Rushwa imevuruga safu ya uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi Mbezi Luis, na sasa viongozi wote wanashikana uchawi, JAMHURI limebaini.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kiwango cha kuaminiana kati ya wabunge wanaoingia kwenye vikao vya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo na watendaji wake kimeshuka mno kutokana na shutuma za rushwa zilizotamalaki kila kona.

“Mradi huu umekuwa zimwi. Fedha zipo kwenye akaunti. Mradi ulipaswa kuanza Septemba, mwaka huu lakini hakuna kinachoendelea kutokana na masilahi binafsi. Tangu Mei, mwaka huu watu wanakaa vikao visivyokwisha. Rais [John] Magufuli amekwisha kuweka fedha kwenye akaunti ya jiji, lakini rushwa imepotosha wengi na hakuna maelewano.

“Lipo kundi linalomtuhumu Mkurugenzi Mtendaji, Mama Sipora Liana, ambaye amekuwa akiwasimamisha wafanyakazi wa Kitengo cha Manunuzi wanaompa ushauri wa kisheria na kuwasweka ndani akidai wamekula rushwa hivyo wanatoa ushauri wenye kuwanufaisha… yeye naye Mkurugenzi Sipora anatajwa kuwa anavunja sheria.

“Wanasema hata akiwa safarini anapiga simu na kuelekeza ajenda ya mradi huu iwepo au isiwepo. Yeye anasikika akisema anasimamia sheria hivyo hawezi kuachia watu wakafanya uamuzi usio na masilahi kwa umma, hivyo anabatilisha uamuzi wa PMU na kusweka ndani watendaji, huku akiwasimamisha kazi wengine na kuwarejesha bila mpangilio. Kimsingi mradi huu umelivuruga Jiji la Dar es Salaam. Ni vurugu tupu,” kimesema chanzo chetu.

Kulingana na nyaraka ambazo JAMHURI limezipata, awali kampuni 17 ziliomba zabuni ya kujenga Stendi ya Mkoa wa Dar es Salaam. Kati ya kampuni hizo, kampuni tatu ndizo zilichaguliwa katika hatua ya awali kwa nia ya kuzishindanisha kupata mshindi wa zabuni Na. LGA/018/2017/2018/W/10. Kampuni zote hizi tatu zilizochaguliwa katika hatua ya awali ni za Kichina, ambazo ni Group Six, Hainnan na CRJE.

Ripoti ya mapitio kwa zabuni zilizowasilishwa na kampuni hizo tatu, ndiyo inayoleta kizungumkuti. “Kampuni ya (jina linahifadhiwa) imekuwa na upungufu unaotia aibu. Kwa mfano haikuonyesha mchanganuo wa gharama, Dhamana ya benki inaonyesha CRDB iliitoa Julai 23, mwaka 2017 ikiwa ni mwaka mmoja kabla zabuni haijatangazwa… na hii kampuni inapigiwa debe la kutisha.

“Mtu aliyepewa Mamlaka ya Kisheria (Power of Attorney) kusaini nyaraka za zabuni za kampuni hii hakuzisaini, badala ya kugonga mhuri wa ofisi amegonga mhuri wa moto, alipaswa kuonyesha makandarasi wasaidizi (sub contractors), lakini hakufanya hivyo. Upungufu wa hivyo hivyo upo kwa kampuni ya pili (jina linahifadhiwa). Tena hii ya pili mamlaka ya kisheria kwa kawaida yanapotolewa na kampuni huwa yanaelezwa kuwa mamlaka hayo yametolewa kwa yeyote anayehusika, wao kwa sababu wanazozijua wakaelekeza mamlaka hayo kwa Mkurugenzi wa Jiji, kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

“Kampuni hii nayo imefanya maajabu ya mwaka, kwani dhamana ya mkopo imetolewa Julai 24, 2018, lakini inaonyesha dhamana hii iligongwa mhuri Julai 23, 2018 ikiwa ni siku moja kabla ya kutolewa dhamana yenyewe, jambo ambalo haliwezekani.

