vya utalii ukiwamo Mlima Kilimanjaro, badala ya kuliacha jukumu hilo kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.

“Vivutio vyetu vikitoweka taifa linakosa mapato, ndiyo maana safari hii tumekuja na kaulimbiu isemayo: ‘Uzalendo na ujasiri dira ya kuimarisha utalii Tanzania’,” anasema.

Anasema kupanda Mlima Kilimanjaro ni zoezi la kudumu na ambalo limekuwa likifanywa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kupeleka bendera na kuisimika kwenye kilele cha Uhuru kilichopo umbali wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari kila ifikapo Desemba 9.

Jenerali Waitara anasema baada ya kustaafu kupanda mlima huo atawasiliana na Mkuu wa Majeshi wa sasa, Jenerali Venance Mabeyo, ili kupata mtu sahihi atakayemkabidhi kijiti hicho.

“Ninastaafu kupanda Mlima Kilimanjaro, ninabaki kuwa balozi katika kutangaza na ninaomba watu wasiwe na wasiwasi kwa sababu zoezi hili ni la kudumu na jeshi litaendelea kupeleka bendera yetu hadi kilele cha Uhuru.

Wakati Jenerali Waitara, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), anastaafu kupanda mlima, kuna maboresho kadhaa yamefanywa katika kupanda Mlima Kilimanjaro.

Moja ya mambo aliyoyapigania ni kuboreshwa kwa hali ya usafi na mazingira ya Mlima Kilimanjaro. Mara zote kabla na baada ya kupanda mlima huo alisisitiza suala la utunzaji wa mazingira ikiwamo kutotupa taka hovyo.

Ujenzi mkubwa wa nyumba za kulala wageni pamoja na vyoo vya kisasa katika vituo vya Mandara, Horombo na Kibo kwa wageni wanaotumia lango kuu la Marangu ni moja ya jitihada kubwa zilizofanywa na Jenerali Waitara. Mengine ni hatua yake ya kupigania kuboreshwa kwa masilahi ya wapagazi, wapishi na waongozaji wageni Mlima Kilimanjaro.

Oktoba 30, mwaka juzi, Rais Dk. John Magufuli alimteua Jenerali Waitara kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

 Septemba 15, mwaka huu, Waitara alisherehekea miaka 68 ya kuzaliwa.