“Hii kampuni nyingine inayotajwa kuwa inabebwa na ofisa anayepewa maelekezo ya mdono na mkurugenzi inaelezwa kuwa imepatia kila kitu, ila kuna wasiwasi kuwa washirika waliwavujishia baadhi ya siri za matakwa ya zabuni mapema hivyo kwa kutumia rushwa wanapata advantage dhidi ya washindani wao. Hii si haki,” kimesema chanzo chetu.

Awali mradi huu ilikuwa ugharimu Sh bilioni 50 zilizotolewa na serikali, lakini mzabuni wa kwanza akaonyesha kuwa kazi hiyo angeifanya kwa Sh 50,698,000,000.00 bila kuonyesha kama gharama hizo zina Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ndani yake au la.

Mkandarasi wa pili kwa mujibu wa nyaraka ambazo JAMHURI limeziona na ambaye kitengo cha ununuzi kilipendekeza apewe kazi ingawa alikuwa na upungufu wa kuonyesha kuwa amepata barua ya dhamana mwaka mmoja kabla ya zabuni kutangazwa, anasema anaweza kuifanya kazi hii ya ujenzi wa stendi kwa Sh 56,999,007,862.00 bila VAT. Hii ina maana ukiongeza VAT gharama inaongezeka kwa asilimia 18.

Mkandarasi wa tatu ambaye anadaiwa kuwa ana gharama kubwa, na kwamba anabebwa na Mkurugenzi wa Jiji naye alitaka alipwe Sh 64,860,367,747.21 bila VAT. Hii ina maana kuwa itaongezeka Sh bilioni 11,674,866,194.49, hivyo kufanya gharama halisi ya mradi kuwa Sh 76,535,233,941.70, badala ya Sh bilioni 50 zilizotolewa na serikali ambazo awali zilitajwa kuwa zinatosha. Jiji linasema kiasi kinachopungua wataongeza fedha kutokana na mapato ya ndani.

“Huu mradi ni pasua kichwa. Kuna madiwani hapa wamekwenda nyumba kwa nyumba kusaka ofisi za kampuni hizi. Katika hizi tatu zilizopitishwa katika hatua ya awali, kuna madiwani wamekula hela kila upande. Sasa najiuliza, tukifika kwenye Bodi ya Zabuni watateteaje kampuni hizi mbili? Wanapita ofisini, wanapiga simu usiku wa manane kuomba zipendelewe, mimi siwaelewi hawa madiwani… baadhi ya wabunge wanafika hatua ya kusema ‘siioni ajenda yangu kwenye kikao cha leo’. Hii ni ajabu,” kimesema chanzo chetu kingine.

Taarifa zinaonyesha kuwa baada ya wataalamu kufanya uchambuzi wa kampuni hizo, kikao cha Bodi ya Zabuni kilikutana kujadili ripoti ya wataalamu, lakini kilishindwa kufanyika kutokana na upungufu mwingi uliojitokeza.

“Baada ya PMU kupitia ripoti na kuandaa taarifa kwa ajili ya kupelekwa kwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni, kikao kiliitishwa lakini hakikufanyika maana hakukuwa na daftari la mahudhurio na hakukuwa na mwandishi wa minutes za kikao hivyo mwanasheria wa jiji akasema kikao ni batili,” anasema mtoa taarifa. Pamoja na kikao hiki kuahirishwa, wajumbe wake walilipwa posho za kikao.

Tangu mwezi Mei mwaka huu, Bodi ya Zabuni imekwisha kukutana mara sita na wajumbe wake wamekuwa wakilipwa posho, lakini hakuna uamuzi wowote wa msingi walioufanya. Hata wiki hii taarifa zinaonyesha kuwa wamepanga kukutana tena.

Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana, anadaiwa kuingilia mchakato wa zabuni hiyo kwa kutoa maagizo kwa Ofisa wa Kitengo cha Ugavi yenye kuwa na upendeleo kwa kampuni moja, ambapo chanzo kingine kimesema: “Kila kitu kinachofanywa sasa kuhusiana na mradi huu kinafanyika kwa matakwa ya Mkurugenzi wa Jiji na si kwa mujibu wa sheria ya manunuzi.”

JAMHURI limefanya mahojiano na Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana, aliyesema: “Anayenituhumu naomba apeleke malalamiko yake TAKUKURU. Huu mchakato ni siri, na bado upo katika hatua za ndani siwezi kuuzungumzia. Naona watu wenye masilahi binafsi wanahaha wanapoona wanayoyataka hayatekelezeki. Namshukuru Rais [John] Magufuli kwa kuendelea kusimama na sisi tunaotetea haki. Sitaruhusu mambo ya hovyo katika mradi huu. Katika hili sina hofu yoyote kwa maana sijachukua hata senti tano ya mtu, hivyo ninyi chapisheni tu gazetini.”

JAMHURI limemtafuta Mwanasheria wa Jiji, Jumanne Mtinangi, kupata ufafanuzi kuhusiana na mradi huo, lakini amesema yeye hawezi kuzungumzia suala hilo kwani mwenye mamlaka ni Mkurugenzi wa Jiji. “Hilo labda umuulize Mkurugenzi wa Jiji, kwani ndiye Msemaji wa taasisi. Yeye ndiye mwenye mamlaka ya kulisemea hilo kwa uhakika,” amesema Mtinangi.

Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi, Vumilia Tigwela, amesema yeye binafsi hawezi kuzungumzia suala hilo kwani si Msemaji wa Jiji. “Ndugu yangu naomba uwasiliane na mkurugenzi ndiye mtu sahihi anayeweza kukwambia lolote kuhusu mradi. Mkurugenzi ndiye mwenye mamlaka ya kuisemea taasisi,” amesema Vumilia.

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, amezungumza na JAMHURI kuhusiana na mradi huu akasema anasikitishwa kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa stendi ya mkoa. Alipoulizwa kuhusiana na tuhuma za rushwa kwenye mradi huu amesema hajasikia suala hilo kwani bado halijafikishwa kwenye vikao vya madiwani.

“Hili suala lingekuwa limefika kwenye vikao likajadiliwa ningekuwa na la kusema kwani huko ndiko yanapoibuka yote unayoniuliza. Lakini mradi huu ni muhimu kwa Watanzania, hivyo natarajia kuwa hautacheleweshwa zaidi,” amesema Kubenea.

Meya wa Manispaa ya Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, alipoulizwa kuhusiana na suala hilo amesema mradi huo upo chini ya jiji, hivyo hawezi kuuzungumzia.

Alipoulizwa kuhusiana na taarifa za yeye binafsi kuhusishwa na rushwa katika mchakato wa upatikanaji wa mkandarasi wa mradi huo, amesema hawezi kuwa na masilahi binafsi katika mradi huo kwani kampuni zilizoomba zabuni ni za Kichina. “Masilahi niliyonayo ni ujenzi wa kituo hicho, ni kuwa upo eneo la Ubungo. Hayo mengine unayosema siyajui,” amesema Meya Jacob.

Mei mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, aliwaonya watu ambao hujinufaisha kupitia miradi ya maendeleo. Jafo alifika Mbezi Luis na kufanya ukaguzi wa eneo linalotakiwa kujengwa kituo cha mabasi ya mikoani na kusema serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaokiuka taratibu.

“Sitarajii kuwaona watu wajanja wajanja wakija kujinufaisha katika huu mradi wa stendi ya mabasi ya mikoani. Baadhi ya watu wanapoona miradi mikubwa huwa wanapanga mikakati ya kuhujumu au kujipatia fedha kwa kufanya ufisadi,” alisema Jafo.

Please follow and like us:
Pin Share